Yawataka wanachama kujitokeza kuchukua fomu, Wagombea urais kuchujwa Ukawa.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe.
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimetoa ratiba kwa wanachama wake wanaotaka kugombea udiwani, ubunge na urais kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa Oktoba, 2015 kujitokeza kuchukua fomu.
Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe, alitangaza ratiba hiyo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dar es Salaam kuhusiana na maazimio yaliyofikiwa na Kamati Kuu ya chama hicho katika mkutano wake wa siku mbili.
Mkutano huo ulifanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Jumapili hadi juzi.
UDIWANI
Alisema uchukuaji na urejeshaji wa fomu za udiwani katika kata ambazo Chadema hakina madiwani utaanza Mei 18 hadi Juni 25, mwaka huu wakati kwa kata ambazo chama hicho kina madiwani utaanza Julai Mosi hadi Julai 20 mwaka huu.
Mbowe alisema uteuzi wa mwisho wa wagombea udiwani wa kata pamoja na viti maalum ambao utafanywa na Kamati Tendaji za Majimbo, utafanyika Julai 15 hadi 20 mwaka huu.
UBUNGE
Mbowe alisema kuchukua na kurejesha fomu za ubunge wa majimbo na ubunge wa viti maalum katika majimbo ambayo Chadema hawana wabunge uchukuaji fomu na urejeshaji fomu utaanza Mei 18, hadi Juni 25, mwaka huu.
Kwa upande wa majimbo ambayo Chadema ina wabunge kwa sasa utafanyika Julai 6 hadi 10, mwaka huu na uteuzi wa awali wa wagombea ubunge utafanyika kati ya Julai 20 na 25, mwaka huu.
Mwenyekiti huyo alisema uteuzi wa mwisho utakuwa kati ya Agosti 1 na 2, mwaka huu.
URAIS
Kuhusu urais, Mbowe alisema kuchukua na kurejesha fomu kutafanyika kati ya Julai 20 na 25, mwaka huu na Agosti 3 na 4, mwaka huu vikao vya Baraza Kuu la Taifa na Mkutano Mkuu wa Taifa wa Chadema vitakutana.
Alisema wanachama watakaochukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania urais mwaka huu, watapelekwa kwenye mchujo wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) na kupatikana mgombea mmoja atakayesimama kwa niaba ya vyama vinavyounda Ukawa.
Vyama vinavyounda Ukawa ni Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR-Mageuzi na National League for Democracy (NLD).
UCHAGUZI MKUU
Mbowe alisema Kamati Kuu ya Chadema imeazimia kuwa uchaguzi mkuu wa mwaka huu lazima ufanyike Oktoba kwa mujibu wa katiba na kwamba Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) isijiandae kutumia kisingizio chochote kuuahirisha kwa sababu uchaguzi siyo jambo la dharura.
Alisema Serikali ya CCM chini ya Rais Jakaya Kikwete iache hila zozote za kutaka kujiongezea muda wa kukaa madarakani ikiwamo kutaka kupeleka Muswada wa Marekebisho ya Katiba Bungeni ili kujihalalishia kuongeza uhai wa Serikali.
Hata hivyo, Rais Kikwete mara kadhaa amekanusha kuwapo mipango ya kujiongezea muda.
Ijumaa iliyopita wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani kitaifa mkoani Mwanza, alisema uchaguzi huo wa madiwani, wabunge na rais utakaovishirikisha vyama vingi vya siasa nchini utafanyika Oktoba.
SEKTA YA USAFIRI
Mbowe alisema Kamati Kuu ilipokea, kujadili na kutafakari hali halisi ya sekta ya usafirishaji nchini na kubaini udhaifu mkubwa ambao unatokana na usimamizi dhaifu wa watu waliopewa dhamana kusimamia sekta hiyo kuanzia Waziri wa Uchukuzi, Samuel Sitta.
Alisema kutokana na viongozi waliopewa dhamana kutokuwa makini hali hiyo imesababisha sekta hiyo kukosa mwelekeo na kusababisha madhara mengi kwa wananchi kutokana na ajali za mara kwa mara zinazotokea barabarani na majini.
Kuhusu mgomo wa madereva wa mabasi, alisema Kamati Kuu imeunga mkono madai ya madereva kwani ni halali na hivyo lazima serikali iyatekeleze badala ya kuyapuuza na kusababisha migomo isiyoisha.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment