ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 11, 2015

HERI KUPENDWA KULIKO MAUMIVU YA KUPENDA!

Ni Jumatatu nyingine ambayo tunakutana tena katika kilinge hiki cha XXLove tunachokitumia kuelimishana masuala ya mapenzi. Katika suala la uhusiano wa kimapenzi ni vigumu sana kujikuta mwanamke na mwanaume mkipendana kwa 100%. Ila ni rahisi mno kwa mmoja wenu kumpenda mwenza wake kwa asilimia zikaribiazo 100. Hata kama mmoja akipenda kwa asilimia mia moja na kumshawishi mwingine, ni nadra kwa ulimwengu wa sasa kuwakuta wapenzi ambao kila mmoja anampenda mwenzake kwa asilimia mia moja.

Ikiwa mwanamke anampenda sana mumewe basi mwanaume atakuwa na matatizo ya kianasaanasa, hata kwa mwanaume anayempenda mkewe basi sehemu kubwa mkewe anakuwa ana shida.

Mpenzi msomaji, asikudanganye mtu kupendwa kuna raha yake, tena mno kuliko kupenda. Unapopendwa una nafasi kubwa ya kufanya chochote unachotaka kama vile kudeka, kujishebedua, kuzira, kulazimisha kisichokubalika na kukubalika n.k.

Kwa wale wanawake wajanja hii ndiyo huwa sehemu ya kutusua kwa maana ya kufanya vitu vya maendeleo akijua kuna jamaa kamshika kwa sababu kazimika basi anatumia mwanya huo, kuvuta mkwanja na kuomba kufunguliwa miradi kadha wa kadha ili hata kama mapenzi yakiisha yeye anakuwa na faida.

Ila kama wewe ndiyo unapenda, ujue kabisa huna nafasi hiyo zaidi ya kuumizwa na mwenzi wako kila kukicha, wewe ni mtu wa majonzi, majuto, kilio na maumivu ya moyo kwani kuna muda anaweza akakufanyia lolote baya analotaka na wewe usikasirike zaidi ya kumbembeleza na wakati mwingine kujitwisha gunia la misumari kwa kujifanya wewe ndiye mwenye makosa ilimradi tu usimuudhi mwenzi wako. Anaweza akaamua kutojibu meseji au kutopokea simu yako, akijua wazi anakumudu na huna chakuzungumza juu yake. Hata kama mkikutana na kumuuliza, atakujibu anavyotaka akijua ameushikilia moyo wako.

Mara nyingi wapenzi wanaopata nafasi ya kupendwa na wenza wao wamekuwa wakitumia silaha hiyo vibaya, ikiwemo kuwaumiza wapenzi wao kwa tabia zao chafu kama umalaya, matusi, kejeli, dharau, masimango, kununa, kulazimisha kununuliwa kitu anachokitaka au apelekwe kiwanja cha starehe, kula anachotaka hata kama mfuko wa mpenzi wake haujitoshelezi. Kinachotumika hapo ni nguvu ya penzi, nguvu ya yeye kupendwa na mtu huyo.

Angalizo; kama utatumia nafasi ya kupendwa vibaya utakuja kuachwa ukiwa katika wakati mgumu, kwani inaonesha kuwa watu wenye kupenda na kutendwa ni wavumilivu sana ila wenye uamuzi mgumu na mzito wanapofika mwisho, na hata wakiamua uamuzi wao huwa hauhitaji ushauri wa ndugu, marafiki au viongozi wa dini. Huwa wanasema ‘potelea mbali, haikuwa riziki yangu’. Tumia vizuri nafasi hiyo ya kupendwa na siyo kumkomoa mwenzi wako. Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine tamu.

GPL

No comments: