ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, June 4, 2015

Pinda aipa CCM wakati mgumu Bunda

Bunda. Waziri Mkuu Mizengo Pinda atakipa wakati mgumu Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilayani Bunda, baada ya baadhi ya wakazi wa wilaya hiyo kutishia kuwa hawatakipigia kura kutokana na kiongozi huyo kutoa ahadi hewa ya upatikanaji wa maji safi na salama.
Wakazi hao wameapa kuwa labda ahadi hiyo iliyotolewa na Waziri Pinda Machi mwaka jana, itekelezwe kabla ya Uchaguzi Mkuu, kinyume cha hivyo hawataipigia kura CCM ili kuonyesha kuwa hawaridhiki na namna wanavyodanganywa.
Wakazi hao walitoa tishio hilo juzi katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa CCM akiwamo, Katibu wa CCM mkoa wa Mara Adam Ngalawa na Naibu Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mfaume Kizigo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kwenye mkutano huo, walisema, wameazimia kutoipigia kura CCM katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba kwa kuwa viongozi wa CCM na Serikali yake wanatoa ahadi za uongo na zisizotekelezeka.
Michael Kweka alitaja ahadi iliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda Machi mwaka jana kwamba tatizo la maji lingekoma Juni, kuwa ni moja ya ahadi hewa za viongozi wa Serikali ya CCM zinazowachefua wananchi.
“Hatutawapigia kura za urais, ubunge wala udiwani wagombea wote watakaoletwa na CCM mwaka huu kwa kuwa wanakuwa wakitudanganya kwa ahadi hewa,” alisema Kweka.
Kweka alisema akiwa ziarani wilayani Bunda Machi mwaka huu, Waziri Mkuu Mizengo Pinda alitoa ahadi kwamba tatizo la maji lingekwisha ifikapo Juni mwaka huu, lakini hadi sasa hakuna dalili zozote za kumaliza kero hiyo.
Alisema hali hiyo inawafanya wakazi wa mji huo ambao wamekuwa wakidamka nyakati za usiku kutafuta huduma ya maji safi na salama kuichukia Serikali ya CCM, wakiamini kuwa haiwajali. “Mimi kero yangu ni maji. Hiki kimekuwa kilio chetu kwa muda mrefu.
Lakini kinachotuumiza ni ahadi hewa za viongozi wa Serikali ya chama chetu cha Mapinduzi kuhusu mradi unaotekelezwa hapa. Mnaonaje tukiwanyima kura sababu mmezidi ubabaishaji,” alisema mkazi mwingine wa eneo hilo akiwahoji viongozi wa CCM waliokuwapo meza kuu.
Nyerere Lucas aliilalamikia Serikali ya CCM kwa kile alichoeleza kuwa imeshindwa kutimiza ahadi zake za kuboresha miundombinu ya barabara wilayani humo kama ilivyoahidi katika Uchaguzi Mkuu uliopita na kuwafanya wakazi wa maeneo hayo kusafiri kwa tabu kutafuta maji mbali na maeneo yao. Kero nyingine walizolalamikia wakazi wa wilaya hiyo ni mikopo kwa vijana na akinamama.
Walisema mikopo kwa makundi hayo imekuwa ikitolewa kwa watu maaalum hasa vikundi vinavyomilikiwa na watumishi wa serikali, jambo ambalo limeonekana kwamba kuna nia ya dhati ya kuwasahau wananchi.

Hata hivyo, Katibu wa CCM mkoa wa Mara, Adam Ngalawa katika majibu yake ameshindwa kueleza lini mradi huo wa maji utakamilika badala yake akasema umepangwa kutekelezwa katika bajeti ya mwaka 20015/16.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Mfaume Kizigo aliwataka viongozi wa chama hicho ngazi zote kutokaa ofisini badala yake waende kusikiliza kero mbalimbali za wananchi na kuzitafutia majawabu.
viongozi hao wa CCM walikuwa katika ziara ya kukijenga chama katika wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Mwananchi

No comments: