Askari Daraja la Pili Malale Patrick Mwita wa Hifadhi ya Taifa Serengeti akiongea na Wanahabari jijini Arusha kuhusiana na Tuzo ya kuwa Askari Bora wa Ulinzi wa Faru Barani Afrika aliyotunukiwa hivi karibuni nchini Afrika ya Kusini.
Askari Daraja la Pili Malale Patrick Mwita wa Hifadhi ya Taifa Serengeti akionyesha Tuzo hiyo mbele ya Wanahabari jijini Arusha.
Askari Daraja la Pili Malale Patrick Mwita kutoka Hifadhi ya Taifa Serengeti ameshinda Tuzo ya kila mwaka ya Askari Bora katika ulinzi wa Faru kwa mwaka 2015 barani Afrika “2015 Rhino Conservation Awards”.
Mwana wa Mfalme Albert wa Pili wa Monaco ambaye ndiye mlezi wa Tuzo hizo alikabidhi Tuzo hiyo kwa Askari Patrick Mwita jijini Johanesburg nchini Afrika ya Kusini tarehe 27 Julai mwaka huu.
Patrick Mwita ameibuka mshindi miongoni mwa washindani wengine kutoka nchi zote za Afrika zenye miradi ya kuendeleza Faru katika Tuzo hizo zitolewazo kila mwaka, baada ya taasisi hiyo kutambua matendo ya kijasiri yaliyofanywa na askari huyo alipokuwa akishiriki katika ulinzi wa wanyama aina ya faru katika Hifadhi ya Taifa Serengeti. Baadhi ya vitendo hivyo vya kijasiri na kishujaa ni pamoja na
- Ni askari pekee aliye na uwezo wa kuwatambua faru asilimia zaidi ya 90 Serengeti kwa kutumia alama za asili.
- Mwaka 2007 alizuia tukio la kuuwawa kwa faru.
- Mwaka 2008 alishiriki kukamata silaha 5 za kivita toka kwa majangili waliokuwa kwenye mpango wa uwindaji haramu wa faru.
- Mwaka 2012 aliongoza askari wenzake kupambana na majangili 4 wenye silaha nzito za kivita wakiwa eneo la mradi wa faru.
- Ana uwezo wa kipekee awapo porini na hutumia muda wake mwingi katika kuwatafuta faru na kutambua maeneo yao mapya wapendayo kutembelea.
Mradi wa faru wa Moru, Serengeti ndio mradi mkubwa kabisa wa faru wenye mafanikio Barani Afrika unaoongoza kwa kasi ya kuzaliana ambayo ni asilimia zaidi ya 5 kwa mwaka.
Tuzo hizi huandaliwa kwa pamoja baina ya Wizara ya Mazingira ya Afrika ya Kusini ambayo husimamia pia masuala ya maliasili (Department of Environmental Affairs) pamoja na Chama cha Askari Wanyamapori cha Afrika (Game Ranger’s Association of Afrika).
Imetolewa na Idara ya Mawasiliano
Hifadhi za Taifa Tanzania
S.L.P 3134
ARUSHA
No comments:
Post a Comment