Rais Jakaya Kikwete.
ZAKAYO PETER, MBEYA
Nakupongeza Mh. JK kwa kusimamia utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM, ila kabla hujaondoka madarakani naomba ututimizie wananchi wa Kamsamba utujengee daraja la kutuunganisha na wananchi wenzetu wa Mkoa wa Rukwa katika Mto Momba kama ulivyotuahidi Oktoba 31, mwaka 2009 ulipofanya ziara ya kikazi huku kwetu.
ANDREA KAYOMBO, NJOMBE
Mh. Rais, hizi vurugu za Mbeya maeneo ya Tunduma na Mwanjelwa hujazisikia maana ni shida kwa wanyonge wanashindwa kufanya shughuli zao kwa ufasaha, kikubwa nakupongeza kwa kulifanya taifa kuwa na utulivu na amani ila kama rais unayetoa madaraka ujue kuna mambo ambayo yatakuja yavuruge amani hapo baadaye, kama hili kundi la vijana wasomi wakati ajira bado ni ndoto na hata hao wanaojiita panya road wamekosa ajira ndiyo maana wanafanya hayo.
NSAJIGWA EDWIN, MBEYA
Kwanza nikushukuru kwa uongozi bora uliouonyesha ambao unaweza kuwa mfano wa kuigwa kwa kiongozi ajaye, ushauri wangu napenda ututafutie kiongozi bora kama ulivyo wewe kwa kuwa huna makuu.
JOSHUA MWAKILONGA, DAR
Nakupongeza rais wangu kwa mazuri yote uliyotufanyia Watanzania, japo umekumbana na mengi lakini kuna vijana wengi hapa nchini ambao hawana ajira, ningeomba ulitazame kwa kina hili wimbi kubwa la vijana wasiokuwa na shughuli maalum za kufanya ikibidi waende Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) wapate ajira.
SALMATA SAIDI, DAR
Shikamoo baba JK, mimi ni mnyonge lakini tunakuomba uendeshe gurudumu sawasawa ili lisitokee tatizo lolote, ni bora tukawa maskini lakini tunaamani, utulivu na umoja, na kusisitiza tu uchague kiongozi aliye bora atakayefuata nyayo zako inabidi uwe makini na vyama pinzani kuhakikisha tunakaa mbali na maswala ya vita.
PETER THOMAS, MARA
Nakushukuru kiongozi wetu kwa kuiongoza vizuri nchi yetu katika nyanja mbalimbali, ni kweli hakuna kiongozi aliyekamilika hivyo hata katika utendaji wako huwezi kutenda mazuri asilimia 100, japo kuna mengi yanakusonga tupilia mbali hili la ajira kwa vijana ni janga la taifa na pamoja na hilo nchi yetu hii tunajivunia kutokana na kuishi kwa amani lakini hili swala la mauaji ya hawa ndugu zetu Albino inabidi upambane nalo kwa juhudi zote na kuondokana nalo.
PIUS PATRIC, SHINYANGA
Nakupa pole na majukumu rais wangu, najua si kazi ndogo kuliongoza taifa letu umejitahidi kulitumikia vyema taifa hili kwa kipindi chote cha miaka kumi na tulikuzoea, kwa kuwa ni kiongozi mnyenyekevu unayependa kucheka na watu japo wapo watakao kusema vibaya, jitahidi kurekebisha yale mapungufu machache ambayo yapo ndani ya uwezo wako kwa kipindi hiki kifupi ulichobakiza madarakani.
SHARIFA MDIRIKO, MTWARA
Binafsi sijavutiwa kabisa na uongozi wako tangu ulipoingia madarakani mpaka sasa unakaribia kumaliza muda wako, kwa kuwa kuna mambo mengi umeshindwa kuyatekeleza vile inavyostahiki na sioni haja ya kuyataja, maana yapo wazi kwenye jamii kuna mambo mengi yameendelea kuwa tatizo kwenye taifa hili kwa ujumla.
KASSIM MTWEVE, NJOMBE
JK umetusahau sana Kijiji cha Mdilidili Wilaya ya Ludewa, ulisema ajira kwa vijana lakini mpaka leo kimya na unakaribia kuondoka madarakani, tunakuomba uje kututembelea na kututimizia angalau yale machache uliyotuahidi tuwe tumeambulia matunda ya uongozi wako na kutuacha tukiwa na mioyo safi bila kinyongo kwa ahadi ulizotupa.
DAUDI MPENZWA, MKURANGA
Nakupongeza rais wetu umetufanyia mambo mengi makubwa Watanzania, umeingia kwenye orodha ya marais wanaopendwa na wananchi, ila kuna jambo moja umetusahau sisi watu wenye matatizo ya ulemavu katika Chama cha Viziwi Tanzania (Chavita) tunahitaji sana faraja yako kiongozi wetu.
EMMANUEL RORYA, MARA
Kwa bahati mbaya Watanzania ni taifa pekee duniani ambao hata ukiwafanyia jema gani hawaoni na pale utakapoondoka madarakani ndiyo tutagundua umuhimu wako, tofauti na Baba wa Taifa, Julius Nyerere hakuna atakayekumbukwa sana zaidi yako, tunaweza kukubeza lakini tutakukumbuka sana kutokana na mengi mazuri uliyoyafanya kadiri Mungu alivyokujalia, nikushauri tu uwe muangalifu kwa wagombea urais wa CCM usielemee upande wowote ule na uwe makini sana ili chama kisigawanyike.
No comments:
Post a Comment