Mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva
Ukiangalia kwa undani unaweza kuhisi kuwa Yanga imeamua kufanya hivyo kama njia ya kuhakikisha Msuva hawaponyoki, hasa baada ya kuwepo kwa tetesi kwamba watani zao Simba wanamwinda mchezaji huyo usiku na mchana ili kumweka chini ya himaya yao.
ILICHOKIFANYA Yanga sasa ni sifa wala si kitu kingine.
Unajua kwa nini? Siku chache baada winga wake Simon Msuva kunyakua tuzo mbili za Mfungaji Bora na Mchezaji Bora kisha kuvuta mkwanja wa Sh11.4 milioni kwa ushindi huo, uongozi wa klabu yake umeamua kumwagia mapesa zaidi. Uongozi wa Yanga umetangaza kumwongezea fuba mchezaji huyo na kumfanya sasa awe anavuta mkwanja wa Sh2 milioni kila mwezi tofauti na ule wa awali na pia kufunguka kuwa wapo mbioni pia kumwongezea mkataba mpya mnono zaidi ya ule alionao sasa.
Ukiangalia kwa undani unaweza kuhisi kuwa Yanga imeamua kufanya hivyo kama njia ya kuhakikisha Msuva hawaponyoki, hasa baada ya kuwepo kwa tetesi kwamba watani zao Simba wanamwinda mchezaji huyo usiku na mchana ili kumweka chini ya himaya yao.
Hata hivyo uongozi wa Yanga chini ya Katibu Mkuu wake, Dk Jonas Tiboroha, umesema umeamua kumuongezea mshahara winga huyo teleza na kutaka kumuongezea mkataba mnono kutokana na kazi kubwa na ya mafanikio aliyofanya katika msimu uliopita.
Dk Tiboroha alisema licha ya kwamba mkataba wake hauibani klabu yao kumwongezea chochote, lakini tayari uongozi wa klabu hiyo umempa Msuva ongezeko hilo la mshahara kuanzia mwezi huu kutokana na kazi kubwa aliyoifanya msimu uliopita.
Ingawa Dk Tiboroha hakutaka kuuanika mshahara mpya wa Msuva, lakini Mwanaspoti inafahamu kuwa sasa atakuwa anavuta Sh2 milioni.
Akifafanua hilo, Dk Tiboroha alibainisha kuwa timu hiyo imeanza mazungumzo na Msuva ili kumwongeza mkataba mpya wa miaka miwili, licha ya kwamba mkataba wake wa sasa umebakiza mwaka mmoja.
“Msuva alifanya kazi nzuri msimu uliopita, kila mmoja aliiona kazi hiyo ndiyo maana amefanikiwa kutwaa tuzo mbili, tumemfanyia ongezeko la mshahara kwa sasa pamoja na bonasi.
“Tupo pia katika mazungumzo ya kumwongezea mkataba mpya, tunasubiri kwanza tuone kama alifuzu majaribio yake ya Afrika Kusini na kama tutapata ofa ya maana tutaweza kuwachia, ila ikishindikana tutamwongeza mkataba mpya,” alisema Dk Tiboroha
Kwa upande mwingine katibu huyo ambaye ni msomi wa ngazi ya udaktari alisema timu yao imepanga kufanya ukarabati wa jengo lao la makao makuu ili liweze kutumika kwa ajili ya kambi ikiwa ni harakati za kubana matumizi klabuni hapo.
“Tutafanya marekebisho ya jengo letu hapa Jangwani kwa ajili ya msimu ujao, tumepanga kutengeneza mgahawa kwa ajili ya wachezaji, tutaweka kambi hapo pia kwa ajili ya baadhi ya mechi,” alisema Tiboroha.
Katika hatua nyingine kiungo Geofrey Mwashiuya ameendelea kumtesa kipa Ally Mustafa ‘Barthez’ katika mazoezi ya timu hiyo yanayoendelea kwenye Uwanja wa Karume.
Waigomea Stars
Katika kile kinachoonekana kuchoshwa na matokeo mabovu ya timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ mashabiki wa Yanga jana walitaka kuizuia timu hiyo isifanye mazoezi kwenye Uwanja wa Karume jijini mpaka pale itakapowapa sababu ya kufanya vibaya.
Mashabiki hao walikwenda uwanjani hapo kutazama mazoezi ya Yanga yanayoendelea kwenye Uwanja huo ambao pia hutumiwa na Timu za Taifa kufanya mazoezi pindi zinapokuwa zinajiandaa na michuano mbalimbali.
Hali hiyo iliwafanya wachezaji na benchi la ufundi la Stars kuchelewa kushuka garini mpaka pale baadhi ya viongozi wa Yanga sambamba na Maofisa wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) walipoingilia kati na kuwatuliza mashabiki hao ambao walikubali kwa shingo upande na kuiacha timu hiyo ifanye mazoezi yaliyofanyika baada ya Yanga kumaliza.
Akizungumzia tukio hilo, Ofisa Habari wa TFF, Baraka Kizuguto alisema kuwa mashabiki wa soka hapa nchini wanapaswa kubadilika na kukubaliana na matokeo pindi timu inaposhindwa kupata matokeo mazuri.
“Tabia kama hizi ni za kihuni na ambazo hazipaswi kufumbiwa macho,” alisema.
“Lazima tukubaliane na hali halisi kwani zipo timu nyingi ambazo zinafungwa na husikii watu wakifanya vurugu. Watu wanapaswa kuwa waelewa.”

No comments:
Post a Comment