ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, May 26, 2015

MAAZIMIO YA KAMATI KUU YA CHAMA CHA ACT WAZALENDO KATIKA VIKAO VYAKE VYA MEI 23-24

Kiongozi wa Chama (ACT), Zitto Zuberi Kabwe.

KAMATI Kuu ya Chama cha ACT-Wazalendo, ilikuwa na kikao chake cha kawaida cha siku mbili kilichokaa tarehe, 23 na 24 mwezi huu na kuongozwa na Mwenyekiti wa Taifa, Anna Mghwira, pia kilihudhuriwa na kiongozi wa Chama Zitto Zuberi Kabwe.

Agenda za vikao hivyo vya siku mbili zilikuwa ni
Uteuzi wa nafasi mbali mbali za kiutendaji ndani ya chama
Operesheni majimaji
Ratiba ya Uchaguzi mkuu na Ngome za Chama
UTEUZI

Baada ya agenda hizo kujadiliwa kwa kina wajumbe wa kamati kuu waliafikiana kuwateua wanachama wafuatao

1. MANAIBU KATIBU WAKUU BARA NA ZANZIBAR

Kwa upande wa Naibu katibu mkuu bara kamati kuu imemteua MNEC Msafiri, Abrahaman Mtemelwa ambaye ni mwanasiasa mzoefu katika siasa za Tanzania na miongoni mwa vijana wa kwanza kusimamia siasa za upinzani nchini.

Mtemelwa ameshika nafasi mbali mbali za uongozi katika vyama vya siasa nchini, ambapo alishakuwa Mwenyekiti wa Kwanza wa vijana wa NCCR-Mageuzi,na baadae kuwa mkurugenzi Habari na uenezi na mkurugenzi wa Kampeni na Uchaguzi wa Chadema kazi alizoziifanya kwa mafanikio makubwa kabla ya kujiunga na ACT-Wazalendo.

Pia kamati kuu ya ACT –Wazalendo, imemteua Juma Said Sanani, kuwa Naibu katibu Mkuu Zanzibar

Juma Sanani, alishawahi kushika nafasi mbali mbali za kiuongozi katika vyama vya CUF na ADC kabla ya kujiunga na ACT-Wazalendo

Mwaka 1992 alijiunga na Chama cha CUF kabla chama hicho hakijapata usajili wa kudumu akiwa ni mwanachama wa kawaida

1993-1999 alikuwa mkurugenzi wa fedha wilaya ya mjini Unguja

1999-2009,Sanani alichaguliwa kuwa mjumbe wa mkutano mkuu wa Taifa wa CUF akitumikia nafasi ya afisa mipango na Uchaguzi katika Idara ya Mipango na Uchaguzi.

2009-2012 Sanani alikuwa mkurugenzi wa Uchaguzi CUF Taifa

2012 alijiunga na Chama cha ADC na kushikilia nafasi ya Naibu katibu mkuu Zanzibar mpaka alipojiunga na Chama cha ACT-Wazalendo machi 2015.

2. MAKATIBU WA KAMATI MBALIMBALI

Kamati kuu imemteua Peter Mwambuja kuwa katibu wa Fedha na Rasilimali

Mwambuja ni msomi wa ngazi ya CPA katika masuala ya mahesabu, aliyewahi kufanya kazi katika maeneo mbali mbali ya nchi akiwa mhasibu

Wengine walioteuliwa na nafasi zao katika mabano ni

Habibu Mchange
(Mipango na Mikakati),

Richard Sabini
(Mawasiliano na Uenezi)

Mohamed Masaga (Kampeni na Uchaguzi)

Deus Chembo (Katiba na Sheria)

Venance Msebo (Mambo ya Nje)

Gibson Kachinjwe (Katibu kamati ya Maadili na Uadilifu)

3. NAFASI YA WENYEVITI

Kamati kuu imemteua Estomih Mallah kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na Rasilimali na Mwanasheria wakili Msomi Albert Msando, ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa kamati ya Katiba na Sheria

WAJUMBE WA KAMATI KUU

Kamati kuu imewateua Mzee Japhari Kasisiko na Hamad Mussa Yusuph kuwa wajumbe wa Kamati kuu

WASHAURI WA CHAMA

Kamati kuu kwa nafasi yake imewateua Profesa Kitilla Mkumbo na Tery Bermunda(mama Tery) kuwa washauri wa Chama.

OPERESHENI MAJIMAJI

Kamati kuu imeazimia kufanya operesheni ya ujenzi wa Chama katika majimbo 59 kwenye mikoa 19, operesheni iliyopewa jina la Maji Maji na kwamba operesheni hii itaanza mapema iwezekanavyo

Lengo la operesheni maji maji litakuwa ni kueneza na kujenga chama na kukagua uhai wake chama kazi itakayofanyika kwa siku 12 kwa timu kumi za kazi kujigawa katika maeneo mbali mbali

RATIBA YA UCHAGUZI

Kamati kuu imekasimu kwa sekretariti ya Chama shughuli ya uandaaji wa ratiba na taratibu za uchaguzi kuanzia uchukuaji wa fomu na kuzirejesha, malipo ya ada ya fomu za wagombea kwa nafasi mbali mbali za kuanzia udiwani, Ubunge na Urais kwa nchi nzima

Pia kamati kuu ya ACT-Wazalendo, iliiagiza sekretariti ya Chama kuandaa utaratibu mzima uchaguzi wa Ngome za vijana, wanawake na wazee na kwamba uchaguzi wa ngome hizo ufanyike kabla ya ratiba ya uchaguzi mkuu.

Imetolewa na

Abdallah Khamis.

Afisa Habari ACT Wazalendo

26/05/2015

0777008686

1 comment:

Anonymous said...

huyu kama mansoour hemid alikuwa ccm kaanzisha chama chake na ccm wana msupport mansoor naye hana chama chaka but ccm wamemtuma aje awachafuliye chama cha cuf,washikaji wale wa cuf hawalijui hili wanamchukua mtu wanampokea na kumtia ndani ya chama na kumpa siri za nyendo zao zote badala ya kumchunguza kisawa sawa.
yote ilikuwa janja ya nyani kukamatwa na yote yale mtakuja kuyajua one day haya.ccm ndo wenye pesa ccm ndo wanaovuruga vyama vingi kwa pesa zao..alam sik.