Advertisements

Wednesday, August 5, 2015

Lowassa anavyowapa Ukawa jeuri kuingia Ikulu

Mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward
By Mwandishi Wetu, Mwananchi
Dar es Salaam.Sasa ni rasmi, waziri mkuu wa zamani, Edward Lowassa ndiye mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chadema. Mwanasiasa huyo mkongwe na ambaye amekuwa gumzo ndani ya CCM, alikitosa chama hicho na kujiunga na upinzani.

Baada ya kujiunga na Chadema, alichukua fomu za kugombea urais na kudhaminiwa na wanachama wapatao 1.6 milioni. Jana alitambulishwa na kupitishwa rasmi na Mkutano Mkuu wa Chadema pamoja na mgombea wake mwenza, Juma Duni Haji.

Wagombea wote wawili ni wapya.

Wakati Lowassa akipokewa kutoka CCM, Juma Duni amejiunga Chadema akitokea CUF katika mkakati maalumu kwa makubaliano ya vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Akiwa CCM, Lowassa alikuwa kada wa kwanza kutangaza nia ya kuwania urais Mei 30 katika mkutano wa hadhara uliohudhuriwa na maelfu ya watu kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.

Katika mkutano huo Lowassa alikumbushia tukio la mwaka 1995 alipojitokeza kugombea urais pamoja na Rais Jakaya Kikwete akisema, “Natarajia safari hii (mwaka 2015), Kikwete ataniunga mkono.”

“Wakati ule sote tulikuwa wanasiasa vijana. Pamoja tulikwenda kuchukua fomu na baadaye kwa pamoja tukazungumza na waandishi wa habari. Tulileta hamasa kubwa pale tulipofanya jambo ambalo halikuzoeleka kwa Watanzania kwa kutangaza kwamba yeyote atakayepita kati yetu, mwenzake ambaye hatafanikiwa angemuunga mkono.”

Waziri Mkuu huyo wa zamani ambaye alichaguliwa kuwa mbunge mwaka 1990, ni kati ya watiania wa CCM walioibua mvutano mkali katika mchakato wa chama hicho kupata mgombea wake, huku akiungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge, viongozi wastaafu wa chama hicho na wenyeviti wa wilaya na mikoa wa CCM. Hiyo ndiyo sababu ya kutoa kauli za kujiamini.

Asiyenipenda CCM aondoke

Akizungumza mjini Dodoma Mei 25, Lowassa alisema iwapo kuna mtu anamchukia ndani ya chama hicho, ni vyema akahama kwa sababu yeye hana mpango huo. “Sina mpango wa kuhama chama changu, sina Plan B, mimi ni Plan A tu, tangu nimemaliza chuo kikuu mwaka 1977, nimekuwa mwana-CCM, sijafanya kazi nje ya CCM ukiondoa miaka ambayo nilikuwa vitani Uganda na nilipohamishiwa Kituo cha Mikutano cha Arusha (AICC). Maisha yangu yote yapo CCM. Kama kuna mtu ambaye hanitaki ndani ya CCM, yeye ndiye ahame, siyo mimi,” alisema.

Sina mpango wa kushindwa

Mara baada ya kuchukua fomu ya kuomba kuteuliwa kuwania urais kupitia CCM mjini Dodoma Juni 5 mwaka huu, Lowassa alisema hana mpango wa kushindwa. “Swali rahisi sana, sina mpango wa kushindwa,” alisema Lowassa alipokuwa akijibu swali aliloulizwa na waandishi wa habari kama ana mpango mbadala ikiwa angeenguliwa na CCM.

Anayemtuhumu kwa ufisadi amtaje

Siku ya uchukuaji wa fomu, Lowassa aliyekuwa akijibu kwa kifupi maswali ya wanahabari, alisema kama kuna mtu ana ushahidi na tuhuma za ufisadi dhidi yake ajitokeze hadharani. “Kama hawakunitaja hawakunihusisha… Mtu anayejiamini aseme, na anitaje. Nachoka na siasa za tuhuma, hatupimi viongozi kwa rekodi za matusi,” alisema.

Alipoulizwa kuhusu uteuzi wa baraza lake la mawaziri iwapo atakuwa rais, Lowassa alisema, “Nitavuka daraja nitakapolifikia.”

Kwa mapokezi haya nimeshashinda

Juni 6 mwaka huu akiwa mjini Mwanza kusaka wadhamini, Lowassa alianza hatua hiyo ya mwisho ndani ya CCM kuelekea kugombea urais kwa kupata mapokezi makubwa yaliyomshawishi kusema; “Kama ni mpira, tayari nimeshinda kwani sijawahi kupata mapokezi makubwa kama haya Mwanza. Nina sababu kuu mbili za kusema kwamba nadeka na kama ni mpira nimeshinda. Mapokezi niliyoyapata hapa Mwanza hayajawahi kutokea, lakini hii ni faraja kubwa ya pekee kwangu,” alisema Lowassa baada ya kukabidhiwa fomu hiyo.

“Leo sitasema sana, lakini nawaomba wanaccm tujenge mshikamano wa pamoja kukabilina na vita ya watu watakaokomba rasilimali za Taifa.”

Pia, alisema Uchaguzi Mkuu wa Oktoba utakuwa mgumu tofauti na uliopita na kwamba, ni mtihani kwa CCM kuteua mtu makini atakayaweza kulinda rasilimali za nchi. Lowassa alisema huu ni wakati wa CCM kujenga mshikamano wa pamoja na kukabiliana na watu ambao wanaweza kukomba rasilimali za nchi.

Muda wa mabadiliko umefika


Juni 20, Alikuwa mjini Iringa ambako alisema kuwa muda wa mabadiliko aliyotabiri Mwalimu Julius Nyerere ni sasa na kwamba yeye ndiye anayeweza kuyaongoza. Alisema kwa sasa CCM inahitaji mabadiliko makubwa na akanukuu kauli ya Mwalimu Nyerere aliyoitoa mwaka 1995 alipozungumzia haja ya chama hicho kujisahihisha.

“Baba wa Taifa alisema kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM,” alisema mbunge huyo wa Monduli kwenye mkutano huo uliofanyika Uwanja wa Samora mjini Iringa. “Huu ni wakati wa mabadiliko. CCM ikijipanga inaweza kuleta mabadiliko na mtu wa kuleta mabadiliko hayo ni mimi,” alisema.

Lowassa alisema aliamua kuingia kwenye mbio za urais kwa sababu tatu: Kufanya mabadiliko ndani ya CCM, kufanyia kazi tatizo la umaskini na kushughulikia tatizo la ajira kwa vijana.

Hakuna wa kumkata

Juni 22, akizungumza mara baada ya kuwasili mkoani Ruvuma alisema hatarajii jina lake kukatwa katika vikao vya CCM vitakavyoketi kumteua mwanasiasa atakayepeperusha bendeara ya chama hicho katika kinyang’anyiro cha urais.

“Nimekuwa mwanaccm tangu mwaka 1977 nilipomaliza chuo kikuu, sijawahi kufanya kazi nje ya CCM, hivyo nakijua chama na hakuna mgombea atakayeweza kuvunja rekodi ya utendaji wangu katika chama, sasa leo anayetaka kukata jina langu anatoka wapi? Anakata kwa sababu gani? Sioni kosa la kukatwa jina na Watanzania hawaoni, kwa hiyo msiwe na wasiwasi jina litarudi tu,” alisema.

CCM ikijipanga itashinda


Juni 25, alikuwa mjini Babati na kusema iwapo CCM itajipanga vizuri ikamaliza migogoro na kujiamini, itashinda mapema katika uchaguzi. “Tukijipanga vizuri, tukajiamini tukaacha ugomvi katika umoja wetu huu, tutashinda uchaguzi mapema dhidi ya watani wetu,” alieleza. Alisema iwapo jina lake lingepitishwa, uchaguzi mkuu ungekuwa umekwisha mapema kutokana na kuwa na ushawishi mkubwa kwa wapigakura nchini.

Pamoja na kauli hizo jina la Lowassa lilikatwa tena katika hatua ya awali kabisa. Kamati ya Maadili na Usalama ndiyo ilifyeka jina lake wakati kanuni zinataka kamati hiyo iwasilishe majina kwa Kamati Kuu yenye jukumu la kukata. Mzozo umeanzia hapo. Hasira zilionekana hapo na mpango mbadala ambao hakuwa nao ulianza kujengwa hapo.

Mpango B

Kutokana na kujiamini sana, Lowassa hakuwa na mpango mbadala hivyo alitoa kauli hizo akidhani makubaliano yake na Rais Kikwete ya mwaka 1995 yangeheshimiwa. Alipata nguvu wabunge waliposhangilia kwa nguvu Rais Kikwete alipomshukuru kwa utumishi wa miaka miwili kama waziri mkuu. Hata hivyo, alipokatwa alilazimika kuungana na waliokuwa maadui wake kisiasa, Chadema ili kufufua safari anayoiita “ya matumaini”.

Utumishi wake

Katika miaka miwili ambayo amekuwa waziri mkuu, Lowassa alionyesha mfano wa namna ambavyo mtendaji na msimamizi mkuu wa shughuli za Serikali anavyopaswa kuwa. Lowassa alikuwa mfuatiliaji. Aliwafuatilia kwa karibu wakuu wa mikoa na wilaya na wakurugenzi hadi akafanikisha ujenzi wa shule za sekondari za kata, na uboreshaji wa barabara za jiji la Dar es Salaam.

Pia, amekuwa kiboko cha wawekezaji wababaishaji. Mwaka 2003 alipokuwa Waziri wa Maji aliifutia mkataba kampuni ya City Water Services.

Wasifu wa Lowassa

Edward alizaliwa Agosti 26, 1953 katika kijiji cha Ngarash, Monduli na ndiye mtoto mkubwa wa kiume kwa Mzee Ngoyai Lowassa (atafikisha miaka 62 Agosti mwaka huu). Alianza kusoma katika Shule ya Msingi Monduli kati ya mwaka 1961–1967.

Aliendelea katika Shule ya Sekondari Arusha kwa masomo ya kidato cha kwanza mpaka cha nne kuanzia mwaka 1968 - 1971, kabla ya kumalizia kidato cha tano na sita katika Shule ya Sekondari Milambo mkoani Tabora mwaka 1972–1973.

Alijiunga na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1974–1977 na kuhitimu Shahada ya Sanaa katika Elimu (B.A Education) na baadaye Chuo Kikuu cha Bath Uingereza kwa Shahada ya Uzamili ya Sayansi katika Maendeleo (mwaka 1983–1984).

Baada ya kumaliza chuo kikuu, Lowassa alifanya kazi ndani ya CCM akiwa ofisa wa ngazi ya juu kuanzia wilaya, mkoa na baadaye makao makuu kati ya mwaka 1977–1989. Aliajiriwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Arusha (AICC), mwaka 1989–1990.

Amewahi kuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Haki na Mambo ya Bunge); Waziri wa Ardhi na Makazi; Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira na Kuondoa Umasikini) na Waziri wa Maji na Mifugo.

Aliteuliwa na Rais Kikwete kuwa Waziri Mkuu mwaka 2005, uwaziri ambao ulikoma Februari 2008, alipojiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond. Ana uzoefu wa zaidi ya miaka 38 ya kuitumikia CCM na Serikali.

Lowassa amemuoa Regina na wana watoto watano; wasichana wawili na wavulana watatu. Watoto hao ni Fredrick, Pamella, Adda, Robert na Richard.

1 comment:

Anonymous said...

dr slaa ndi peke yake mkombozi wa nchii hii na wanyonge hataki mambo yakijinga jinga.mnapenda pesa ya lowassa na kuuwa upinzani.
mnajuaje kama hawa wote wamekuja kuuwa upinzania.mnawapokea tu watu hivi hivi.kweli ukawa mazuzu wote bara na visiwani.
ccm wanasuka mipango wanajidai kuwafukuza mnawaonea huruma halafu mnawaingiza kwenye vyama vyenu wanasoma mbinu zenu zote wanakuja kukumalizeni.

useless ukawa.bora mtu ufanye yako mambo ya siasa unaweka kando ni vizuri kujifunza lakini wote ni sawa tu hakuna kitu hapo kwa upeo wangu wa mawazo yangu sijui wenzangu wenye akili za kupewa pesa na mwaka wa kuvuna kanga,vitenge,kofia.

na ahadi za hewa.