Msomaji wa Maoni hayo Mhe. Mohamed Habib J. Mnyaa (Mb) K.n.y Msemaji Mkuu-Kambi Rasmi ya Upinzani, Wizara ya Fedha 29.06.2015.
(Yanatolewa chini ya Kanuni ya
86(6) ya kanuni za Bunge,Toleo la mwaka 2013)
Mheshimiwa Spika, awali
ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu,Subhanahu wa Taala kwa kutujalia sote afya
njema na kuendelea na kazi ya kulitumikia Taifa.
Pili
nishukuru Chama changu cha CUF kwa uamuzi wake wa busara wa kunirejesha mimi
kuwa Mgombea wa Jimbo la Mkanyageni na kama ukataji wa majimbo utaathiri Jimbo
hilo, naamini chama pia kitafanya uamuzi wa hekima na busara kwa faida ya Chama
wala sio matakwa binafsi ya yoyote.
Tatu
nichukue nafasi hii kumpongeza Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif kwa
ukomavu, uvumilivu na uhodari wake kisiasa na hata kama walimzuia kuingia
katika Baraza, yeye alikwishafanya uamuzi mapema zaidi wa kutokwenda katika
Baraza hilo maana hakuwa tayari kwenda kinyume na wajumbe wa Baraza kutoka CUF
wakiwemo mawaziri. Uamuzi huo alioufanya mapema zaidi kuungana na Wawakilishi
wake ndicho kilichomfanya Spika wa Baraza na wajumbe wa CCM kukasirika na
kuchukua uamuzi wa chuki na kisasi ambao kwa waliokuwa hawajui wanadhani kuwa
yeye alikuwa na shauku ya kwenda Barazani humo.
Mheshimiwa Spika,
kitendo cha CUF cha kususia baraza ni cha demokrasia popote pale Duniani
kinachoonesha kutokukubaliana na jambo kwa njia ya kistaarabu. Kwa kuwa
uchaguzi huru ni mchakato na unaanzia katika daftari la kuandikisha wapigakura,
hivyo basi kitendo chochote cha kuwazuia au kutokuwaandikisha wapiga kura iwe
Bara au Zanzibar ni jambo la hatari la kukiuka Demokrasia na kuufanya uchaguzi
usiwe huru na wa haki.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni inaisihi,kuionya na kuitaka Serikali
iwaandikishe watu wote wenye sifa katika daftari la wapiga kura kwa Bara au
Zanzibar ili kufikisha makisio ya wapigakura milioni 24. Aidha
Haitakuwa
uchaguzi huru na haki ikiwa idadi kubwa ya wapiga kura imeachwa kuandikishwa na
kukoseshwa haki yao ya kikatiba.
Mheshimiwa Spika,
kwa masikitiko makubwa ni kwamba hali ya siasa Zanzibar imeshavurugwa na
ilianzia pale vikosi vya ulinzi vilivyopewa silaha kuwapiga wananchi katika
zoezi la kujiandikisha. Baya zaidi ni pale askari hao wanapovaa ki-ninja ili
wasionekane nyuso zao na kuwachukua baadhi ya wananchi majumbani kwao usiku wa
manane na kuwapiga na kuwatesa kisha
kuwatupa mwituni wakiwa taaban.
Mheshimiwa Spika,
vitendo hivi vinavyofanywa sasa Zanzibar haifai kuvinyamazia na ni lazima
Serikali ya Jamhuri ya Muungano ichukue hatua madhubuti vinginevyo
vinakaribisha machafuko yasiyo na ulazima-Mwanzo wa kutoweka kwa amani uanza
taratibu na kama hatua zisipochukuliwa majuto yatakuwa ni mjukuu. Amani tayari
imeanza kutoweka Zanzibar!!!
Mheshimiwa Spika,
mwisho lakini kwa umuhimu mkubwa ni kwamba UKAWA utatoa mgombea Urais mmoja na
kuleta matumaini ya Watanzania na wanaojidanganya kuwa tutafarakana wanaota
ndoto za mchana na watasubiri sana jambo hilo la kufarakana halitatokea.
Mheshimiwa Spika,
muswada huu unaoletwa na Serikali kwa ajili ya kupitishwa una lengo la kufuta
Sheria ya Benki ya Posta Tanzania, Sura 301 na kuweka masharti yatakayoiwezesha
benki hiyo kusajiliwa na kuwa Kampuni, na pia kuweka masharti ya mpito kwa
lengo la kuwezesha utekelezaji wa Sheria hii inayopendekezwa na Serikali.
Mheshimiwa Spika,
kwa mujibu wa maelezo ya Mheshimiwa Waziri aliyoyatoa katika Kamati ya Fedha,
Uchumi Viwanda na Biashara ni kwamba Benki ya Posta ilikuwa inafanya kazi bila
ya kukidhi matakwa ya sheria ya Mabenki na Taasisi za Fedha ya mwaka 2006.
Mheshimiwa Spika,
kwa maelezo hayo ni wazi Taasisi hiyo haikuwa na haina vigezo vya kuitwa Benki,
hivyo basi Kambi Rasmi ya Upinzani inasema hata kama Serikali itabadili sheria ili ikidhi kigezo cha kuitwa
benki kwa mujibu wa sheria ya Benki na
Taasisi za Fedha ya mwaka 2006. Ambacho ni kusajiliwa chini ya sheria ya
makampuni Sura, 212, lakini bado kigezo cha mtaji kitaendelea kuwa ni tatizo
katika kutimiza matakwa ya sheria ya Benki
na taasisi za fedha.
Mheshimiwa Spika,
kwa kuwa umiliki wa benki hii tunaweza kusema ni kuwa taasisi hii inamilikiwa
na Watanzania kwa asilimia mia moja (100%), kwa maana kwamba Serikali ya
Tanzania inamiliki asilimia 86.4, Tanzania Zanzibar inamiliki asilimia 3.05,
Shirika la Posta Tanzania asilimia 8.23
na Posta na Simu SACCOS asilimia 2.68. Kuhusu Zanzibar Kambi Rasmi ya Upinzani
inazotaarifa kwamba inakusudia kuwekeza kiasi cha shilingi 950,000,000/- ili
kuongeza hisa zake na kufikia asilimia 10 kutoka asilimia 3.05 za sasa.
Mheshimiwa Spika,
kwa kuwa tatizo ni mtaji na mtaji unapatikana kwa wananchi kama utaratibu
ulitumika kwa Serikali kupunguza hisa zake na kuwamilikisha wananchi, kabla ya
kuziweka kwenye Soko la Hisa kwa sababu tahadhari kubwa ichukuliwe ili hisa
hizo zikiachwa kwenye soko zisije kuchukuliwa na wageni wachache wenye fedha,
na ile dhamira ya kuwa Benki ya watanzania ikatoweka na kuleta migogoro na
Serikali kama ilivyofanywa na PSRC kwa makampuni mengine.
Mheshimiwa
Spika, Kambi Rasmi ya Upinzani kwa dhati kabisa inatoa pongezi kwa utawala na
bodi ya wakurugenzi ya benki ya Posta Tanzania na hasa Mtendaji wake Mkuu kwa
kuweza kuiondoa benki kutoka kwenye mtaji hasi wa shilingi milioni 78 mwaka 1992 hadi kuwa na mtaji chanya wa shilingi
milioni 32,142 mwaka 2014. Hii ni kazi kubwa ukitilia maana na ushindani wa
mabenki uliopo hapa nchini.
Mheshimiwa Spika,
katika kifungu cha 2 cha muswada
kinachohusu tafsiri ya maneno “benki”
limetolewa tafsiri kuwa ni Benki ya Posta Tanzania. Kambi Rasmi ya Upinzani
inasema tafsiri hiyo ingeongezewa maneno kuwa ni Benki ya Posta Tanzania
iliyosajiliwa kwa mujibu wa sheria ya Benki na Taasisi za Fdha ya mwaka 2006.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inapendekeza hivyo kwa kuwa toka mwanzo Benki hiyo ilikuwa inaitwa hivyo lakini haikuwa inakidhi
vigezo kwa mujibu wa Sheria ya Benki na Taasisi za Fedha ya Mwaka 2006.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani haipingani na hoja ya ubadilishwaji wa sheria ya uanzishwaji wa
Benki ya Posta bali inasisitiza tena hitaji la mtaji, Serikali isikimbilie
kutafuta wawekezaji toka nje ya nchi, madhara yake kimbilio hilo tumeliona
kupitia Benki ya Biashara (NBC 1997 Ltd). Tunaamini wapo watanzania wenye fedha
nyingi za kuwezesha kutimiza sharti la mtaji kwa mujibu wa sheria ya benki na
taasisi za fedha ya mwaka 2006.
Mheshimiwa Spika,
kifungu cha 6 cha muswada kinahusu kuhamisha wafanyakazi waliokuwa watumishi wa
Benki ya posta na kuwa watumishi katika
kampuni mpya. Jambo hili limeleta mgogoro sana na watanzania wengi ambao wana
kesi zao mahakama za kazi kwa kiasi kikubwa ni kutokana na kampuni kubadilisha
muundo wake. Ni maoni ya Kambi Rasmi ya
Upinzani kwamba Serikali ihakikishe na kusimamia maslahi ya watumishi, pamoja
na muswada huu wa sheria umetambua suala
hilo ingekuwa ni vyema muswada ukaweka kifungu cha adhabu pale utawala wa benki
utakapokiuka matakwa ya kifungu hiki.
Mheshimiwa Spika,
Kambi Rasmi ya Upinzani inapenda kutoa changamoto kwa watendaji wakuu wa
mabenki yetu hasa (NMB, NBC, Dar es Salaam Community Commercial Bank, DTB,
Akiba Commercial Bank na sasa TPB n.k)
kwa nini hasa hazijitanui hadi nchi za jirani hata kama sio zaidi ya Bara letu
la Afrika?
Mheshimiwa Spika,
tulitarajia NMB kwa kuwa inamilikiwa na Waholanzi kwa asilimia kubwa kuwa
itafungua tawi lake Uholanzi na katika Mataifa mengine ya Ulaya, lakini imekuwa
ni kinyume badala yake wanachota faida ya hapa na kupeleka nje. Tusaidieni
kueleza tatizo liko wapi? Kama wenzetu wa Kenya mabenki yao yanajaa Tanzania
mabenki yetu kwanini hayana matawi Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Malawi,
Zambia, Zimbabwe, DRC n.k.
Je,
ni kweli tumekosa ubunifu na uthubutu kiasi hicho? Kama ni sheria kazi yetu
kama wabunge ndio kazi tunayotakiwa kuifanya ili kuleta ustawi katika sekta
ambazo sheria zinawazuia.
Mheshimiwa Spika,
baada ya kusema hayo kwa niaba ya Kambi Rasmi ya Upinzani,
Mheshimiwa Spika,
Naomba kuwasilisha.
………………………
Mohamed Habib J. Mnyaa (Mb)
K.n.y Msemaji Mkuu-Kambi Rasmi ya Upinzani,
Wizara ya Fedha
29.06.2015
No comments:
Post a Comment