Mbio za kusaka urais kwa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) zimezidi kushika kasi baada ya mtoto wa tano wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, Charles Makongoro Nyerere kujitosa kwenye kinyang’anyiro hicho.
Wakati Makongoro akichukua uamuzi huo kwa mara ya kwanza katika historia ya familia ya Mwalimu Nyerere, mkoani Mbeya Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais Kazi Maalumu, Profesa Mark Mwandosya naye ameingia kwenye mbio hizo.
Akitangaza nia yake katika eneo la Mwitongo kijijini Butiama jana, Makongoro aliwashambulia makada wenzake ndani ya CCM ambao wanaongoza makundi ya kuwania urais kwa kuwaita ni ‘vibaka’ wanaokivuruga chama hicho kwa maslahi yao binafsi.
Akitoa mfano kwa baadhi ya makada wanaoongoza makundi ndani ya chama hicho, Makongoro aliwataja kwa majina kuwa ni Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, Naibu Waziri wa Fedha,Mwigulu Nchemba na Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Steven Wasira.
Alisema makada hao kwa muda mrefu wamekuwa wakitumia fedha nyingi kuendesha makundi ya urais na akahoji sababu za kutafuta cheo hicho cha juu kwa fedha.
CCM irudishwe kwa wazalendo kwa sababu vibaka wamekuwa na mlengo mbaya wa kukiendeleza chama hicho, alisema.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuwa maradhi ya rushwa ambayo yameiambukiza nchi nzima.
Makongoro alisema yeye ni mzalendo wa kweli na anataka kuirudisha nchi katika misingi ya uadilifu endapo CCM itampa ridhaa ya kupeperusha bendera katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Alisema ndani ya chama hicho kumekuibuka genge la watu wachache ambao utajiri wao ni wa shaka na umejijenga kwa fedha chafu.
“Ndani ya chama tawala wamekuwapo ‘vibaka’ wachache… unajua kibaka ni kibaka tu hata kama kapewa gari la Serikali lina bendera ya taifa mbele atabaki kuwa kibaka tu.
“Wananijua vizuri huwa siwaonei haya kuwaambia ukweli, hawa ndiyo wanaotuvurugia chama na hawamheshimu Mwenyekiti wa chama, Rais Jakaya Kikwete,” Makongoro.
Katika hotuba yake ambayo alitumia saa mbili, Makongoro alijikita kuzungumzia madhara yanayotokana na rushwa ndani ya CCM na alisema baadhi ya makada wanaotumia rushwa wamezalisha makundi na mipasuko isiyo ya lazima huku akisisitiza kuwa anachukia kuwapo makundi ndani ya chama hicho.
Kwa mujibu wa Makongoro, hali hiyo imechochea badhi ya viongozi wa CCM katika ngazi mbalimbali wakiwamo wenyeviti wa mikoa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho kuishi kama mifugo.
Alisema hali hiyo imesababisha baadhi ya viongozi hao kuishi maisha ya kusukumwa kwa upepo wa makundi yanayomilikiwa na watoa fedha.
Aliwaasa Watanzania wawaogope watu wanaoonekana kuwa na haraka ya kukimbilia kutawala nchi.
“Ukiona watu kazi inatangazwa ifanywe kwa utaratibu wake na mtu aliyeiomba kazi hiyo anakiuka taratibu, muogopeni sana huyo hafai kukukuongoza maana hata akikuongoza ataendelea kukiuka taratibu ili ajinufaishe,” Makongoro.
MTANZANIA NA MILLARDAYO.COM

4 comments:
Huyu naye hana quality ya kuwa rais, amewekwa pale ili amsapoti Benard Membe hakuna jingine, ndiyo maana hakumtaja kama kibaka. Kweli nchi hii inaweza kuongozwa na Makongoro? Wote waliopo wanamuogopa Lowassa ndiyo maana ulikuwa ni mpango mzima wa kumhusisha na Richmond ulisukwa muda mrefu. Inavyoonekana Makongoro amedanganywa na kambi ya Kikwete kuwa aingie kwenye kinyang'anyiro hiki cha urais lakini amsapoti Membe halafu yeye apewe uwaziri mkuu (wamemdanganya wanamtayarisha baada ya Membe)
Mdau hapo juu kweli umenena
Mhe. baba wa taifa, Julius kambarage Nyerere- alikuwa kiongozi wa kwanza kupiga marufku uongozi wa Umangi, cheifs na uflame na uongozi wa kifamia nchini Tanzania. Itakuwayeke Charless Makongoro ambaye ni mtoto wa baba wa Taifa Mh. Julius Nyere kugombea urais wa nchi ambapo anajua kwamba anavunja sheria aliyoitekeleza baba yake. Quality au sifa ya kuwania Uraisi sio kulalamika kwa wale walio mbele, bali kuonyesha mambo utayofanya tofauti na wengine ambao wamejitokeza. Hata kama Mh. Charles Makogoro Nyeere akipat sifa zote, hataweza kuwa raisi kwa sababu moja: Raisi wa Tanzania hawezi kutoka kwenye familia moja.
haaahaahaa makongoro akiwa rais nitaamini hii nchi ni kweli kichwa cha mwendawazimu.. usikute hapo aliisha piga viroba vya kutosha kabla ya kuhutubia.. maana huyu jamaa 24/7 anawaza kangara-pombe.
Post a Comment