Advertisements

Friday, April 17, 2015

TANZANIA YASHIRIKI KATIKA MKUTANO WA KAMISHENI KUHUDU IDADI YA WATU NA MAENDELEO


Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi akizungumza wakati wa Mkutano wa 48 wa Kamisheni ya Idadi ya Watu na Maendeleo, Tanzania ni mjumbe wa Kamisheni hii ikiwa ni kati ya nchi 12 kitoka Afrika zikiliwakilisha Bara ya Afrika. pamoja na naye ni Bw. Seif Shaban Mwinyi, Kamishna wa Mipango kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Bw. Stephen Kiberiti kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii


Sehemu wa Wajumbe kutoka nchi 47 zinazounda Kamisheni ya Idadi ya Watu na Maendeleo. wajumbe wa kamisheni hii, 12 wanatoka nchi za Bara la Afrika , 11 kutoka Bara la Asia na Pacific, 5 kutoka nchi za Ulaya Mashariki, 9 wanatoka Latini ya Amerika na Visiwa na Karibiani, na 10 wanatoka Nchi za Ulaya Magharibi na Mataifa mengine. Wajumbe hawa huchaguliwa na Baraza Kuu la Uchumi la Umoja wa Mataifa ( ECOSOC).


Bi. Samira Diria, Afisa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa KImataifa, na Bi. Esther Suvi kutoka Kamisheni ya Mipango, ambao ni sehemu ya Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 48 wa Kamisheni kuhusu Idadi ya watu na maendeleo wakifuatilia majadiliano ya jumla

Na Mwandishi Maalum, New York

Mkutano wa 48 wa Kamisheni kuhusu idadi ya watu na maendeleo (CPD) unaendelea hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, ambapo wajumbe kutoka nchi 47 zinazounda Kamisheni hiyo wamekuwa wakibadilishana mawazo, uzoefu na namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali kuhusu dhima nzima ya idadi ya watu na maedeleo

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kati ya nchi 47 zinazounda Kamisheni hiyo ikiwa miongoni mwa nchi 12 zinazoiwakilisha Bara la Afrika, wajumbe wa Kamisheni hiyo wanachaguliwa kikanda, ambapo Afrika inawajumbe 12, Asia na Pacific ikiwakilishwa na nchi 11, Bara la Ulaya likiwakilishwa na nchi 5, Bara la Amerika na Visiwa vya Karibian likiwakilishwa na nchi 9 wakati kundi la nchi za Ulaya Magharibi na Mataifa mengine likiwakilishwa na nchi 10.

Majadiliano ya jumla ya mkutano huu wa 48 yamejielekeza zaidi katika kuelezea uzoefu wa kila nchi katika eneo hilo la idadi ya watu na maendeleo mkazo ukiwa namna gani masuala ya idadi ya watu na maendeleo yanavyoweza kuingizwa katika suala zima la maendeleo endelevu hususani baada ya mwaka 2015.

Ujumbe wa Tanzania katika Mkutabo huu unawahusisha wawakilishi kutoka Wizara ya Afya, kamisheni ya Mipango, Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, na Asasi isiyo ya Kiserikali inayohusiana na masuala ya Vijana.

Pamoja na kubadilishana uzoefu wa kitaifa kuhusu masuala ya idadi ya watu na maendeleo na namna gani nchi wanachama zinavyotekeleza mipango mbalimbali ya maendeleo, wajumbe wa mkutano huu pia wamepata fursa ya kupata taarifa za kitaalamu kutoka kwa wasomi na watafiti waliobobea katika maeneo ya idadi ya watu, maendeleo, ajira, takwimu, mazingira na mabadiliko ya tabia nchi pamoja na mambo mengine.

Akizungumza wakati wa majadilino ya jumla, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Katika Umoja wa Mataifa, Balozi Ramadhan Mwinyi, amesema, masuala ya idadi ya watu na maendeleo ni moja ya ajenda muhimu kwa Tanzania na kwamba Tanzania iko katika mchakato wa kufanya marejeo ya sera ya taifa ya idadi ya watu kwa lengo la kuimarisha mifumo ya takwimu.

Vile vile amesema katika kipindi cha mpito baada ya 2015 ambao ndio mwisho wa utekelezaji wa malengo ya maendeleo ya millennia, ni kipindi kinachokwenda sambamba na muhula wa pili wa mpango wa miaka mitano wa maendeleo ambapo unalenga katika mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye uchumi wa kati kupitia visheni 2025.

Akabainisha kuwa ili kufikia azma hiyo, serikali imejipanga kushirikiana na wadau kutoka sekta mbalimbali yakiwamo mashirika yasiyo ya kiserikali.

Uwezeshwaji wa wanawake ni moja ya eneo ambalo Tanzania imeelezea kama moja ya vipaumbele vyake katika suala zima la idadi ya watu na maendeleo. Pamoja na changamoto ya kukabili tatizo la ajira kwa vijana .

Na kwa sababu hiyo, Balozi Radhani Mwinyi asema, Serikali imejiwekea mikakati na mipango inayolenga katika kuwawezesha wanawake na vijana kiuchumi.

Kwa upande wa eneo la huduma za afya, amesema serikali imejiwekea mipango na mikakati inayolenga katika kusambaza huduma za afya kwa wananchi wake, zikiwamo afya ya uzazi, upunguzaji wa vifo vya watoto wachanga na wanawake wajawazito, elimu ya jumla kuhusu masuala ya uzazi na haki za binadamu.

Tanzania katika mchango wake imesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa kikanda kwa madhmuni ya kubadilishana, kuhabarishana na kuelimishana pamoja na kubadilishana uzoefu kuhus masuala mtambuka yakiwano ya maendeleo endelevu na uhusiano wake na idadi ya watu

No comments: