ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 26, 2015

NGORONGORO: MIGOGORO YA ARDHI INATISHIA USALAMA WA RAIA

Mheshimiwa Kaika Saning’o Telele.

Ngorongoro ni moja kati ya wilaya tano zinazounda Mkoa wa Arusha. Upande wa Kaskazini inapakana na nchi ya Kenya, Mashariki kuna Wilaya ya Monduli, Kusini kuna Wilaya ya Karatu na Magharibi kuna Mkoa wa Mara.
Pia Ngorongoro ni jimbo la uchaguzi linaloongozwa na Mheshimiwa Kaika Saning’o Telele kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), likiwa na jumla ya wakazi 129,776, wengi wakiwa ni kutoka jamii ya Kimasai kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2002.

Wiki iliyopita, Uwazi lilifanya ziara jimboni humo na kuzungumza na wananchi mbalimbali ambao walieleza kero zinazowasumbua, kubwa ikiwa ni mgogoro sugu wa ardhi na jinsi mbunge wao anavyoshughulikia kero zao.
MATATIZO YA WANANCHI
Katika ziara hiyo, Uwazi lilizungumza na wananchi mbalimbali ambao wengi kilio chao kikubwa kilikuwa ni mgogoro mkubwa wa ardhi unaoendelea wa Pori Tengefu la Loliondo ambapo wanalalamika kwamba serikali kwa kushirikiana na makampuni ya kigeni ya uwindaji, wanataka kuwapora ardhi yao bila kuzingatia sheria, jambo linalotishia usalama wa wananchi na mali zao.

“Tupo hapa tangu enzi za ukoloni, leo tunaambiwa eti haturuhusiwi kuchunga mifugo yetu kwa sababu hili ni pori tengefu, wanataka tukalishe wapi mifugo yetu? Huu ni uonevu,” Daudi Ole Sayinka, mkazi wa Loliondo aliliambia Uwazi.

Uwazi liliendelea na ziara yake ambapo lilibaini matatizo mengine mengi yanayowasumbua wananchi wa eneo hilo ambapo kutokana na utata uliopo kwenye eneo la Pori Tengefu la Loliondo, wakulima na wafugaji wameanza kugombea sehemu za malisho na kilimo, huku wakulima wakilalamika kwamba wafugaji wa Kimasai wanaingiza mifugo kwenye mashamba yao, jambo linalosababisha machafuko ya mara kwa mara kati ya jamii hizo mbili.

Mwamko mdogo wa kielimu jimboni humo ni tatizo lingine ambapo watoto wenye umri wa kuandikishwa shule, wamekuwa wakinyimwa fursa hiyo na badala yake kupewa kazi ya kuchunga mifugo, jambo linalosababisha watu wengi washindwe kusoma na kuandika, huku mahudhurio shuleni yakiwa hafifu.

Uhaba wa walimu, madarasa na vifaa vya kujifunzia ni tatizo lingine lililobainishwa na wananchi wa jimbo hilo huku pia suala la kutonufaishwa na rasilimali zilizopo jimboni humo, zikiwemo mbuga za wanyama na Kreta ya Ngorongoro kukionekana kuwasononesha wananchi wengi.

“Jimbo letu lina rasilimali lukuki lakini sisi wala hatufaidiki, hata kuwinda vitoweo haturuhusiwi wakati kuna wageni wanakuja hapa na wanapewa vibali vya kuwinda na kutalii watakavyo, tunaomba serikali ituangalie kwa jicho la huruma,” Matei Sanko aliliambia Uwazi.

Kero nyingine ni uduni wa huduma za afya, ubovu wa miundombinu kwenye baadhi ya maeneo na wanyama wakali wanaovamia maboma ya wafugaji na kuua mifugo pamoja na binadamu. Uhaba wa maji safi na salama kwenye baadhi ya maeneo, ni kero nyingine jimboni humo.

Baada ya kuzungumza na wananchi mbalimbali, Uwazi lilimtafuta mheshimiwa mbunge wa jimbo hilo, Telele ili kupata ufafanuzi wa kero zilizoibuliwa na wananchi wake.

Hata hivyo, juhudi za kumpata mbunge huyo ziligonga mwamba kutokana na simu yake kuita muda wote alipopigiwa bila kupokelewa. Hata mwandishi wetu alipomtumia ujumbe mfupi wa maandishi na kumuorodheshea kero za wapiga kura wake, mbunge huyo hakujibu chochote mpaka gazeti hili linakwenda mitamboni.
Juhudi za kumtafuta mbunge huyo bado zinaendelea ili atoe ufafanuzi wa kero za wapiga kura wake, likiwemo suala sugu la mgogoro wa ardhi Loliondo.
CREDIT:GPL

No comments: