ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 27, 2015

Kipindupindu Dar chaua 10, wagonjwa sasa wafikia 65

Jumla ya watu 10 hadi kufikia jana walikuwa wameshapoteza maisha kutokana ugonjwa wa kipindupindu jijini Dar es Salaam huku 93 wakiwa wamelazwa kwenye kambi zilizotengewa kwa ajili ya walioathirika na ugonjwa huo.

Nipashe ilitembelea katika Kambi ya Mburahati wilayani Kinondoni jana na kushuhudia madaktari na wauguzi wakiendelea kutoa matibabu.

Akizungumza na gazeti hili msimamizi wa kambi hiyo, ambaye pia ni Mratibu wa Mafunzo Idara ya Afya Wilaya ya Kinondoni, Alfred Ngowi, alisema hadi kufikia jana wagonjwa 65 wa kipindupindu kati yao wakiwamo wanaume 36, wanawake 18 na watoto 11 walikuwa wamelazwa katika kambi hiyo.

Katika Wilaya Kinondoni hadi sasa watu watano wameshafariki wakiwamo wawili wakazi wa Alimaua, mtoto wa mwaka mmoja na nusu (Mwanyamala) na wengine wawili wa eneo hilo.

“Mpaka jana asubuhi kulikuwa na wagonjwa 52 lakini waliongezeka 13 na kufanya idadi kufikia 65 wakitokea majumbani na katika Kituo Cha Sinza,” alisema Ngowi.

Aidha, alisema wagonjwa wote wa kipindupindu hupokelewa katika kambi za Sinza na Mwanayamala na kupewa huduma ya kwanza kisha hupelekwa kwenye Kambi Kuu ya Mburahati kwa matibabu zaidi.

Ngowi alisema maeneo yaliyoathirika ni Manzese mtaa wa Mianzini, Tandale, Kijitonyama, Kinondoni, Ubungo, Wazo na Goba.

Aliongeza kuwa, kabla ya wagonjwa kuruhusiwa kurudi nyumbani, hupewa elimu ya afya na jinsi ya kujikinga na ugonjwa huo huku wakipewa dawa za kuweka kwenye maji na kumwaga katika vyoo zikiwamo Waterguard na Chlorine kwa ajili kuzuia maambukizi.

Aliishukuru Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Shirika la Afya Duniani (WHO), Shirika la Msalaba Mwekundu na Jeshi la Wananchi wa Tanzania kwa misaada wanayoendelea kuitoa.

Naye Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Mussa Natty, alisema manispaa hiyo ilianza kufanya mikakati ya kupambana na ugonjwa huo kabla wizara husika haijatoa agizo la kupiga marufuku ya uuzaji vyakula kiholela na maji ya kunywa maarufu kama ‘Kandoro’.

Alisema kwa kuzingatia madhara ya ugonjwa huo wananchi walipewa elimu ya jinsi ya kujikinga na kupeleka wataalamu wa afya katika mitaa na kata kutoa elimu.

Kwa upande wa Mganga Mkuu wa Wilaya Ilala, Dk. Victorina Ludovick, alisema wagaonjwa 25 wa kipindupindu walikuwa wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Buguruni Mnyamani.

Dk. Ludovick alisema katika wilaya hiyo tangu ugonjwa huo uanze kimeshatokea kifo cha mtoto mmoja wa kike wa miaka mitatu mkazi wa Buguruni Kisiwani.

Aliyataja baadhi ya maeneo yaliyoathirika kuwa ni Buguruni, Vingunguti, Gongo la Mboto, Majohe na Tabata.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Dk. Sylivia Mamkwe, alisema katika Kambi ya Temeke watu watatu pekee ndio waliolazwa huku wanne wakiruhusiwa kwenda nyumbani. Maeneo yaliyoathirika katika wilaya hiyo ni Keko na Mtoni kwa Azizi Ali.

Jumanne wiki hii, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid (pichani) alitoa agizo la kupiga marufuku biashara ya uuzaji chakula kiholela bila kuzingatia usafi na maji ya kunywa maarufu kama kandoro Jijini Dar es Salaam na mkoani Morogoro
CHANZO: NIPASHE

No comments: