ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, July 29, 2015

UNODC KUISAIDIA ZANZIBAR KUPAMBANA NA DAWA ZA KULEVYA KWA JAMII

Kiongozi wa ujumbe kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu, Jose Vila Del Castillo akimsikiliza kwa umakini Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad alipofika ofisini kwake Migombani.


Shirika la Umoja wa Mataifa la Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (UNODC) limesema litafanya tathmini ya kina kupata njia muafaka za kuisaidia Zanzibar kukabiliana na biashara, matumizi na athari za dawa za kulevya kwa jamii.
 


Hayo yamesema na Kiongozi wa ujumbe kutoka Shirika hilo, Jose Vila Del Castillo alipokutana na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad huko ofisini kwake Migombani na kufanya naye majadiliano.
 


Del Castillo amesema kutokana na mazingira ya nchi za visiwa kama Zanzibar mikakati maalum ya kupambana na dawa na biashara za dawa za kulevya haina budi kuchukuliwa ili kuwaokoa wananchi wake na kugeuzwa njia za kusafirishia biashara hiyo haramu.
 


Amesema msaada huo utalenga zaidi kuipatia Zanzibar vifaa vya kisasa, kukuza utaalamu kwa watendaji na wadau muhimu wa kupambana na dawa za kulevya, ikiwemo wendesha mashitaka, wapelelezi, watendaji wa Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali pamoja na wanasheria.
 


Alisema UNODC litaanza kufanya tathmini hiyo mwezi ujao na ikikamilika, Shirika hilo litaweza kufahamu ni hatua gani linapaswa kuanza kuzichukua kwa mashirikiano na Serikali ya Zanzibar kukabiliana na biashara hiyo na madhara yake.
 


Katika mazungumzo hayo, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad amesema Serikali inachukua hatua mbali mbali kuiepusha Zanzibar kuwa kituo cha kuingizwa na kusafirishiwa dawa za kulevya.
 


Maalim Seif amesema juhudi hizo pia zinajumuisha kuwasaidia wananchi wasijiingize kwenye vitendo vya kutumia au kufanya biashara hiyo, ikiwemo kutoa miongozo kwa makundi mbali mbali ya jamii, wakiwemo wanafunzi wa skuli mbali mbali.
 


Kuhusu wale ambao tayari wanatumia dawa hizo, Maalim Seif amesema Serikali kwa mashirikiano na jumuiya na watu binafsi imefungua vituo maalum kwa ajili ya kuwasaidia kubadilisha tabia, ili baadaye wawe raia wema katika jamii yao.
 


Makamu wa Kwanza wa Rais amesema hivi sasa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar tayari imeanza ujenzi wa kituo cha kisasa cha kurekebisha tabia wananchi wanaotumia dawa hizo, ambacho jengo lake litakuwa na ghora tatu na sehemu zote muhimu kwa mahitaji yao.
 


Hata hivyo, alisema zipo baadhi ya changamoto zinazojitokeza katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya Zanzibar, ikiwemo uhaba wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi na ukaguzi katika maeneo ya kuingilia na kutokea nchini.
 


Changamoto nyengine alizozitaja ni mazingira ya visiwa vya Zanzibar kuwa na bandari nyingi zisizokuwa rasmi ambazo hutumiwa na baadhi ya watu kuingiza vitu vyenye madhara, zikiwemo dawa za kulevya.

Katika mazungumzo hayo, Mshauri wa masuala ya Ukimwi wa Shirika hilo Kanda ya Afrika Mashariki, Sylvie Bertrand amesema msaada huo wa UNODC pia utajumuisha kuimarisha mazingira ya vyuo vya mafunzo, ili kuepusha maambukizi ya ukimwi na athari nyengine zitokanazo na dawa za kulevya.

No comments: