ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 27, 2015

Mdahalo wa Uchaguzi Mkikimkiki 2015 wazinduliwa Vyama vikuu vya siasa kujadili sera zao

25 Agosti, 2015, Dar es Salaam: Twaweza inatangaza uzinduzi wa midahalo iitwayo Mkikimkiki 2015. Midahalo hii imeanzishwa ili kutoa fursa na jukwaa kwa vyama vya siasa kunadi sera zao kwa wananchi. Aidha midahalo hii tawapa wananchi fursa ya kuwahoji na kuwapima wagombea na wataalamu wa vyama vikuu vya siasa.

Mfululizo huu wa midahalo umekuja wakati muafaka. Utafiti ulidhaminiwa na Twaweza, uligundua kuwa wananchi 8 kati ya 10 wanafikiri kuwa wagombea ubunge (78%) na urais (79%) wanapaswa kuwa na midahalo ya pamoja. Mbali na mikutano ya hadhara ya kampeni, wananchi wana nafasi finyu sana ya kuwasikiliza na kuwahoji wagombea na vyama vya siasa kuhusu mitazamo, ilani na sera zao katika nyanja mbalimbali.

Maswali ya wananchi na majibu ya hapo kwa hapo ni fursa muhimu kwa wote kupanua uelewa wa wote kuhusu sera na mipango hiyo..

Wananchi wote wanakaribishwa kuwasilisha maswali yao kupitia mtandao na ujumbe mfupi wa simu (SMS). Vilevile, washiriki wa mdahalo na watazamaji wataweza kuuliza maswali wakati wa midahalo.

Tumeandaa mfululizo wa midahalo minne itakayojikita kujadili ilani za vyama vikuu vitano vya siasa. Midahalo hii itahusu: utaifa; uchumi na kukosekana kwa usawa; huduma za kijamii hususan afya na elimu; na rushwa, utawala bora na uadilifu.

Vyama vitano vya siasa tulivyochagua ndivyo vina wagombea wengi zaidi (ngazi ya ubunge na udiwani) kwenye uchaguzi mkuu ujao. Vimealikwa kutuma wataalam wao kushiriki midahalo itakayojadili maeneo haya muhimu. Wawakilishi hawa watahojiwa na jopo la wataalam wa sekta husika.

Aidha, midahalo mitatu tofauti imepangwa kufanyika kwa ajili ya wagombea nafasi ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Urais wa Zanzibar na Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Kila mdahalo utachukua masaa mawili na nusu, na utarushwa moja kwa moja na Star TV na Radio Free Africa (RFA),  vyombo vya habari vya mshirika wetu, Sahara Media Group. Midahalo imeandaliwa na Compass Communications na kwenye mitandao ya kijamii itaratibiwa na Jamii Forums.

Ratiba ya midahalo ni kama ifuatavyo:

TAREHE
MADA
MSHIRIKI
30 AGOSTI 2015
Utaifa
Mdahalo wa masuala la utaifa kuhoji ilani za vyama
6 SEPTEMBA 2015
Mdahalo wa wagombea Urais wa Zanzibar
20 SEPTEMBA 2015
Elimu na Afya
Mdahalo wa masuala la elimu na afya kuhoji ilani za vyama
27 SEPTEMBA 2015
Uchumi, ajira na usawa
Mdahalo wa masuala la uchumi, ajira na usawa kuhoji ilani za vyama
4 OKTOBA 2015
Mdahalo wa wagombea nafasi ya Makamu wa Rais
11 OKTOBA 2015
Rushwa/uadilifu/ maadili
Mdahalo wa masuala la rushwa na maadili kuhoji ilani za vyama
18 OKTOBA 2015
Mdahalo wa wagombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Aidan Eyakuze, Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza amesema " Wakati huu wa kihistoria nchini Tanzania, ni vyema wananchi wakapata taarifa za kutosha kuhusu jinsi gani wagombea wa nafasi za uongozi wamepanga kushughulikia changamoto zetu. Twaweza na washirika wake imedhamini midahalo hii kuwapa fursa wananchi kuwahoji na kuwapima wagombea, pamoja na ilani na sera za vyama vinavyoomba ridhaa yao kuwaongoza kwa kipindi cha miaka mitano ijayo."

"Takwimu tulizokusanya kupitia 
utafiti wa Sauti za Wananchi na Uwezo, zinaonesha kuwa wananchi wameendelea kusisitiza mambo matatu," aliendelea Eyakuze. "Kwanza, wananchi wana hamu kubwa ya kuona serikali ikifanya kazi vizuri zaidi. Wananchi wengi waliodai kuwa wabunge wao hawakutekeleza ahadi za uchaguzi wanasema hawatawachagua tena wabunge hao. Pili, wananchi wametaja umaskini, na huduma duni za afya na elimu kama changamoto za msingi zinazowakabili. Tatu, licha ya changamoto hizi, wananchi wana matumaini makubwa kwamba maisha yao yataboreshwa na uongozi bora pamoja na juhudi zao. Kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mkuu huu wa kipekee, ikiwa ni pamoja na kuwahoji wagombea, ni njia muhimu ya kuchochea mabadiliko chanya. Mkikimkiki 2015 inatoa fursa pana na ya bure kabisa kwa vyama vya siasa, pamoja na wagombea wao, kukutana na wapiga kura, na kunadi dira, vipaumbele and sera zao moja kwa moja. Tunatarajia ushiriki wao mzuri na wenye hamasa kubwa."
Vyombo vya habari vinakaribishwa kushiriki lakini lazima wajiandikishe kabla ili kufanya hivyo. Tafadhali tuma barua pepe kwa pr@compass-tz.com au piga simu +255 768 129974. Hakutakuwa na posho zozote zitakazotolewa kwa washiriki.
----Mwisho----
Kwa taarifa zaidi wasiliana na:Risha Chande
Mshauri Mwanadamizi wa Mawasiliano, Twaweza 
e:
 
rchande@twaweza.org |Simu: (+255) (0) 656 657 559

No comments: