ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 4, 2015

Hali siyo salama kwa CCM majimbo ya Mbinga, Peramiho

Jimbo la Peramiho
Jimbo la Peramiho ni eneo lote la Halmashauri ya Wilaya ya Songea, maarufu kwa jina la Songea Vijijini. Halmashauri hii inaundwa na kata 19, vijiji 74 na vitongoji 617 na kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 hapa Peramiho kuna wakazi 173,821 wanaume wakiwa 86,548, wanawake 87,273 na kuna wastani wa watu wanne katika kila kaya.
Peramiho ni kati ya majimbo ambayo yalikuwa na vuguvugu la mabadiliko mwaka 1995 kwenye uchaguzi mkuu wa kwanza wa vyama vingi, japokuwa lilikuwa chini ukilinganisha na baadhi ya maeneo ya Ruvuma na mikoa jirani.
Vyama vinne vilijitokeza kuweka wagombea na dalili zilionyesha kuwa NCCR ndiyo ingekuwa tishio kubwa kwa CCM, bahati nzuri jambo hilo lilijiri pamoja na kuwa CCM haikuwa kwenye wakati mgumu sana.
Uamuzi wa wananchi kwenye masanduku ya kura yaliipa ushindi mkubwa kwa CCM na kuviacha vyama vingine vikiendelea kujifunza namna ya kupambana na chama hicho kikongwe siku za usoni.
Vyama vya Tadea na CUF vikiwasimamisha Yustin Liganga na Fulgence Kagaruki vilipata asilimia 2.2 ya kura zote kwa ujumla. Ally Madamba wa NCCR alijaribu kuvua asilimia 19.6 (kura 6,651) na Michael Mbilinyi wa CCM alichukua asilimia 78.2 (kura 26,539) na kuwa mbunge wa kwanza wa Peramiho chini ya mfumo wa vyama vingi.
Hata mwaka 2000 kwenye uchaguzi mkuu, Mbilinyi wa CCM ndiye aliibuka mshindi kwa mara ya pili, akiwaacha mbali wapinzani wake kutoka vyama vingine, akafanikiwa kuliongoza jimbo hili hadi mwaka 2005.
Ule uchaguzi wa “kimbunga” ulipowadia (mwaka 2005), CCM ilimuweka Mbilinyi pembeni na kumpa nafasi mwanamama machachari, Jenista Mhagama. Jenista hakuwa na kazi ya kutisha mwaka huo kwa sababu alikutana na wagombea wasio na mitandao mikubwa kutoka vyama vya Chadema, CUF na TLP. Mwisho wa siku mwanamama huyu aliwashinda kwa zaidi ya asilimia tisini ya kura zilizopigwa. Jenista alipata kura 46,480 (93.2%) huku vyama hivyo vitatu vikipata jumla ya asilimia 6.8 ya kura zote. Ndio tuseme, matokeo ya mwaka 2005 yalidhihirisha kuwa nguvu ya CCM imeimarika sana mwaka huo.
Matokeo mabaya kwa upinzani Peramiho yaliendelea mwaka 2010 wakati CCM iliposhinda kwa kishindo ikiwa tena na Jenista Mhagama. CCM ilichukua asilimia 89.43 (kura 28,782) na CUF, chama pekee kilichopambana na CCM kwenye uchaguzi huo, ikipata asilimia 8.21 (kura 2,642), mgombea akiwa ni Emmanuel Chilokota.
Katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika mwezi Disemba 2014, Katika jimbo la Peramiho Chadema na CUF zilipata zaidi ya vijiji 31 tofauti na mwaka 2009 wakati viliopokuwa na chini ya vijiji 10.
Ndiyo kusema kuwa vyama vya upinzani vinazidi kujiimarusha kwenye jimbo hili, japo vikifanya hivyo polepole sana. Kwa maoni yangu, ushindani mkubwa wa kulisaka jimbo hili mwaka huu utakuwa ndani ya CCM ambako makada mbalimbali wa chama hicho wamezidi kujiimarisha wakiwa na nia ya wazi ya kumuondoa Jenista ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Utaratibu wa Bunge).
Pamoja na kuwa vyama vya Chadema na CUF vina wagombea wazuri, tatizo kubwa lipo kwenye mtandao wa chama kulinganisha na CCM ambayo ina mtandao thabiti mno wakiviacha mbali vyama vingine. Pamoja na hali hiyo, ukweli unabakia kwamba jimbo la Peramiho si zuri kwa CCM miaka michache ijayo na lina kila dalili kwamba litashika kasi ya mabadiliko baada ya mwaka huu.
Wilaya ya Mbinga
Mbinga ni moja kati ya wilaya sita za Mkoa wa Ruvuma.. Kwa ujumla, wilaya ya Mbinga ina kata 45, vijiji 165 na vitongoji 1,108 na kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012. Mbinga kuna wakazi 203,309, wanaume ni 96,347, wanawake 106,962 na wastani wa watu wanne katika kila kaya.
Wilaya hii inaundwa na majimbo mawili ya uchaguzi, jimbo la Mbinga Magharibi na Mbinga Mashariki.
Jimbo la Mbinga Magharibi
Kama vyama vya upinzani, hususan Chadema, Tadea na NCCR vingekuwa na mpango wa pamoja, labda jimbo hili lingechukuliwa na upinzani mwaka 1995. Katika uchaguzi huo, CCM ilimsimamisha Dkt. Luoga Thadeus ambaye alishinda kwa kupata kura 11,331 (63.5%) akifuatiwa na Michael Mahecha wa NCCR aliyepata kura 2,622 (14.7%) na Neema Masanche wa Tadea alishikilia nafasi ya tatu kwa kura 2,567 (14.4%), huku mgombea wa Chadema, Gray Maltaka akishika nafasi ya mwisho kwa kupata asilimia 7 ya kura zote.
Ukichunguza kwa umakini utagundua kuwa kwenye uchaguzi huu vyama vya upinzani vilipata takribani asilimia 40 ya kura zote, jambo lenye maana kuwa kama vingelikuwa vimeweka mgombea mmoja vingeweza kabisa kupata asilimia zaidi ya 51 kutokana na kupigiwa kura za wananchi wasiofanya maamuzi haraka.
Kwenye uchaguzi wa mwaka 2000 yale yale ya 1995 yakajirudia. Huku NCCR ikionekana kuyumba na kupoteza mwelekeo kutokana na migogoro isiyokwisha ndani ya chama hicho, Dkt. Luoga Thadeus alisimamishwa na CCM kwa mara ya pili na kuwashinda wapinzani. CCM iliendelea kuliongoza jimbo hili hadi mwaka 2005.
Aliyewahi kuwa mwimbaji maarufu wa kikundi cha sanaa za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakati akiwa ofisa, Kepteni John Komba (sasa marehemu), ndiye alikuwa mgombea wa CCM kwenye uchaguzi wa mwaka 2005 hapa Mbinga Magharibi.
Komba aliendesha kampeni zake kisayansi akitumia vizuri ustadi wa sauti na nyimbo zake. Wananchi wa Mbinga wanasema watu walijazana kwenye mikutano yake mwaka 2005 kwa sababu walikuwa na fursa adimu ya kumuona ‘LIVE” akitumbuiza na kisha baadaye akiwaomba kura. Wakazi hao walimruhusu Komba awe kiongozi wao. Walimpigia kura 32,773 (91.1%). Washindani wake kutoka TLP, Tadea, CUF, NCCR na Chadema waliambulia asilimia 8.5 ya kura zote.
John Komba alitumikia kipindi chake cha kwanza cha ubunge akitumia sehemu kubwa ya muda wake kuzunguka na viongozi wa CCM katika mikutano mikubwa ya kitaifa ambako alikuwa anatumbuiza na kuvuta wasikilizaji wengi, na kwa mtindo huu CCM ilikuwa inajipatia wasikilizaji na huenda kufanikiwa kuwashawishi wengine waunge mkono chama hicho.
Mwaka 2010, CCM bado ilikuwa imara Mbinga Magharibi, japokuwa upinzani uliendelea kukua kiasi. Walau mwaka huo vyama vilijipunguza vyenyewe na kubakia vine, huku CCM ikitaka tena mbunge wake John Komba apewe kipindi cha pili, jambo lililowezekana. Katika uchaguzi wa mwaka 2010 walau walioweza “kuvuta soksi” na kuipa CCM presha kidogo ni Chadema. Hata hivyo chama hicho kilifanikiwa kuchukuu asilimia 10 tu ya kura za CCM tofauti na mwaka 2010 wakati CCM iliposhinda kwa zaidi ya asilimia 90.
Katika uchaguzi huo, Gilbert Jamesa Zannie wa Chadema alipata kura 3,613 (15.26) na kuwa mshindi wa pili huku Kepteni John Komba akiwa na kura 18,969 (80.11%). Safari ya John Komba kuwaongoza wana Mbinga Magharibi hadi mwaka 2015 iliishia katikati, miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu 2015 alipofariki dunia.
Kabla ya kifo cha John Komba, niliambiwa kuwa ndani ya CCM hakukuwa na hofu ya kuporwa jimbo hili aidha na mtu mwingine zaidi ya Komba mwenyewe au mtu atokeaye upande wa upinzani. Kifo chake kimesababisha makada kadhaa wa CCM kuanza harakati za haraka tangu nyumbani kwake msibani Dar es Salaam hadi alipokwenda kuzikwa kijijini kwake ndani ya jimbo la Mbinga Magharibi.
Wanasiasa hao ndani ya CCM wanapambana kuwa karibu na familia ya Komba ili ikiwezekana, mmoja wa vijana wa John Komba ambaye alikuwa kipenzi cha baba yake aweze kuwaunga mkono na ikiwezekana kuwanadi ndani ya kura za maoni za CCM na hata kwa wananchi kwa kutumia ukuu wa jina la baba yake (marehemu) hapa jimboni.
Hata hivyo nilipowasiliana na kijana huyo sikumpata hewani hadi naamua kuchapisha uchambuzi huu. Lakini pia baadhi ya makada wa CCM wanaoishi Dar Es Salaam na wakiwa na nia ya kurithi viatu vya John Komba, wanasema kuwa huwenda mwanaye mmoja pia akaingia kwenye kinyang’anyiro cha kusaka ubunge ili kuendeleza sifa ya baba yake na labda kumalizia mipango ambayo alikuwa hajaikamilisha jimboni.
Vyama vya upinzani havikupata matokeo mazuri sana kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wa mwaka 2014 japokuwa vimefanikiwa kushinda vijiji na vitongoji vingi mno kushinda mwaka 2009. Pamoja na hayo, CCM bado ina nguvu ya kujivunia sana hapa Mbinga Magharibi na sioni kama kuna dalili ya upinzani kutwaa jimbo hilo, badaye Oktoba mwaka huu.
Jimbo la Mbinga Mashariki
CCM ilitumia vizuri mwanya wa uchanga wa vyama vya upinzani katika jimbo hili, mara mfumo wa vyama vingi ulipotangazwa kuanza rasmi na kufuatiwa na uchaguzi mkuu wa kwanza wa kitaifa mwaka 1995.
Kwenye uchaguzi huo, chama hicho kikongwe kilimuandaa kada wake mkongwe, Kanzolo Komba ambaye alipata bahati ya kukutana na wagombea wa upinzani ambao hawakuna uwezo wa rasilimali fedha wala uzoefu wa kutosha wa siasa za ndani ya nchi. Chama kilichoonekana kuwa na nguvu hapa Mbinga Mashariki ni NCCR na mgombea wake Ndemiwaka Ndunguru.
Kura zilipopigwa na matokeo kuwekwa hadharani, upinzani haukweza kupoka kiti cha ubunge. Kanzolo Komba wa CCM alishinda kwa kupata kura 29,348 (76.9%) akafuatiwa na Ndemiwaka Ndunguru wa NCCR aliyekuwa na kura 5,760 (15.1%) huku wagombea wa CUF na TADEA kwa pamoja wakipata asilimia 8.1 ya kura zote. Kanzolo aliingia kwenye historia ya kuwa mwanasiasa aliyeliongoza jimbo hili katika kipindi cha kwanza cha mageuzi ya kisiasa Tanzania.
Mwaka 2000 bado CCM iliendelea kujipanga huku NCCR ikiwa dhoofu. Ngwatura Ireneus ndiye alikuwa mgombea wa chama hicho kilichokuwa na mbunge hapa Mbinga Mashariki. Mgombea huyu alitumia faida ya kuparaganyika kwa upinzani na akafanikiwa kushinda kwa kura nyingi. Na ndiye ameingia katika rekodi kama mbunge wa pili wa CCM jimboni hapa, tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.
Ilipofika mwaka 2005, taratibu za uteuzi ndani ya CCM ikiwemo kura ya maoni zilimbwaga Ngwatura Ireneus na kumpa nafasi kada mwingine wa chama hicho, Gaudence Kayombo. Baada ya Ireneus kukosa nafasi ya kuendeleza kipindi cha pili, alilalamika waziwazi kwamba amechezewa michezo michafu na viongozi wenzie akiwemo huyu Gaudence Kayombo aliyeshinda.
Kura za jumla zilipopigwa, Gaudence Kayombo wa CCM ndiye aliibuka mshindi wa kwanza dhidi ya wagombea kutoka vyama vya TLP, CUF na Chadema. Gaudence Kayombo alipata kura 82,277 (89.1%), akifuatiwa kwa mbali sana na mgombea wa Chadema, Masendi Lupogo Pancras aliyepata kura 7,520 (8.1%) huku Elzear Kawonga wa CUF akiambulia asilimia 1.8 ya kura zote.
Gaudence Kayombo alifanikiwa kuanza uongozi wa jimbo hili kwa maana ya mwakilishi wa wananchi na mshindani wake wa kisiasa ndani ya CCM, mbunge wa jimbo hili mwaka 2000 – 2005, Ngwatura Ireneus, alihamia Chadema na kuanza harakati za kusaka ushindi kupitia upinzani.
Ndiyo maana kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 CCM ilitishika sana, naambiwa ikajipanga kwa hali na mali na viongozi wakubwa wakapelekwa kuweka sawa hali ya mambo. Hofu ya CCM ilikuwa kwamba chama hicho kinapambana na mgombea ambaye amewahi kuwa mbunge wa jimbo hili kwa miaka mitano na amewahi kuwa kada wa CCM kwa kipindi kirefu na kwa hiyo alitegemewa kuwa na ushawishi mkubwa ndani ya CCM na kwa wananchi kwa ujumla.
Mipango na mikakati ya CCM kumdhibiti kada wao wa zamani ambaye mwaka 2010 aligombea kwa tiketi ya Chadema, ilifanikiwa. Mpambano kati ya CCM na Chadema uliishia kwa CCM ikiongozwa na Gaudence Kayombo kupata ushindi wa asilimia 88.88 (kura 54,645) huku Chadema ikiwakilishwa na Ngwatura Ireneus, kupata asilimia 9.06 (kura 5,598). Matokeo haya yalimshangaza kila mwana Mbinga Mashariki kwa sababu yalikuwa mapambano ya vigogo kwa vigogo.
Lakini baadhi ya wananchi wanasema kuwa kulikuwa na dalili zote kuwa Ngwatura angeangushwa kwa sababu alipokuwa mbunge kupitia CCM (mwaka 2000 – 2005) hakufanya kazi kama ambavyo wananchi walitegemea na ndiyo maana hata CCM wenyewe wakamtosa kwenye taratibu za ndani ya chama chao.
Baadhi ananchi wa Mbinga Mashariki ambao nimewasiliana nao, wanasema kwamba mbunge wao amebadilika sana tangu apewe uongozi kwa mara ya pili mwaka 2010 na nilipowauliza ikiwa watamchagua tena, walianza kunitajia amajina ya makada mbalimbali wa chama hicho ambao wameonesha nia ya kusaka ubunge wa jimbo hili.
Hali hiyo inamaanisha kuwa Gaudence Kayombo anaweza kuangushwa kirahisi mno mwaka huu ndani ya kura za maoni za CCM. Hadi sasa, pamoja na juhudi kubwa za vyama vya upinzani kuongeza ushawishi kwa wananchi na kupata ushindi kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa na kuwa na wagombea ubunge wazuri ambao hawajachujwa, naona sehemu kubwa ya wananchi inaongelea sana ushindani ndani ya CCM kuliko nje ya CCM.
Dalili hizo zinaweza kutufanya tuamini kuwa huwenda vyama vya upinzani vinaweza kukosa jambo kubwa la kujivunia kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu katika jimbo hili. CCM bado iko imara sana Mbinga na kutahitajika miujiza ya upinzani kulitwaa jimbo hili kwa mipango ya muda mfupi kabla ya upigaji kura unaotarajiwa kufanywa miezi michache kutoka sasa.
Hitimisho
Jumatano ya wiki ijayo (Tarehe 27 Mei) tutamalizia mkoa huu kwa kuchambua majimbo ya Songea na Namtumbo na kisha, Jumamosi (Tarehe 30 Mei) tutahamia mkoa wa Mwanza na kuanza uchambuzi wa majimbo ya Nyamagana, Magu na Misungwi.
(Julius Mtatiro ni kiongozi mzoefu katika siasa. Ana shahada ya Uzamili ya Utawala na Uongozi (M.A), na ni mwanafunzi wa fani ya sheria (L LB): +255787536759, kuelekeamajimboni@yahoo.com – Uchambuzi huu ni maoni binafsi ya mwandishi).
Mwananchi

No comments: