ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 27, 2015

KUMTAFUTIA MCHUMBA ISIWE NONGWA

ASSALAAM aleikum na Bwana Yesu asifiwe wapenzi wasomaji wangu. Bila shaka ni wazima wa afya na mnaendelea vema na kazi za kulijenga taifa letu hili ambalo kwa sasa linapita kwenye mchakato mzito wa kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu.

Nafurahishwa na jinsi mnavyoungana na mimi kunisoma na kunirudishia maoni yenu. Hakika nitaendelea kuwaelimisha kwa kila ninachoona kinafaa kuwafikia ili kuwekana sawa ndani ya maisha ya uhusiano.
Leo nimekuja na mada hii; kumtafutia mchumba isiwe nongwa, mwache atulie na ndoa yake. Nimeamua kuyasema hayo kwa sababu imekuwa kero kwa watu wengi ambao wametafutiwa wachumba.

SIPENDI HIVI

Tabia ya kuchaguliwa mchumba mazao yake ni manenomaneno. Tena maneno yenye kukera wakati mwingine. Inafika mahali unaweza kusikia mtu akisema, ‘bila mimi wewe asingeolewa’. Au, ’bila mimi wewe usingemuoa fulani.’
Hivi wewe ni Mungu mpaka useme hivyo? Unajuaje huyo uliyemtafutia ni Mungu ndiye amekuongoza wewe kufanya hivyo? Kwa nini usikae na kusubiri thawabu yako kutoka kwa Mungu kwa kujitolea kwako kumtafutia mchumba huyo mwenzako, ndugu yako, rafiki yako?

WENGINE HUGEUZWA ATM

Kuna baadhi ya watu wakimtafutia mchumba msichana au mvulana basi wanalifanya tendo hilo kama mtaji au ATM ya kuchumia au kufaidika na uhitaji wake. Akiwa na shida zake anataka amaliziwe na huyo tena kwa amri.
Akiulizwa nini, anasema, ‘si nimemuweka mahala pazuri hivi hamjui kuwa riziki ya mtu hupitia kwa mtu?’

MPAKA KUPITILIZA

Utakuta mwanamke ndiye amemtafutia mchumba mwanamke mwenzake. Mungu akabariki, ndoa ikafungwa. Sasa huyo mtafuta mchumba kapata shida, basi anaamua kwenda kuomba kwa mume moja kwa moja bila kumshirikisha yule aliyemuunganisha. Hivi unasahau kuwa mwanaume au mwanamke hawezi kutoa kitu bila kuongea na mwenzake? Na kwa nini akupe wewe kipaumbele kama ulishawaunganisha na kumaliza kazi yako?

HAWA WANANISHANGAZA ZAIDI

Mwingine anataka aliyemuunganishia akinunuliwa dela na yeye anunuliwe. Akinunuliwa kanga na yeye anunuliwe. Hii si sawa kabisa. Kumbuka huwezi kulinganishwa na mke. Huyo amekwishakuwa mke. Kama ulitaka wewe ndo’ ungeolewa basi.

Suala hili nimeamua kuliweka hadharani kwa sababu kuna msomaji mmoja limemkuta. Kuna mwanamke alimtafutia msichana mwanaume, akabahatika kumuoa. Mwanaume huyo ‘mambo safi’. Basi mtafutaji ameamua kumfanya mume kama wake. Ukiuliza nini anasema amemtafutia mwenyewe. Hili si sawa kabisa.

Mbaya zaidi mke akijaribu kuhoji anaambiwa bila huyo asingeolewa huku akilazimisha na mwanamke huyo ampe zawadi kwa sababu alisababisha yeye kuolewa. Sasa limemfika kooni, ameamua kulitoa kwani anaona ni kero.
“Bi. Chau ikafika mahali nikaona ndoa chungu. Moyoni nilikuwa najiuliza nimeolewa mimi peke yangu kama mke mmoja au tumeolewa wake wawili. Kusema kweli nimeamua kusema ili moyo wangu utulie sasa. Na kwa sababu nimesema sasa moyo umetulia kwani najua akisema kwenye sindano za mahaba atajua dongo ni lake.” Hayo ndiyo maneno ya msomaji wangu.

IWE FUNZO

Kila mwanamke anayefanya hivyo hili liwe funzo kwani wao ndiyo wapo mstari wa mbele kusema maneno hayo anapokuwa amempatia mchumba mtu. Ni nadra sana kumsikia mwanaume akiwa na tabia hiyo.
Anataka mtu amfanye yeye kama ndiyo mama mkwe wakati mama mkwe naye ana nafasi yake. Nawaonya! Kama unaona umemsaidia mtu basi subiri shukurani, usiiombe kwa lazima au kama vipi Mungu atakubariki wewe kwa njia nyingine.

Tuonane wiki ijayo kwa mada nyingine.

GPL

No comments: