Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mara, Christopher Sanya, amesema kitendo cha Lowassa, kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinaashiria chama hicho kumomonyoka, baada ya kumalizika kwa kura za maoni.
Alisema ni pigo kubwa kwa CCM na litasababisha madhara makubwa baada ya kura za maoni kumalizika.
“Lowassa ametumia haki yake kufanya hivyo, kama mwenyewe alivyosema hakuridhishwa na mchakato mzima wa kumpata mgombea urais wa CCM ingawa ni pigo kubwa kwa chama chetu,” alisema Sanya na kuongeza kuwa uamuzi wake sio wa kubeza kwani yeye ni mtu kukatwa Dodoma alikaa kimya muda mrefu bila kuzungumza chochote hadi alipofikia kuchukua maamuzi hayo ya juzi.
Mbunge wa Mwibara anayemaliza muda wake, Kangi Lugola, alisema uamuzi huo una madhara makubwa kwa CCM hasa kipindi hiki.
“Kwanza namtakia kila la heri katika kuendeleza safari yake ya matumaini, huyu ni mtu mzima, mwenye elimu, amekuwa kiongozi mwandamizi serikalini na mkongwe wa siasa, hivyo hadi kufikia hatua hiyo hakufanya maamuzi ya pupa bali ametumia busara na hekima kubwa,” alisema Lugola.
Hata hivyo, alipoulizwa endapo atamuunga mkono kwa kuhamia Chadema, alisema anatambua kufanyiwa mizengwe mingi na viongozi wa CCM ngazi ya wilaya, lakini kwa sasa anashiriki katika kura za maoni akiamini viongozi hawawezi kumzuia kuingia bungeni kwa mara nyingine.
“Nilienda Dodoma miaka mitano hii tunayomaliza kwa kupelekwa na wananchi wa Mwibara, wananchi hao hao bado wapo hivyo viongozi wa CCM watambue pia nitapelekwa Bungeni na wananchi hao hao si viongozi wa chama,” alisema Lugola.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Hamisi Mgeja, alisema licha ya Lowassa kuwekeza jasho lake kwa kipindi kirefu ndani ya CCM, lakini ana haki na ni mtu mzima ambaye hawezi kuingiliwa katika kufikiwa maamuzi yake.
“Ingawa hili ni jambo kubwa na zito, lakini tumekuwa naye kwa kazi, tumeshirikiana naye kukijenga chama chetu, lakini ikifika mahali huwezi kuzuia mtu kufanya maamuzi yake,” alisema Mgeja.
Hata hivyo, alisema licha ya rafiki yake kuondoka, yeye atabaki kuwa mwana-CCM mwaminifu na muadilifu na mwenyekiti wa mkoa huo.
Mwanasiasa Mkongwe na kada maarufu wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru, alisema: “Kwa sasa sina cha kusema, bwana mwandishi, no comment, ila nitatoa comment zangu wakati muafaka utakapowadia.”
Naye Mwenyekiti wa CCM, mkoa wa Singida, Mgana Msindai, alisema kwa sasa hana maoni na kuomba apatiwe muda hadi leo.
Mbunge wa Ilala, Mussa Azan Zungu, alisema hana maoni na anasuburi chama kitoe maamuzi yake.
Imeandikwa na Rapahael Kibiriti, na George Marato, Anceth Nyahore na Mary Geofrey.
CHANZO: NIPASHE
No comments:
Post a Comment