Advertisements

Tuesday, July 7, 2015

Nape: Hakuna nafasi ya kukata rufaa majina yakikatwa

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye.

Dodoma.Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema hakutakuwa na nafasi ya kukata rufaa kwa wanachama  wa chama hicho walioomba ridhaa ya chama kupeperusha bendera ya CCM katika nafasi ya Urais iwapo majina yao yatakatwa.
Kauli hiyo imetolewa mjini Dodoma leo na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama hicho, Nape Nnauye alipokutana na waandishi wa habari  wakati  akitoa taarifa ya ratiba ya vikao vya mchujo wa wagombea utakaoanza siku mbili zijazo.
Kikao hicho kitaongozwa  na Katibu Mkuu CCM Abdulrahaman Kinana pamoja na kikao cha sekretarieti ya chama.
Nape alisema hakutakuwa na nafasi ya kukata rufaa kwasababu, kwanza hakuna kanuni hiyo na pia hakutakuwa na muda wa kutosha kufanya hivyo.
“Tuwe wakweli tu, muda wenyewe siuoni na kanuni haisemi habari ya kukata rufaa…uchujaji wa majini kikao hakitakiwi kutoa sababu, sasa unakataje rufaa,” alisema Nape.
Hata hivyo Nape amewapa matumaini wanachama wa chama hicho kuwa watatoka kwa umoja hata baada ya kupatikana kwa mgombea urais kupitia chama hicho.
 Aidha amebainisha  kuwa  hakuna fujo zozote zitakazotokea, kwa kuwa vyombo vyote vya ulinzi vimejipanga vya kutosha.
Kwa mujibu wa ratiba  ya kikao,Kamati Kuu itakutana tarehe tisa  na kutoa wagombea watano kabla ya Halmashauri Kuu kukutana  tarehe 10mwezi huu, ambapo majina matatu ya wagombea yatateuliwa kabla ya kupigiwa kura na wajumbe wa mkutano mkuu tarehe 11 ili kumpata mgombea mmoja atakaepeperusha  bendera ya chama hicho.

MWANANCHI

No comments: