Afisa Madini Mkazi- Ofisi ya Madini Handeni, Frank Makyao (kulia) akifungua mafunzo kuhusu huduma za leseni za madini kwa njia ya mtandao yaliyokutanisha wachimbaji wa madini kanda ya mashariki mjini Handeni. Kutoka kushoto ni wawezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Pendo Elisha na Charles Gombe.
Mwezeshaji wa mafunzo hayo kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Charles Gombe (kushoto) akisisitiza jambo katika mafunzo hayo. Kulia ni Afisa Madini Mkazi- Ofisi ya Madini Handeni, Frank Makyao.
Na Greyson Mwase, Handeni-Tanga
Wachimbaji wa madini nchini wametakiwa kuendana na teknolojia
inayokua kila kukicha ili kuwezesha sekta ya madini kuwa na mchango
zaidi katika pato la taifa.
Rai hiyo ilitolewa na Afisa Madini Mkazi kutoka Ofisi ya Madini- Handeni
mkoani Tanga, Frank Makyao kwenye ufunguzi wa mafunzo juu ya
matumizi ya huduma za leseni za madini kwa njia ya mtandao
yaliyokutanisha wachimbaji wa madini katika kanda ya mashariki
yanayoendelea mjini Handeni.
Lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kuwapa uelewa wa matumzi ya
huduma za leseni za madini kwa njia ya mtandao ijulikanayo kama
online mining cadastre transactional portal.
Makyao alisema kuwa ni vyema wamiliki wa leseni za madini
wakaachana na mfumo wa zamani wa kutumia makaratasi katika
huduma za leseni kwani mfumo wa kisasa wa huduma za leseni kwa
njia ya mtandao utawawezesha kupata leseni kwa wakati na uwazi
zaidi.
“ Kwa mfano kuanzia sasa mtaweza kufanya malipo ya leseni zenu kwa
njia ya M-Pesa, Airtel Money na Tigo Pesa hali itakayowezesha ofisi za
madini kupata mapato zaidi.” Alisisitiza Makyao
Makyao aliendelea kusema kuwa wachimbaji wa madini wanatakiwa
kuchangamkia mafunzo yanayotolewa na wataalam kutoka Wizara ya
Nishati na Madini na kuanza kutumia huduma hiyo mara moja ili
kurahisisha utendaji wao wa kazi.
Alisema biashara katika nchi nyingi duniani imekuwa ikifanyika kwa njia
ya mtandao na kuwataka wachimbaji wa madini kuchangamkia fursa
hiyo ili waweze kuendana na ushindani wa biashara ya madini duniani.
Aidha aliwataka wachimbaji wa madini kufuata sheria za madini katika
uombaji na umiliki wa leseni za madini pamoja na kushirikiana na
serikali kwa kulipa kodi na tozo mbalimbali kama Sheria ya Madini ya
Mwaka 2010 inavyowataka ili sekta hiyo iwe na mchango zaidi katika
ukuaji wa uchumi wa Taifa.
No comments:
Post a Comment