Mgombea Urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ambaye pia ni Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo Pinda ameanza safari ya kusaka wadhamini kwa kuzuru Mkoa wa Katavi.
Waziri Mkuu Pinda ambaye aliwasili Mpanda jana jioni (Jumapili, Juni 14, 2015), alipokelewa na maelfu ya wakazi wa mji wa Mpanda ambao waliamua kumsindikiza kwa mchakachaka na bodaboda kutoka uwanja wa ndege hadi nyumbani kwake, Makanyagio.
Hadi mchana huu amekwishapata wadhamini 4,243 kwa kuzuru vituo viwili tu vya Inyonga na Mpanda Mjini. Ratiba yake inaonyesha atazuru vituo vitatu katika mkoa wa Katavi.
Katika kituo chake cha kwanza leo asubuhi (Jumatatu, Juni 14, 2015), Waziri Mkuu aliwasili Inyonga yalipo makao makuu ya wilaya yake ya Mlele ambako alipata wadhamini 1,440. Alirejea Mpanda saa 9 mchana ambako katika ofisi ya CCM Wilaya alipata wadhamini 2,803.
Hata hivyo, bado anaendelea na safari ya kuelekea kijijini kwake Kibaoni, kata ya Mpimbwe, wilayani Mlele ambako ni upande wa bondeni wa wilaya ya Mlele ambako pia kuna wadhamini wanamsubiri jioni hii.
Waziri Mkuu ambaye ametumia saa 6:05 kwenda na kurudi Inyonga kutokana na ubovu wa barabara, alikuta maelfu ya watu wakimsubiri katika makao makuu ya ofisi ya CCM wilaya ya Mpanda. Alisafiri umbali wa km. 259 kwa vituo hivyo viwili tu.
Aliwashukuru wazee, wafanyabiashara na akinamama wa Inyonga kwa mchango wao wa sh. milioni 1.9/- ambao waliutoa ili umsaidie katika harakati zake za kusaka wadhamini.
Waziri Mkuu Pinda alichukua fomu hizo Ijumaa iliyopita, Juni 12, 2015) na kuanza kutafuta wadhamini kwa kuanzia wilayani kwake Mlele.
No comments:
Post a Comment