Naibu waziri wa Afya wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mahamoud Thabiti Kombo amesema bodi ya Chakula, Madawa na Vipodozi inajenga maabara ya kisasa ya uchunguzi wa madawa , chakula na vipodozi ambayo itakuwa na ubora wa Kimataifa.
Hayo ameyasema leo huko Baraza la Wawakilishi nje kidogo ya Mji wa Zanzibar wakati akijibu swali la Mwakilishi wa Jimbo la Muyuni Mhe. Jaku Hashimu Ayoub aliyetaka kujua kwamba bodi ya Chakula, Madawa na Vipodozi ni taasisi muhimu kwa afya za binaadamu, kwanini Wizara haifikirii kuipa ruzuku na lini watawapa ruzuku hizo.
Alisema ruzuku ya bodi hiyo itapatiwa katika bajeti ijayo na zaidi ya milioni 70 zimetengwa kuipa bodi hiyo ili kuyafikia mahitaji yao ikiwa pamoja na ujenzi huo wa maabara.“Hivi sasa bodi wana tengeneza laborali ya kisasa inayoweza ushindani kuvipima vyakula vinavyoingia nchini”,alisema Naibu Waziri huyo.
Aidha Naibu Waziri huyo alisema kuwa hakuna ruhusa ya chakula, dawa na vipodozi kuingia dukani bila ya bodi hiyo kuvifanyia uchunguzi wa kimaabara na pale vitu hivyo vinapobainika kuwa ni vibovu ndio bodi huchukua jukumu la kuviangamiza.“Inapobainika kuwa chakula, Madawa na vipodozi ni vibovu basi mmiliki hupigwa faini kwanza na baadae hulazimika alipie kazi ya uangamizaji”, alisema Mahamoud.
Wakati huo Naibu Waziri huyo kwa niaba ya Waziri wa Afya alitoa tarifa fupi ya dharura juu ya ukosekanaji wa maji katika Hospitali ya Mnazi Mmoja ambayo ilileta usumbufu mkubwa hospitalini hapo.Hata hivyo alisema huduma hiyo tayari imeshapatiwa ufumbuzi kwa ushirikiano na mafundi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar ambapo huduma hiyo inapatikana bila ya usumbufu.
IMETOLEWA NA IDARA YA HABARI MAELEZO- ZANZIBAR
No comments:
Post a Comment