ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 29, 2015

Rais Mstaafu asisitiza haja ya kuilinda na kuiendeleza amani ilyopo nchini

Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, akisalimiana na waislamu mbali mbali wakati akiwasili “Masjid Imani” iliyoko Mbweni kwa ajili ya kufutari.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad na Rais Mstaafu wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume, wakisalimiana na waislamu mbali mbali katika “Masjid Imani” iliyoko Mbweni walipofika kwa ajili ya kufutari.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad na Rais Mstaafu wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume, wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waumini wa msikiti huo.
Rais Mstaafu wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume, akipokea zawadi ya misahafu kutoka kwa waumini wa msikiti huo

Na: Hassan Hamad, OMKR
Rais mstaafu wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume, amesisitiza haja ya kuilinda na kuiendeleza amani iliyopo nchini.
Amesema suala la amani si jambo la kufanyiwa mzaha bali ni suala la kulichukulia kwa umakini mkubwa, ili kuinusuru Zanzibar isije ikarejea ilikotoka.
Dkt. Karume ametoa nasaha hizo katika hafla ya futari maalum iliyoandaliwa na kamati ya msikiti wa “Masjid Imani” ulioko Mbweni, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
Amefahamisha kuwa amani ni rasilimali muhimu ya wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla, hivyo haipaswi kufanyiwa mzaha, kwani iwapo amani itatoweka inaweza kuigharimu serikali na taifa kwa ujumla.
Akizungumzia kuhusu suala la umoja na mshikanao, Dkt. Karume amesema umoja kwa wazanzibari ni neema iliyotokana na Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, na kwamba lengo la Mapinduzi hayo ni kuwaunganisha wananchi.
“Wazanzibari ni wamoja, ni kitu kimoja licha ya kuwa wametoka katika maeneo tofauti ya visiwa vya Unguja na Pemba”, alinasihi Dkt. Karume.

Rais huyo mstaafu wa Zanzibar amesema umoja wa wazanzibari ni jambo la asili linalopaswa kuenziwa, licha ya kuwepo tofauti ndogo ndogo miongoni mwa wananchi.
Dkt. Karume ameelezea kuridhishwa na hali ya amani na utulivu, na kuiombea nchi iendelee kudumu katika hali hiyo wakati wote kabla na baada ya uchaguzi wa Oktoba, 2015.
Naye Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema dhamira ya kuendeleza umoja na mshikamano iko pale pale, licha ya kuwepo kasoro ndogo ndogo zilizoanza kujitokeza.
Amesema kila mmoja ana wajibu wa kuendeleza umoja na kuwaunganisha wananchi, ili kuhakikisha kuwa Zanzibar inabakia kuwa visiwa vya amani na utulivu.
Maalim Seif amewashauri wananchi kuendeleza utamaduni wa kualikana na kufutari pamoja, ili kuzidisha mapenzi miongoni mwao.
“Utamaduni wa kualikana katika futari ni mila na silka ya Zanzibari, hatuna budi kuzuendeleza silka hizi katika visiwa vyetu”, alieleza Maalim Seif.

Ameishukuru kamati ya msikiti huo wa “Masjid Imani” kwa kuandaa futari hiyo na kuwakutanisha waislamu kutoka maeneo mbali mbali ya Zanzibar, jambo ambalo limeleta faraja kwa waalikwa hao.

No comments: