Mwanamuziki Banza Stone
Banza kweli anaumwa, amedhohofika, amepoteza ubora wake wa afya ya mawazo, mwili na utimamu kwa jumla. Familia yake inaelezea kwamba kwa sasa angalau kidogo afya yake imeimarika, lakini kwa mtu uliyekuwa unamfahamu Banza, huwezi kukubaliana nao. Ni kwa jinsi anavyoonekana na kile anachokifanya au kukujibu.
UKIMWANGALIA mwanamuziki, Ramadhan Masanja ‘Banza Stone’ kuanzia juu mpaka chini, ukijumlisha na mambo anayozungumza yeye, yanayosemwa na familia yake pamoja na hali halisi ilivyo, utaishia kusema: “Kweli tumwachie Mungu.”
Banza kweli anaumwa, amedhohofika, amepoteza ubora wake wa afya ya mawazo, mwili na utimamu kwa jumla. Familia yake inaelezea kwamba kwa sasa angalau kidogo afya yake imeimarika, lakini kwa mtu uliyekuwa unamfahamu Banza, huwezi kukubaliana nao. Ni kwa jinsi anavyoonekana na kile anachokifanya au kukujibu.
Hana kumbukumbu ya mambo mengine, anapewa uangalizi wa karibu sana kwa kila kitu anachofanya pale nyumbani kwao Sinza Kijiweni jijini Dar es Salaam ambapo Mwanaspoti ilimtembelea Jumamosi iliyopita.
Anatumia muda mwingi kutafsiri mambo au kufikiria swali au neno unalomwambia na huenda akakujibu kitu tofauti kabisa na ulichomuuliza.
Hakuna ruhusa yoyote kwa mgeni au rafiki kumpiga picha kuonyesha uhalisia wa afya yake kwa sasa kutokana na familia kupiga marufuku. Lakini hali ya watu kumsusa na kutotaka kumpa msaada imemfanya aombe radhi japo kwa shida kwa kuzungumza kwa kinywa chake pamoja na kusaidiwa na familia yake, amewaomba wote aliowahi kuwakosea wamsamehe.
“Bado naumwa ndugu yangu, ingawaje hivi sasa nina afadhali kidogo, lakini wanamuziki wenzangu wamenitupa, labda lipo nililowakosea, natumia fursa hii kuwaomba radhi niliowakosea na kama wapo walionikosea nami nimewasamehe kwa moyo mmoja,” alisema kwa unyonge huku familia yake ikieleza kwamba anasumbuliwa na ‘fangasi ya kichwa’ ambayo inamuumiza ndani kwa ndani.
Akiwa mbele ya mama yake mzazi, Khadija na kaka zake Hamis na Jabiri, Banza alisema mpaka sasa wanamuziki waliofika kumwona ni Bob Kisa, Rama Pentagon na Badi Bakule.
Mwanamuziki huyo aliyewahi kupata umaarufu mkubwa akiwa na Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’, Tanzania One Theatre ‘TOT Plus’, anasema bado hali yake ni mbaya na alizidiwa katika miezi mitatu iliyopita kiasi cha kushindwa kwenda kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi wake wa TOT na Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Damian Komba.
“Wakati Komba akiagwa pale Karimjee, miye nilikuwa hoi kitandani, hali ilikuwa mbaya sana,” anasema huku akiongea kwa sauti ya chini huku akisema atamkumbuka Kapteni Komba kwa mengi lakini kubwa ni uwezo wake wa kutunga nyimbo za maombolezo kwa haraka zaidi.
“Kila mtu atamkumbuka kwa hilo, kwani amekuwa akiwashangaza wengi kwa uwezo wake,” aliongeza msanii huyo ambaye muda wote unapozungumza na Banza unatakiwa kutumia sauti kubwa na kujaribu kumwelewesha kile unachotaka akujibu kwani amekuwa mzito kuelewa kwa haraka.
Kuna wakati anaweza kukujibu kwa ufasaha na kuna wakati anaweza kukujibu kitu tofauti kabisa na kile ulichomuuliza. Kwa mujibu wa mama yake, Banza alikuwa katika hali mbaya miezi mitatu iliyopita.
“Kama kuumwa, miezi mitatu hii ndiyo Banza aliumwa, ilikuwa ni mtihani mkubwa kwetu, mwanangu alikuwa katika hali mbaya sana, ilifika hatua tulimwachia Mungu.
“Banza alikuwa hamjui anayeingia wala anayetoka, tunashukuru Mungu leo anaweza hata kuchechemea na kutoka nje.
“Mikono na miguu ilikuwa ikikakamaa na kushindwa kufanya chochote, lakini Mungu mkubwa,” alisema Bi Khadija.
Kauli ya mama huyo iliungwa mkono na ndugu zake, Hamisi na Jabiri ambao ndio wauguzaji wa karibu wa Banza.
“Tulikuwa hatuchezi mbali, kila wakati tulihakikisha mmoja wetu anabaki nyumbani kwa ajili ya kumwangalia,” alisema Hamisi.
Naye Jabiri alisema hata Banza alipopata nafuu bado alikuwa hana nguvu za kuweza kujihudumia mwenyewe.
“Kama wanaume ilitubidi kuwa karibu kumsaidia kwa kila kitu,” anasema Jabiri.
Kuzushiwa vifo
Banza ndiye mwanamuziki wa dansi anayeongoza kwa kuzushiwa kifo.
“Kweli Banza amezushiwa sana kufariki dunia, taarifa ambazo familia zimekuwa zikituumiza, lakini mara zote hatuna cha kufanya zaidi ya kumwachia Mungu,” alisema Hamisi.
Aidha nduguze hao wameungana na ndugu yao kuwaomba radhi wanamuziki wanaoonekana kumsusa Banza.
“Hiki ni kitu kikubwa sana, kuna maisha ya leo na kesho, siye binadamu tupo safarini, hatuna budi kusameheana,” alisema Jabiri.
Banza alizaliwa Oktoba 20, 1972 akiwa mtoto wa tano katika familia ya watoto 11.
Amesoma katika Shule ya Msingi Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam. Pia, alisoma Shule ya Msingi Sinza. Alijifunza muziki katika Jumba la Utamaduni wa Korea alipopelekwa na jirani yao, Mzee Kapizo na chombo alichoanza kujifunza ni ‘drums’.
Banza alipitia Madrasa na baadaye akajiunga na Kundi la Home Boyz lililokuwa likicheza shoo mbalimbali za muziki. Pia alipitia Bendi za Afriswezi na Twiga kabla ya kujiunga na Twanga Pepeta na alitamba na wimbo wake wa kwanza wa Kumekucha.
Banza alijaribu kumiliki bendi ya Bambino lakini ikamshinda, pia amepitia African Revolution na ameshiriki Zing Zong ya Mafahari Watatu, pia alipitia Extra Bongo.
Mwanaspoti linamwombea apate nguvu na kurudia katika shughuli zake.
No comments:
Post a Comment