ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 15, 2015

Yanga yajifua kijeshi


Wachezaji wa Yanga mazoezini 

Ilikuwa pale pembezoni mwa Hospitali ya Aga Khan ambapo kikosi hicho kikiwa chini ya makocha wao, Hans Pluijm na Charles Boniface Mkwasa kilifanya mazoezi hayo makali yaliyolenga kuimarisha nguvu kwa wachezaji hao.
YANGA kweli imepania msimu ujao. Kwani baada ya kupiga tizi kwenye Uwanja wa Karume, Ilala kikosi cha timu hiyo kimehamia ufukweni kufanya mazoezi fulani ya nguvu kama wanajeshi.

Ilikuwa pale pembezoni mwa Hospitali ya Aga Khan ambapo kikosi hicho kikiwa chini ya makocha wao, Hans Pluijm na Charles Boniface Mkwasa kilifanya mazoezi hayo makali yaliyolenga kuimarisha nguvu kwa wachezaji hao.

Katika mazoezi hayo ambayo pia Pluijm alishiriki kwa sehemu fulani kuyafanya, Mholanzi huyo aliwataka wachezaji hao kubebana migongoni na kukimbia utamu ukiwa kwa beki Rajab Zahir aliyekuwa akibebana na kiungo mpya Lansana Kamara.

Kamara na Zahir hawakuishia hapo waliendelea kuhenyeshana katika aina nyingine ya mazoezi ya kusukumana kwa nguvu kila mmoja akitakiwa kumrudisha nyuma mwenzake hatua ambayo ilileta mchuano mkali kufuatia wote kuwa na nguvu za kutosha.

Wakati Zahir akitoana jasho na Kamara, Pluijm alijaribu kidogo kupimana ubavu na kiungo mpya kinda Geofrey Mwashiuya katika aina hiyo ya mazoezi, lakini Mzungu huyo akashtuka na kukimbia na kisha akasema: “Huyu kijana ana nguvu za ajabu sana.”

Kivutio kingine kilikuwa ni kwa mshambuliaji Hussein Javu ambaye alikuwa akipambana na kipa mpya wa timu hiyo, Benedicto Tinocco ambapo Pluijm aliangalia maumbo ya wawili hao na kutamka kwamba: “Javu umejipendelea huyo mwepesi sana,” Kauli ambayo ilizua kicheko kwa wachezaji wote.

Mbali na mazoezi hayo pia Pluijm alitaka wachezaji hao kusukumana kwa kutumia misuli ya paja na ubavu ambapo Kamara pia alionekana tishio kwa kumsumbua Zahir.

Akizungumza na Mwanaspoti mara baada ya kumalizika kwa mazoezi hayo, Kocha Pluijm alisema mazoezi hayo ni hatua ya kwanza katika wiki ya kwanza ambapo watayarudia tena wiki hii mwishoni ikiwa ni ratiba yake ya kuwapa nguvu na stamina wachezaji wake.

“Tunataka kuimarisha stamina leo (juzi) tumeanza hivi, tutarudi tena wiki ijayo tutakuwa tunafanya mazoezi haya mara moja kwa wiki, ingawa tunaweza kubadilisha hata kwa kwenda gym,” alisema Pluijm.

Pondamali na Tinoco

Kipa mpya wa Yanga, Benedictor Tinoco bado anaendelea kufanyiwa tathmini juu ya uwezo wake lakini kocha wa makipa wa timu hiyo Juma Pondamali akadokeza udhaifu mkubwa wa timu aliyotoka kipa huyo yaliyopelekea aonekane hana jipya ndani ya Yanga. Pondamali akaomba apewe siku 60 kumbadilisha Tinoco.

Tinoco ana umbo lililowavutia wengi, lakini tatizo likaja katika uwezo wake wa kudaka na makocha wa timu hiyo wakaingiwa na wasiwasi na haraka wakaanza kufikiria huenda walikosea kumsajili. Hata hivyo akizungumza na Mwanaspoti Pondamali alisema amegundua mengi juu ya mapungufu ya kipa huyo, kisha akatamka kwamba kama ataachiwa kipa huyo kwa miezi miwili atambadili na kuwa bora.

Pondamali alisema amezungumza na kipa huyo aliyesajiliwa akitokea Kagera Sugar na kubaini sababu kubwa ya kuwa mbovu kiufundi ni kutokana na kukosa kocha wa makipa katika kikosi chake hicho cha zamani.

Alisema mapungufu ya kiufundi ya kipa huyo yanaweza kutatuliwa ndani ya Yanga lakini ni lazima apewe muda taratibu wa kuweza kufanyishwa mazoezi makali yatakayompa makali zaidi.

“Ukimuangalia urefu wake ni mzuri, lakini kiufundi ana mapungufu mengi, watu hawajajua mimi nimezungumza naye ni alichoniambia ni kwamba kule katika timu yake ya zamani hawakuwa na kocha wa makipa ambaye angeweza kuwapa mazoezi yanayostahili na mengi ameyakuta Yanga, “ alisema Pondamali.

“Tutayafanyia kazi taratibu na nikiachiwa kwa siku 60 kipa huyu atakuwa na mabadiliko makubwa kiufundi ingawa tunahitaji uvumilivu katika kazi hiyo.”
Credit:Mwanaspoti

No comments: