Dinaldo Ngoma, FC Platinum ya Zimbambwe.
Nicodemus Jonas na Hans Mloli
MBIO za usajili zinazidi kukolea, Yanga imemalizana na Dinaldo Ngoma wa FC Platinum ya Zimbambwe, wakati upande wa pili wapinzani wao, Simba wanaweza kukwama kumnasa straika Mrundi, Laudit Mavugo kutokana na Klabu ya Vital’O kuonekana kuweka ngumu.
Yanga wameeleza kuwa wamemalizana na mchezaji huyo lakini wanachosubiri ni tamko la Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) juu ya kuongeza idadi ya wachezaji wa kimataifa.Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha, ameliambia gazeti hili kuwa, kama TFF itaendelea kushikilia kanuni za kuruhusu wachezaji watano tu, basi watalazimika kupitisha panga kwa mmoja wa wachezaji wao wa kimataifa ili kumpisha Ngoma.
Yanga imekuwa ikiomba idadi ya wachezaji wa kimataifa iongezwe ili isajili wachezaji wengi wa kimataifa kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye kikosi chao kitakachoshiriki Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Upande wa Mavugo, Simba wamesema walishindwa kuzungumza na viongozi wa Klabu ya Vital’O ambayo inammiliki mchezaji huyo, kutokana na hali ya machafuko nchini Burundi lakini mpaka sasa viongozi hao hawapatikani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hans Poppe, amesema: “Kuna viongozi wachache tumewapata na kuzungumza nao lakini nao wamesema hawawezi kufanya maamuzi kwa kuwa wengi wao hawapo, kwa hiyo sasa wanaendelea kufanya utaratibu wa kuona jinsi gani wanajitafuta na kukaa pamoja kisha kujadili suala hili.”
CREDIT:GPL
No comments:
Post a Comment