Dar es Salaam. Wakati Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameunda kamati kwa ajili ya kushughulikia mgomo wa madereva uliotikisa nchi kwa siku mbili, katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye amesema haoni mantiki ya kuunda tume kuchunguza jambo ambalo linafahamika.
Wajumbe wanaounda kamati hiyo ni makatibu wakuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, Kazi na Ajira na Wizara ya Uchukuzi.
Wengine ni wajumbe watatu kutoka Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (Tatoa) na wajumbe watatu kutoka Chama cha Wamiliki wa Mabasi (Taboa), mjumbe mmoja kutoka Kikosi cha Usalama Barabarani na mmoja Sumatra.
Pia wanaingia wajumbe wengine watano ambao wanawakilisha madereva baada ya mkuu wa wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda kukubaliana na viongozi wao juzi.
Lakini Nape haoni kama kulikuwa na haja ya kuunda kamati ya kushughulikia tatizo ambalo linajulikana.
“Kama huundwa kuchunguza mambo ambayo hayafahamiki, lakini madai ya madereva hao yanafahamika,” alisema msemaji huyo wa chama tawala alipotakiwa kuzungumzia maoni ya baadhi ya wananchi kwamba mgomo huo ni matokeo ya CCM kushindwa kuwajibika na hivyo kutostahili kuendelea kupewa nafasi ya kuongoza nchi.
“Watupe au watunyime kura, ni kweli CCM na Serikali yake inapaswa kutatua suala hilo. Ndiyo maana mimi nasema sikubaliani na tume. Serikali ishughulikie suala hili kwa kuwa madai ya madereva hao yanafahamika,” alisema Nape.
“Mimi sioni mantiki ya kuunda tume kwa tatizo ambalo linajieleza. Madai ya madereva na wamiliki wa magari yanajulikana, tume ya nini?” alihoji.
Madereva waliendesha mgomo huo nchi nzima wakipinga uamuzi wa serikali kuweka sharti jipya la kwenda kupata mafunzo ya muda mfupi kabla ya kupewa leseni upya na kutaka Serikali iwalazimishe waajiri wao kuwapa mikataba inayozingatia maslahi yao.
Wakati Nape akisema hayo, CCM mkoani Mbeya imeilaumu Serikali kwa kuchelewesha mazungumzo na madereva na hatimaye kusababisha mgomo huo kuwaathiri wananchi bila sababu za msingi.
Katibu mwenezi CCM mkoani hapa, Bashiri Madodi alisema Serikali ilipaswa kuchukua hatua za haraka kutatua tatizo hilo ili kuondoa kero wanazozipata madereva.
Alisema CCM inawapa pole wananchi walioathirika na mgomo huo na inalaani ucheleweshwaji uliofanywa na Serikali.
“Tunaona hili ni tatizo kubwa ambalo linaweza kukiathiri chama kwani vitu vinavyohusu jamii vina athari nyingi, hivyo ni vema Serikali ikachukua hatua za haraka kumaliza tatizo linapotokea kwa kukaa meza moja na viongozi wa wamiliki wa magari na madereva,” alisema.
Katibu wa CCM mkoani hapa, Mwangi Kundya alisema mgomo huo haukuwa wa lazima kwa kuwa ufumbuzi wake ni rahisi, hivyo Serikali kupitia mamlaka husika zilikuwa na nafasi ya kukaa mezani mapema na kuzungumza jinsi ya kushughulikia madai ya madereva.
“Rai yangu ni Serikali kukaa meza moja na viongozi wa madereva na wamiliki wa magari ili kuzungumza na mamlaka zinazohusika kufanya utekelezaji wa haraka na kumaliza mgogoro huu ambao athari zake ni kubwa na anayeathirika ni mwananchi,” alisema.
Alisema tatizo hilo lisiposhughulikiwa vizuri litasababisha athari kubwa kwa CCM kwani mtu wa kuadhibiwa atatafutwa kwenye sanduku la kura wakati wa Uchaguzi Mkuu.
Kauli ya Nape imeungwa kuungwa mkono na baadhi ya wasomi ambao kwa nyakati tofauti walisema Serikali haikupaswa kupoteza muda kushughulikia mgomo huo kwa kuunda tume, bali ifanye uamuzi mgumu.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Benson Bana amemlaumu Waziri Pinda aliyeunda kamati hiyo akisema ameshindwa kutoa uamuzi mgumu kwa sababu naye ni miongoni mwa wanaotaka kuwania uongozi wa nchi.
“Waziri Mkuu anatafuta urais sasa kwa kiasi kikubwa akili yake inawaza jinsi ya kuupata. Hawezi kutoa sauti ya ukali dhidi ya wanaosababisha mateso haya,” alisema Dk Bana.
“Wakati wa vita vya wahujumu uchumi, wafanyabiashara wakubwa walikamatwa na kurundikwa ndani kisha kutaifishwa mali zao. Hicho ndicho kinachopaswa kufanya hata kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri waliogoma,” alisema.
Alisema kitendo cha Waziri Mkuu kusema itaundwa kamati ya kushughulikia tatizo hilo hakieleweki, kwani tayari kuna Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) ambayo ndiyo yenye jukumu hilo.
Mhadhiri mwingine Richard Mbunda alisema anaamini kwamba hali ya migomo inayoendelea kujitokeza nchini kama ya wafanyabiashara na madereva, ina lengo la kufikisha ujumbe kwa rais ajaye aweze kuweka sera nzuri za kuwakomboa.
“Wanajaribu kucheza karata zao kufikisha masikitiko yao ikiwa ni ujumbe kwa rais ajaye ili aweze kujenga mazingira ya kuwaondolea kero zao, lakini tusiangalie katika hali ya kawaida,” alisema Mbunda.
DC Makonda
Mkuu wa wilaya ya Kinondoni jana alitangaza hatua zilizofikiwa katika majadiliano baina ya Serikali na viongozi wa madereva ambapo Kamati iliyoundwa na Pinda kushughulikia mgogoro huo iliongezewa wajumbe watano ambao ni madereva.
Makonda alizima mgomo huo baada ya kuwahakikishia madereva hao kuwa angesimamia madai yao hadi kupata suluhisho, ikiwamo kuondolewa kwa sharti la kupata mafunzo ya muda mfupi, mikataba ya ajira na vikwazo vya askari wa usalama barabarani.
Makonda aliahidi kufikia suluhisho hilo na kuwapatia taarifa kamili madereva hao jana na iwapo matatizo yasingetatuliwa, angeungana nao katika mgomo.
Akitoa mrejesho kwa wanahabari jana, Makonda alisema katika vikao vya pande mbili zinazohusika juzi jioni walikubaliana kumaliza mgomo huo na kamati ya waziri mkuu iongezewe majina ya uwakilishi wa madereva watano ili kufikia watu 16.
Alisema kamati itakuwa ikikutana mara moja kwa mwezi, lakini kwa sasa vikao vitakuwa mfululizo. Alitaja ajenda za awali kuwa ni madai ya sasa ya madereva.
Akizungumzia makubaliano hayo, mwenyekiti wa muungano wa vyama vya madereva, Clementi Masanja alisema wamekubaliana na uamuzi huo wa kuundwa kwa chombo maalumu cha kushughulikia kero zao.
“Hii ni kwa mara ya kwanza kuundwa kamati ya kudumu na tumeridhika kwani ina wadau wote wakiwamo madereva, ambao leo tutachagua wa kutuwakilisha katika Kamati hiyo. Tunaamini madai yetu yatashughulikiwa kwa sasa,” alisema Masanja.
Imeandikwa na Beatrice Moses, Kelvin Matandiko na Brandy Nelson
Mwananchi
1 comment:
Good Nape
Post a Comment