ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 31, 2015

LEO NDO’ UNAJUA KUWA HAKUFAI, ANA WAPENZI WENGI?-2

Mpenzi msomaji wangu, wiki hii nitaimalizia makala haya niliyoanza wiki iliyopita ili niweze kuanza mada nyingine.
Ninachokizungumzia kwenye makala haya ni ile tabia ya baadhi ya watu kuwatangazia wapenzi wao wa zamani mambo mabaya ili kuwachafulia katika mahusiano yao yajayo.

Wanaofanya hivyo wapo wengi sana huko mtaani. Unaweza kukuta wameishi kwa miaka mingi wakitamkiana kila aina ya maneno matamu ya kimahaba, kuitana majina mazuri lakini walipokuja kuachana mpenzi amegeuka kuwa fala. Hii ni mbaya sana.


Kibaya zaidi wapo ambao hufikia hatua ya kuanika mapungufu ya wenzao faragha, mambo ya siri yaliyokuwa kati yao ili tu kumfanya mwenzake aonekane asiyefaa kwenye jamii.Je, ni kweli leo ndiyo unagundua kuwa siyo mjuzi faragha? Eti ooh hana lolote faragha, hajitumi, ni kama gogo tu, mbona ulidumu naye miaka yote hiyo?

Leo hii mmeachana ndiyo unaanza kumtangazia kuwa ni goigoi faragha, huoni kwamba unatapatapa? Halafu ni mazuri mangapi ambayo amekufanyia? Mbona hayo huyasemi umekazania upungufu wake tu?

Nadhani tunatakiwa kuacha huu ulimbukeni wa kutangaziana mabaya baada ya kuachana. Hakuna kitu ambacho kinaweza kukufanya ukaonekana wa ajabu kama kumzungumzia vibaya mpenzi wako wa zamani.
Utaonekana unatapatapa kwa kuachwa na wengine watahisi una dhamira ya kumchafulia tu mwenzako. Matokeo yake sasa unaweza usipate mtu wa kuwa naye kimapenzi, kila mtu atakuogopa.

Hawawezi kuwa na wewe kwa kuwa wanaogopa mkiachana utawatangazia mabaya na udhaifu wao.
Hivi wewe unadhani huna upungufu ambayo mpenzi wako naye akiamua kukutangazia kwa watu utaaibika? Najua kuachwa kunauma sana na wengi wanashindwa kuvumilia ile hali lakini naomba niseme kwamba, ukiachwa shukuru kwani hujui Mungu ana siri gani.

Pia ukipata ujasiri wa kumuacha mtu ambaye ulikuwa unampenda sana, jua kwamba hakukuwa na jinsi, ilikuwa ni lazima ufanye hivyo kisha zilipendwa wako abaki tu kwenye historia kuwa, uliwahi ‘kudate’ na flani.
Kama alikuwa mchovu faragha, alikuwa mchafu, alikuwa anakojoa kitandani, alikuwa kiwembe na mambo mengine kama hayo, muachie yeye na huyo atakayekuwa naye baada ya wewe.

Kwani wewe ukifanya hivyo utapata faida gani? Kwamba aaibike? Sawa, akishaaibika wewe utapata nini kwa mfano?
Kama ulikuwa hujui basi leo tambua kwamba, kuacha na kuachwa ni kitu cha kawaida. Muachane kwa ubaya au kwa uzuri, bado mlikuwa wapenzi na ‘mlishea’ mambo mengi hivyo mna kila sababu ya kuendelea kuheshimiana badala ya kuanza kuanikana.

Hivi ingekuwa ni kanuni kwamba kila mtu akiachana na mpenzi wake anaanika siri zake ingekuwaje? Mimi sina jibu la moja kwa moja ila najua wewe msomaji wangu unajua kipi kingetokea.
Naomba niishie hapo kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.
GPL

No comments: