ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 14, 2015

SAME MASHARIKI: HUDUMA ZA KIJAMII ZINAVYOWATESA WANANCHI

Rais Jakaya Kikwete akiwa na Mbunge wa Same kwa tiketi ya CCM, Mh. Anne Kilango Malecela.
Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Abdulrahman Kinana na Mh. Anne Malecela.

Same ni moja kati ya wilaya saba zinazounda Mkoa wa Kilimanjaro, upande wa Kaskazini ikipakana na Wilaya ya Mwanga, Kaskazini Mashariki ikipakana na nchi ya Kenya, Kusini na Kusini Mashariki ikipakana na Tanga na Magharibi ikipakana na Manyara.

Ndani ya Wilaya ya Same, linapatikana Jimbo la Uchaguzi la Same Mashariki, linaloongozwa na Mheshimiwa Anne Kilango Malecela kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, Uwazi lilifunga safari mpaka jimboni humo na kufanya ziara katika kata mbalimbali ambapo lilizungumza na wananchi walioeleza matatizo yanayowakabili na jinsi mheshimiwa mbunge anavyozishughulikia kero zinazowakabili.

MATATIZO YA WANANCHI
“Elimu jimboni kwetu ni tatizo ndugu mwandishi, jimbo letu limekuwa likifanya vibaya katika matokeo ya mitihani ya taifa hasa kidato cha nne, shule zetu za sekondari hazina walimu kwani wanaopangiwa wakija huku huwa hawakai, wanaondoka na kusababisha watoto wetu wakose haki yao ya msingi ya kufundishwa, tunaomba serikali yetu itusaidie,” alisema Nicodemus Mgonja, mkazi wa jimbo hilo.

Naye Barikieli Mbwambo, mkazi wa Kihurio, alisema jimbo hilo lina uhaba mkubwa wa sekondari za kidato cha tano na sita, jambo linalowanyima fursa watoto wao wanaohitimu kidato cha tano na sita kuendelea na elimu ya juu.

“Wakati mwingine wanafunzi hata hawafanyi juhudi kwenye masomo kwa sababu wanajua wakishahitimu kidato cha nne, hakuna shule za kuwafanya waendelee mbele, pia kuna uhaba wa madawati na madarasa, tunamuomba mheshimiwa mbunge atusaidie,” alisema.

Kwa upande wa sekta ya afya, wananchi waliozungumza na Uwazi walieleza kuwa kuna matatizo ya ukosefu wa huduma za uhakika za afya jimboni humo, yakiwemo madawa na wauguzi, huku pia ikielezwa kuwa katika jimbo hilo, hakuna hospitali kubwa hata moja.

“Kama unaumwa au una mgonjwa wako amezidiwa, unalazimika kumsafirisha mpaka Same Mjini, huku kwetu hakuna hospitali zaidi ya zahanati na vituo vya afya, tunaomba na sisi tukumbukwe jamani,” alisema Chediel Mchome.

Suala la ubovu wa miundombinu, pia ni miongoni mwa matatizo yaliyotajwa na wananchi wa jimbo hilo la Same Mashariki, ambapo Barabara Kuu ya Mkomazi- Gonja- Same, licha ya ahadi za mara kwa mara za kujengwa kwa kiwango cha lami, hadi leo suala hilo halijatekelezwa, jambo linalotajwa kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi.

Uharibifu wa vyanzo vya maji, ni tatizo lingine lililotajwa na wananchi waliozungumza na Uwazi ambapo wameeleza kwamba baadhi ya watu, hufanya shughuli za kibinadamu kandokando ya vyanzo vya maji, jambo linalohatarisha vyanzo hivyo, huku kukiwa hakuna juhudi zozote zinazochukuliwa kuwadhibiti. Pia uharibifu wa misitu, ukiwemo wa Shengena, umesababisha mabadiliko ya hali ya hewa jimboni humo, jambo linalosababisha wananchi wanaotegemea kilimo waishi kwa hofu.

“Zamani tulikuwa tunategemea mvua za vuli na masika kwa ajili ya kilimo lakini kutokana na uharibifu wa mazingira, siku hizi hakuna mvua za kueleweka, jambo linalosababisha mazao yetu yanyauke, hata kama mvua zikinyesha, basi zinasababisha maafa makubwa ikiwemo maporomoko ya ardhi,” alisema Yunus Kathera, mkazi wa jimbo hilo.

Pia kuna tatizo lingine la ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana.
“Sisi vijana tunahangaika huku wengi wetu hatuna kazi. Tunamshukuru mbunge wetu kwa kufanikisha kujengwa kwa kiwanda cha kusindika tangawizi ambapo vijana wengi wamepata ajira. Pia tunampongeza kwa kufanikisha kujengwa kwa Chuo cha VETA Maone kinachomilikiwa na kanisa, wengi tutanufaika, tunampongeza mheshimiwa mbunge,” alisema Sospeter Makange, mkazi wa jimbo hilo.

MAELEZO YA MBUNGE
Baada ya kusikia maelezo ya wananchi, Uwazi lilimtafuta Mheshimiwa Anne Kilango kwa njia ya simu ambapo alipopatikana, mwandishi wetu alimsomea matatizo ya wananchi na kumuuliza hatua alizochukua ambapo katika hali ya kushangaza, mheshimiwa huyo alikata simu.Uwazi halikuishia hapo, lilimtumia kero zote za wananchi kwa njia ya ujumbe mfupi wa maandishi ambapo alijibu kwa kifupi: “Nitashughulikia yote msijali.”

GPL

No comments: