ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 27, 2015

BONNY MWAITEGE KUZINDUA ALBAMU TATU KWA MPIGO AGOSTI 2 JIJINI DAR



MKURUGENZI wa Msama Promotions, Alex Msama  amewaita Maaskofu na viongozi wengine wa dini katika uzinduzi wa albamu tatu za mwimbaji nguli Bonny Mwaitege zinazotarajia kuzinduliwa Agosti 2 kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.

Kwa  mujibu  wa  Msama  ambaye  ni  mdhamini  wa  uzinduzi  huo, Maaskofu watafikisha  ujumbe wa neno la Mungu  kwa karibu zaidi baada ya waimbaji kumaliza kazi yao jukwaani.

Msama alisema uzinduzi huo unatarajia kusindikizwa na waimbaji mbalimbali wa Tanzania na nje lengo likiwa ni kufanikisha uzinduzi mahiri wa albamu hizo. Msama alisema pamoja na uzinduzi huo kusindikizwa na waimbaji mahiri pia, waimbaji chipukizi watamsindikiza Mwaitege ambaye hivi sasa anaendelea na mazoezi kuelekea uzinduzi huo.


Aidha Msama alisema hivi sasa muimbaji huyo pia anamalizia kurekodi baadhi ya nyimbo zilizomo kwenye albamu hizo katika majiji ya Mwanza, Arusha, Mbeya  na Nairobi. Msama alitumia fursa hiyo kutoa wito kwa mashabiki wa muziki wa injili kujiandaa na uzinduzi huo ambao utakuwa ni wa aina yake.

"Maandalizi makubwa kuelekea uzinduzi wa Mwaitege yameshafanyika, kilicho mbele ni uzinduzi wa hali ya juu, mashabiki wakae mkao wa kula," alisema Msama na kuongeza. "Uzinduzi wa Mwaitege utakuwa ni wa aina yake kwa sababu maandalizi yake kwa sababu yamefanywa kwa ustadi mkubwa, mashabiki watarajie kazi bora zaidi kutoka kwa muimbaji huyo," alisema.  

No comments: