Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba juzi alijikuta akitamka kuwa anakusudia kufuta maadhimisho mbalimbali ya kitaifa yanayotumika kama kichaka cha kutafuna fedha za Serikali baada ya wabunge wa upinzani kuitoa jasho Serikali wakati wa kupitisha Muswada wa Sheria ya Baraza la Vijana wa mwaka 2015.
Mwigulu alitoa kauli hiyo pale alipoingilia kati mjadala huo, akiponda kitendo cha watumishi wa Serikali kutumia magari na fedha lukuki katika wiki za kuadhimisha kumbukumbu mbalimbali za kitaifa.
Kilichoibua mjadala huo ni suala la uanzishwaji wa Mfuko wa Vijana na maadhimisho ya wiki ya vijana ambayo imepangwa Oktoba kila mwaka.
“Napendekeza wiki hii (ya Mfuko wa Vijana) iondolewe mwezi Oktoba kwa sababu ndani ya wiki hiyo pia kuna maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere na kuhitimisha mbio za mwenge,” alisema Mbunge wa Ubungo (Chadema), John Mnyika.
Kauli ya Mnyika iliungwa mkono na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu aliyesema si jambo la busara kuiweka siku hiyo sawa na kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu Nyerere.
“Kila mtu hapa anajua jinsi siku ya kilele cha mwenge yanavyofanyika mambo mabaya. Hatulitaki jambo hili,” alisema Lissu.
Msimamo huo ulimnyanyua Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia na kusema kuwa hata Mwalimu Nyerere alikuwa kijana wakati akifanya harakati za kulikomboa Taifa, si vibaya kama Wiki ya Vijana ikaadhimishwa mwezi huo.
Kwa nyakati tofauti Mawaziri Jenister Mhagama, Mary Nagu, Dk Fenella Mukangara na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju walisimama kuitetea hoja hiyo bila mafanikio.
Wakati mvutano ukizidi kuwa mkali, alisimama Mwigulu na kusema: “Mimi nina mawazo tofauti kidogo. Nadhani umefikia wakati wa kufikiri tofauti na kuachana na hizi kumbukumbu za wiki ya maafa, wiki ya mtoto wa jicho, wiki ya kichaa cha mbwa, wiki ya maziwa, sijui kunyonyesha… sijui wiki ya nini. Nikiwa...”(akakatishwa na Mwenyekiti wa Bunge Zungu).
Mwigulu alisema katika maadhimisho hayo watumishi wa Serikali hutumia mamilioni ya fedha na magari ya Serikali kushiriki, kuifanya Serikali kutumia fedha nyingi katika mambo ambayo si ya msingi sana.
“Kuna maadhimisho Mtwara watendaji kutoka Mwanza wanakwenda. Sijui kuna shughuli Kigoma watu wanatoka Dar es Salaam. Tufikie wakati tuachane na hizi wiki na tubaki na maadhimisho ya muhimu,” alisema.
Akifafanua baadaye jana, Mwigulu alisema, “Nililenga kuonyesha jinsi fedha zinavyotumika hovyo. Unajua katika maadhimisho haya, watu wanatengeneza fulana, kofia na mambo mengine mengi. Sidhani kama ni sahihi.” Alisema kuna mambo mengi ya msingi yanayohitaji kufanyika lakini fedha zinakosekana, kama maadhimisho ya wiki yakiangaliwa kwa umakini, fedha nyingi zinaweza kuokolewa.
Alipoulizwa alitaka kusema nini aliposema niki... alisema kuna kitu alitaka kusema lakini hakumalizia, ingawa hoja yake ilikuwa kusisitiza kuwa fedha nyingi za Serikali zinatumika vibaya katika maadhimisho hayo.
Hata hivyo, pamoja na kauli hiyo, Mwigulu alipohitimisha kauli hiyo bungeni alipondwa na Lissu na Mnyika wakisema kuwa kauli yake haikutakiwa kutolewa na mtu kama yeye, kwamba licha ya kuwa ni waziri mdogo, pia anataka kugombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Mvutano huo haukufikia mwafaka na kumlazimisha Zungu kulihoji Bunge kama linakubaliana na hoja ya wapinzani. Kutokana na wingi wa wabunge wa CCM, hoja ya Serikali ya kuanzisha mfuko katika baraza hilo iliungwa mkono.
Hata hivyo, baadhi ya watu wametafsiri kuwa Mwingulu aliposita na kutamka nikiwa.. alitaka kusema nikiwa Rais.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment