ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 12, 2015

PINDA - WATANZANIA WAISHIO NJE KUTOPIGA KURA OKTOBA

*Waziri Mkuu aomba Watanzania waiombee nchi yao. (Picha na Maktaba yetu)

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Watanzania waishio ughaibuni hawataweza kupiga kura wakiwa nje ya nchi kwenye uchaguzi wa Oktoba mwaka huu, kwa sababu kuna mambo kadhaa ambayo Serikali inabidi iyatekeleze kabla ya zoezi hilo kufanyika.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Jumamosi, Aprili 11, 2015) wakati akizungumza na baadhi ya Watanzania waishio Uingereza kwenye makazi ya Balozi wa Tanzania nchini humo, Balozi Peter Kallaghe, yaliyoko Highgate, Kaskazini mwa Jiji la London.

Akizungumza na Watanzania hao ambao baadhi yao walitoka miji ya Leicester na Manchester, Waziri Mkuu alisema mambo makuu ambayo yanahitaji kuzingatiwa kabla hawajaweza kupiga kura ni pamoja na marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi Na. 1 ya mwaka 1985 pamoja na uandikishwaji wa Watanzania wana-Diaspora kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

"Najua suala kubwa ambalo mnatamani kulisikia ni hili la Watanzania kuweza kupiga kura kutokea huku mliko. Hili inawezekana lisifanikiwe wakati huu kwa sababu kuna mambo muhimu ya kuzingatia kubwa likiwa ni marekebisho ya sheria na hili zoezi la uandikishaji wapigakura kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura. Ili mwananchi aweze kupiga kura ni lazima awe ameandikishwa kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura," alisema.

"Itabidi tuangalie kama mashine za BVR nazo zitapaswa kupelekwa kwenye kila ubalozi ili watu wetu waweze kujiandikisha au itafutwe njia nyingine ya kufanikisha hilo jambo.... lakini watu wa Tume wanaamini kwamba jambo hilo linaweza kufanikiwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2020," aliongeza.

Waziri Mkuu ambaye aliwapatia nakala zisizopungua 40 za Katiba Inayopendekezwa, alitumia fursa hiyo kuwasisitizia wasome kwa makini Katiba hiyo ili wawe na uelewa mpana na kisha wailinganishe na Katiba ya mwaka 1977 ambayo inatumika hivi sasa ili waweze kubaini kama kweli haina kitu kama ambavyo watu wengine wanadai.

"Moja ya changamoto zinazotukabili huko nyumbani ni mjadala kuhusu Katiba Inayopendekezwa,wako watu wanaosema kwamba hakuna kitu kipya kabisa kwenye Katiba Inayopendekezwa, lakini mimi nasema hayo ni mawazo yao binafsi," alisema.

Akifafanua kuhusu Katiba hiyo, Waziri Mkuu alisema: "Mimi nilikuwa sehemu ya Bunge Maalum la Katiba, ni kweli tulibadili baadhi ya vipengele lakini kwa nia ya kuiboresha. Ninawasihi kila mmoja wenu aisome na kuangalia kama kweli hamna kitu au kuna kitu kipya ikilinganishwa na Katiba inayotumika hivi sasa. Angalieni na pimeni, je kuna kitu kimeboreshwa au la?"

Aliwasihi waendelee kuiombea nchi ya Tanzania ili iendelee kuwa na amani na utulivu na hasa katika kipindi hiki ambacho inakabiliwa na uchaguzi wa madiwani, wabunge na Rais. "Ninawasihi muendelee kuiombea nchi yetu ili ipate viongozi wazuri ambao watajali maslahi ya wengi," aliongeza.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAPILI, APRILI 12, 2015.

4 comments:

Anicetus said...


Kama Banki za Tanzania Zinaweza kufungua account za watanzania walioko ugaibuni-diaspora- kwanini serikari hawezi kunandikisha wapiga kura waishio ugaibuni -Diaspora.

Maisha ya sana ni ya electronic na Mheshimiwa pinda asituchangayishe akili kwa kutumia katiba ya 1977 na ya 2015.
Hakuna mtanzania anayenyimwa haki ya kupiga kura duniani. Mfano- wamarekani na wayahudi wana piga hura popote wanakoishi duniani.

Anonymous said...

...KAFARA ZIMEZIDI "YARABI TOBA" MNYAANZ MUNGU TUNUSURU NA UCHAGUZI HUU MBELE YETU...

Anonymous said...

Huko kote kunasababishwa na Serikali kukosa seriousness. Inasemekana wakati wa kupitisha hii Katiba Inayopendekezwa, Serikali iliwafuata baadhi ya wajumbe wa Bunge la Katiba waliokuwa Uarabuni kwenye hija na wakapiga kura huko huko. Hilo liliwezekana kwa sababu ya maslahi ya watawala katika hiyo Katiba Inayopendekezwa. Viongozi acheni visingizio na sababu zisizo na mashiko!

Anonymous said...

Siasa za Tanzania zinachekesha.Mwanasiasa mmoja, jambo moja majibu matatu tofauti!