ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, May 21, 2015

JK: Nitasaini miswada ya habari kabla ya Bunge la 20.

Rais Jakaya Kikwete

Rais Jakaya Kikwete, amesema atahakikisha anasaini miswada miwili ya habari kabla ya kumalizika kwa mkutano wa 20 wa Bunge la Bajeti unaendelea.

Miswada hiyo ni wa sheria ya kupata habari na wa sheria ya vyombo vya habari huku.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo wakati akifungua mkutano wa kimataifa kuhusu uwajibikaji na uwazi katika serikali, jana jijini Dar es Salaam.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo mbele ya washiriki wa mkutano huo takribani 200 kutoka nchi 65 ambazo ni wanachama wa mpango huo wa kidunia wa kuendesha serikali katika uwajibikaji na uwazi (OPG), wakati akielezea mafanikio yake katika kukuza demokrasia na uwazi kupitia maeneo mbalimbali yakiwamo uhuru wa habari na matumizi ya mitandao ya kijamii.

“Tayari miswada ya habari imeshapelekwa bungeni, ilishapelekwa kwa mara ya kwanza. Ni matumaini yangu wabunge wataijadili kabla ya kumalizika kwa vikao vya bunge la bajeti linaloendelea mjini Dodoma ili nami niweze kuisaini katika muda wangu uliobaki,” alisema Rais Kikwete.

Hata hivyo, Rais Kikwete, hakueleza namna wadau wakiwamo waandishi wa habari watakavyoshirikishwa katika utoaji wa maoni kuhusu miswada hiyo kabla ya kusainiwa kuwa sheria.

Miswada hiyo ilipelekwa bungeni kwa hati ya dharura katika mkutano wa 19, lakini wadau walipinga wakisema serikali ilikuwa na nia mbaya.

Hata hivyo, baada ya wadau kukutana na Spika, Anne Makinda, Spika aliirejesha miswada hiyo kwa Kamati ya Huduma za Jamii ili ipitishwe kwa utaratibu wa kawaida ili kuwapa fursa wadau kushirikishwa.

Alipiulizwa Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashililah, ili kuthibitisha iwapo miswada hiyo kwa mujibu wa kanuni za kibunge imo katika ratiba kwa ajili ya kujadiliwa katika mkutano wa bajeti, hakuwa tayari kulizungumzia jana.

Hibi karibuni, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Saidi Mtanda, alisema tangu kumalizika mkutano wa 19, kamati yake haikupokea miswada hiyo kwa ajili ya kuanza utafutaji wa ,aomi ya wadau.

Mtanda aliongeza kuwa, iwapo wangepewa, kamati hiyo ingebainisha namna shughuli ya kukusanya maoni hayo ingeendeshwa kwa uwazi kwa kuwashirikisha wadau.
CHANZO: NIPASHE

No comments: