Magufuli
Na Waandishi WA, Mwananchi
Bila makeke, majivuno wala majigambo, Magufuli ambaye ni waziri wa ujenzi alipochukua fomu alisema tu kuwa kipaumbelea chake ni kutekeleza ilani ya uchagzi ya CCM. Hata katika safari yake ya kusaka wadhamini mikoani, mbunge huyo wa Chato alikwenda kimya kimya, bila mbwembwe, ahadi wala kukusanya mashabiki.
Dar es Salaam. Kama alivyowashangaza wengi pale alipojitokeza kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa na CCM kuwania urais Mei 29 mwaka huu, ndivyo Dk John Magufuli alivyowashangaza tena jana kufikia hatua hii ya tano bora.
Bila makeke, majivuno wala majigambo, Magufuli ambaye ni waziri wa ujenzi alipochukua fomu alisema tu kuwa kipaumbelea chake ni kutekeleza ilani ya uchagzi ya CCM.
Hata katika safari yake ya kusaka wadhamini mikoani, mbunge huyo wa Chato alikwenda kimya kimya, bila mbwembwe, ahadi wala kukusanya mashabiki.
Bila shaka hiyo ndiyo siri yake ya ushindi, alihofia kukatwa mapema kwa kukiuka masharti ya chama, kama ilivyowatokea wengine.
Hata kabla hajachukua fomu, Dk Magufuli hakuwahi kutangaza nia yake ya kuwania urais, hadi alipoibuka ghafla na papo hapo akapenya hadi hatua hii muhimu, hadi alipolidokeza gazeti hili mjini Dodoma.
“Swali hili nimeulizwa mara nyingi. Mara zote nimekataa kulijibu kwa sababu katika chama chetu (CCM) kuna utaratibu wake wa namna ya kuomba nafasi ya uongozi. Muda ulikuwa haujawadia.
“Lakini utakumbuka wiki hii hapa hapa Dodoma, vikao vya juu vya chama chetu vimetoa ratiba kwa wanaotaka kuwania nafasi mbalimbali kujitokeza. Kwa maana hiyo sasa niko huru kujibu swali lako kwa kusema rasmi ‘nitagombea urais’.
“Nafanya hivyo kwa sababu naamini ninazo sifa za kuchagua na kuchaguliwa kama mwanachama wa CCM kwa nafasi yoyote inayojitokeza kulingana na Katiba ya chama chetu na pia Katiba ya nchi,” alisema Dk Magufuli.
Pamoja na kutokuwa na papara za kutangaza nia wala kuanza kupitapita kwa wanachama kutafuta kuungwa mkono, Dk Magufuli alikuwa vinywani mwa watu wengi, ndani na nje ya CCM, wakisema akiteuliwa anaweza kuleta ushindani dhidi ya upinzani.
Waziri huyo wa muda mrefu na maarufu kwa kumbukumbu na kukariri takwimu mbalimbali, kila wizara anayokwenda inageuka maarufu na kuanza kusikika, lakini kazi kubwa inayomweka kwenye mwanga wa kisiasa nap engine hata kumfikisha katika hatua hii ni wizara ya Ujenzi na hasa usimamizi wa ujenzi wa miundombinu.
Dk Magufuli alizaliwa katika Kijiji cha Rubambangwe kilichopo Wilaya ya Chato mkoani Geita, ndipo unapoweza kukutana na wananchi ambao wanafahamu maisha yake ya ujana na hatua alizopita hadi hadi hatua ya leo.
Kuna simulizi za kusisimua kuhusu maisha ya Magufuli ambaye wananchi wengi wa jimbo lake wanamtumia kama alama ya ushindi, akihusishwa na mafanikio ya kujitenga kutoka Wilaya ya Biharamulo hadi wakapata jimbo na hatimaye Wilaya.
Alivyoachishwa kazi
Kama ilivyowahi kuelezwa na gazeti hili, wakazi wa Chato wanaamini kuwa Dk Magufuli hakuwa na ndoto za kuwa mwanasiasa mpaka aliposhawishiwa na wazee kugombea ubunge baada ya kuona wamekuwa wanyonge kwa muda mrefu.
Mzee Emmanuel Francis anayakumbuka maisha ya ujana ya Magufuli, ‘’Wazee tulikaa na kumuona huyu ndiye msomi wa kiwango cha juu anayeweza kutukomboa tulikuwa tunamfuatilia tangu akiwa mwalimu shule ya sekondari Sengerema hata alipokuwa mkemia kwenye shirika la pamba,” alibainisha Francis.
Anasema Magufuli hakuwakatisha tama, alikubali kujitosa kugombea ubunge akipambana na Phares Kabuye (sasa marehemu) ingawa matokeo hayakukidhi kiu yao, japokuwa mgombea mwenyewe aliyakubali.
Tukio la Magufuli kumshika na kumpongeza mshindani wake liliwashangaza na kumuona kama kijana asiye na kinyongo.
KIlichomponza hata hakina maana, wanasema hata uvaaji wake wa miwani ulimpunguzia kiasi fulani cha kura baada ya baadhi yao kuamini kuwa miwani ni kielelezo cha usomi na hivyo asingekuwa kiongozi wa kukimbiliwa.
‘’Wasukuma tuna kasumba ya kupigiwa magoti, baadhi ya wananchi walipomuona ni kijana anayependa kuvaa miwani walisema huyu ndiye atatusahau kabisa,” anabainisha Francis.
Alipojaribu mara ya pili baada ya jimbo kutengwa na kuanzishwa Chato akaibuka mshindi, sasa wanajivunia kuwa na shule nyingi za sekondari zikiwamo wa Muungano, Meghji na Chato na nyingine zikiwa na kidato cha tano na sita, suala ambalo Francis anasema lisingewezekana bila Dk Magufuli.
Tetesi za urais
Wanakijiji wenzake wanakiri kuvuma kwa jina la mbunge wao na kutajwa miongoni mwa waliokuwa wanataka kuwania urais katika.
Francis anasema hana wasiwasi na kutajwa kwa jina la mbunge wake miongoni mwa wanataka uongozi wa nchi kwa kuwa amepata uzoefu mkubwa kupitia wizara alizoongoza katika awamu tofauti.
“Amepita katika wizara nyingi bila kuwa na tuhuma za ubadhilifu kama ilivyotokea kwa mawaziri wengine, alionyesha uadilifu na kila wizara aliyoongoza ilionekana kuwa imara na yenye mafanikio,” alisema Francis.
Tangu awali, mzee huyo na wenzake walibainisha kuwa wanatamani mbunge huyo achukue fomu ya kugombea nafasi ya urais, huku akiamini kuwa anaweza kuungwa mkono na wananchi wengi kutokana na historia yake ya kuwatumikia kwa uadilifu.
Hata hivyo, wasiwasi wa wengi ni kuwa waadilifu wa aina yake ni vigumu kupata nafasi hadi kufikia kiwango cha kupendekezwa kuwania uongozi wa nchi kwa kuwa kuna makundi hayawapendi.
Mchunga ng’ombe
Familia ya Magufuli ambaye ni baba yake na John ilikuwa ya wafugaji, hivyo watoto waliozaliwa katika kaya hiyo kwa vyovyote vile wasingeweza kulikwepa jukumu la kuchunga ng’ombe.
Hata wakati wa likizo wananchi walizoea kumuona John akifanya kazi za kawaida za nyumbani ikiwa ni pamoja na kuchunga ng’ombe na kukamua maziwa wakati wa likizo.
“Baba yake alikuwa na mifugo mingi na hakuwa mtu wa kujikweza, wakati wa likizo tulizoea kumuona John akifanya kazi za nyumbani hata kwenda shambani kulima na kukamua maziwa,” alisema mkazi wa kijiji hicho.
Mkazi mwingine, Maritha Rufunga ana kumbukumbu tofauti kuhusu maisha ya ujana wa mbunge huyo na hata hajasahau wakati mbunge huyo kwa sasa alipoanza safari yake kielimu kwa kujikwaa.
“Hakuwa na majivuno na hata alipomaliza shule na kushindwa kuchaguliwa baba yake alikuwa amekataa asiendelee na masomo, lakini kuna mwalimu wake alikwenda kumtetea kwa baba yake ili akarudie shule,” alisema Maritha Rufunga.
CREDIT:MWANANCHI
CREDIT:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment