- UTANGULIZI
- Tangazo hili linatolewa kwa lengo la kutoa mwongozo kwa watoa huduma za helikopta, marubani wake na umma kwa ujumla kuhusiana na hatua za kiusalama zinazopaswa kuzingatiwa inapolazimika kutoa huduma ya usafiri wa helikopta hapa nchini, hususani, maeneo ya mbali (vijijini) ambapo huduma za uongozaji ndege hazipo au sio maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya helikopta kutua (mahsusi kwa helikopta au viwanja vya ndege kwa ujumla). Tangazo hili limetolewa baada ya Mamlaka kugundua kwamba kumekuwa na matumizi mabaya ya huduma hizi kinyume na kanuni za usafiri wa anga nchini na weledi unaozingatia taratibu za kitaaalamu na miongozo katika usafiri wa anga.
. - Mamlaka inatambua kwamba matumizi ya helikopta wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 yanatarajiwa kuongezeka na kuna uwezekano wa kuleta athari za kiusalama kwa maisha ya watu na mali pamoja na watumiaji wa vyombo hivi. Pia vitendo vya kuning’iniza vitu kama mabango ya matangazo mbalimbali kwa kutumia ndege (helikopta ikiwemo) yanaweza kuleta hatari endapo sheria na taratibu zinazohusiana na matumizi hayo hazitazingatiwa.
- Tangazo hili linatolewa kwa mamlaka aliyopewa Mkurugenzi Mkuu chini ya Sheria Namba 80 ya Usafiri wa Anga na kanuni zake zinazohusiana na masuala ya usafiri wa anga nchini zilizowekwa kwa lengo, hususan, kuhakikisha usalama katika matumizi ya vyombo vya usafiri wa anga sambamba na kulinda usalama wa umma na mali wakati wa matumizi ya vyombo husika.
- Watoa huduma za usafiri wa helikopta au ndege na marubani wake wanaokodishwa kutoa huduma wakati wa kampeni, na mtu yeyote anayetarajiwa kutumia huduma hiyo wanakumbushwa kuhakikisha wanazingatia kanuni za usafiri wa anga na ikibidi kuomba kibali kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania. Kanuni zinapatikana kupitia tovuti yetu kwa anuani ya:www.tcaa.go.tz; na endapo utahitaji maelezo ya ziada au miongozo zaidi usisite kuwasiliana na Mamlaka.
- Tangazo hili linatolewa kwa lengo la kutoa mwongozo kwa watoa huduma za helikopta, marubani wake na umma kwa ujumla kuhusiana na hatua za kiusalama zinazopaswa kuzingatiwa inapolazimika kutoa huduma ya usafiri wa helikopta hapa nchini, hususani, maeneo ya mbali (vijijini) ambapo huduma za uongozaji ndege hazipo au sio maeneo maalum yaliyotengwa kwa ajili ya helikopta kutua (mahsusi kwa helikopta au viwanja vya ndege kwa ujumla). Tangazo hili limetolewa baada ya Mamlaka kugundua kwamba kumekuwa na matumizi mabaya ya huduma hizi kinyume na kanuni za usafiri wa anga nchini na weledi unaozingatia taratibu za kitaaalamu na miongozo katika usafiri wa anga.
- CHETI CHA NDEGE KWA USALAMA WA KURUKA – AIRWORTHINESS CERTIFICATE
- Helikopta yeyote itakayotoa huduma katika kampeni za kisiasa lazima iwe ina cheti halisi cha usalama wa kuruka kilichotolewa na mamlaka husika ya helikopta ilikosajiliwa. Kwa hapa nchini cheti hicho ni lazima kiwe kimetolewa na Mamlaka ya Usafiri wa Anga. Na cheti hicho ni lazima kiwe kimetolewa kwa ajili ya helikopta yenye usajili na mahsusi kwa kazi ya kubeba abiria ambayo inaweza kutumika kwa shughuli nyingine zozote. Kwa tangazo hili helikopta nyingine yeyote ile isiyokuwa na sifa hiyo haiwezi kutumika kufanya biashara ya usafiri wa abiria katika kampeni.
- Endapo helikopta itakuwa ina usajili wa nje ya Tanzania, mtu anayetarajia kuitumia hapa nchini ni lazima apate kibali cha kuiingiza nchini na kuitumia kwa usajili wa nchi iliyotoka kama ilivyoainishwa katika Waraka wa Mamlaka unaoainisha taarifa za usafiri wa anga – Aeronautical Information Circular (AIC 08/09). Hakikisha unapoomba kibali uwe umekidhi vigezo vya waraka huu ikiwa ni pamoja na kuwasilisha nakala za nyaraka zinazopaswa kuwasilishwa zikiwemo cheti cha usajili wa ndege, cheti cha ndege kwa usalama wa kuruka, cheti cha leseni za radio za ndege, cheti cha bima, makubaliano/mkataba wa kukodisha ndege hiyo, utaratibu wa kufanya matengenezo ya ndege hiyo, leseni za marubani, na ushahidi wa karibuni wa matengenezo ya ndege hiyo.
- TARATIBU ZA USALAMA WA UENDESHAJI
- Mahitaji ya jumla ya kiuendeshaji
Matakwa ya marubani na uendeshaji unatakiwa kufuata maelekezo husika yaliyomo kwenye Kanuni inayohusiana na uendeshaji, yaani, The Civil Aviation (Operation of Aircraft) Regulations. Rubani Mkuu anawajibika kuhakikisha kwamba vituo vya Mamlaka vya kuongoza ndege vinavyohusika katika eneo atakalokuwepo au kwa utaratibu wa uongozaji ndege, wanakuwa na taarifa za mpango wake mzima wa safari husika kwa siku au wakati husika.
Njia itakayotumiwa na rubani izingatie matakwa ya kuepuka kuruka chini ya kiwango cha umbali unaotakiwa hasa katika maeneo yenye watu wengi yakiwemo maeneo yaliyopangwa kufanyika kwa mikutano husika.
Tahadhari ni lazima zichukuliwe wakati wa kuelekea kutua, kutua kwenyewe na hata wakati wa kuondoka, hasa ikizingatiwa kuwa kuna uwezekano wa wananchi kuikimbilia helikopta au eneo la utuaji. Katika hali yeyote ile rubani hapaswi kutumia chombo chake kukusanya wananchi kwa ajili ya mkutano au kuitumia kwa utaratibu wowote mwingine kinyume na matakwa ya kiurukaji kwa ndege husika. - Usalama wa eneo la kutua na kuruka
Maeneo yote yatakayotumika kwa ajili ya kutua ama kuruka ni lazima yafahamike mapema. Maeneo ya kuruka ama kutua ni lazima yawe mbali na eneo mkutano utakapofanyika ili kuweza kutoa eneo salama kwa ajili ya kuruka ama kutua kutoka katika mikusanyiko ya watu.
Maeneo ambayo yatatambuliwa kama ni ya kuruka ama kutua hasa yale ambayo hayajatambulika kisheria kwa kufanyia shughuli hiyo ni lazima yawekewe alama maalum na uzio ili kuzuia watu wasiohusika kusogelea eneo hilo.
Eneo husika ni lazima lilindwe; rubani mkuu ahakikishe helikopta itakayokuwa imetua eneo hilo inalindwa dhidi ya uvamizi kutoka kwa watu wasiohusika. Hatua maalum za kiulinzi ni vyema kuchukuliwa endapo kutakuwa na ulazima wa chombo hicho kulala katika eneo husika usiku mzima. Kila wakati rubani anapotaka kuruka ni vyema ahakikishe amekagua chombo chake kwa mujibu wa taratibu zinazohusika kwa umakini kabla ya kuanza safari. - Usiamizi wa Chombo kikiwa ardhini na usalama kwa umma
Mtu mwenye wajibu wa usimamizi wa chombo kikiwa ardhini lazima awe ni mwenye mafunzo ya kutosha na awe anajua madhara yanayoweza kusababishwa na mapanga ya helikopta yanapozunguka. Kwa marejeo zaidi kuhusiaha na hilo tafadhali zingatia yaliyomo kwenye Waraka wa Mamlaka AIC33/2000 unaoelezea masuala ya madhara yanayoweza kusababishwa na mapanga ya helikopta yanayozunguka.
Ni wajibu wa Rubani mkuu na mhusika aliyekodisha helikopta kuhakikisha wananchi wanakuwa salama na mbali na helikopta. Matumizi ya kizembe na yasiyo ya kiweledi ya helikopta yatakayohatarisha usalama wa wananchi yatachukuliwa kama ukiukwaji wa kanuni za usafiri wa anga na Mamlaka itawachukulia hatua kama ilivyoanishwa kwenye kanuni hizo. - Kuchukua na kuangusha vitu ardhini na kupeperusha mabango angani
Huduma hizi zinaweza kufanywa na helikopta na hata ndege zingine za kawaida. Kabla ya kufanya shughuli za namna hiyo, mmiliki wa chombo ni lazima ahakikishe anakidhi vigezo vya Kanuni za Usafiri wa Anga kwa huduma hizi, yaani, The Civil Aviation (Aerial Work) Regulations na pia awe amepatiwa kibali kutoka Mamlaka ya Usafiri wa Anga kwa kazi hiyo. Mmiliki wa ndege yeyote anayefanya shughuli za namna hii bila ya kuzingatia vigezo vya Kanuni hizi atachukuliwa hatua. - Kutoa taarifa za matukio
Rubani Mkuu ni lazima aandike taarifa ya matukio na kuiwasilisha Mamlaka ya Usafiri wa Anga kama ilivyoanishwa kwa mujibu wa kanuni za usafiri wa anga hususan, kanuni za 52, 74,75 na 76 zilizomo kwenye Kanuni ya The Civil Aviation (Operation of Aircraft) Regulations. Wananchi nao wanatakiwa kutoa taarifa ya tukio lolote waliloliona hatarishi kwa mujibu wa kanuni namba 262 ya Kanuni iliyotajwa.
Mamlaka itafuatilia na kuchunguza taarifa inazozipokea na kuchukuwa hatua stahiki ili kuhakikisha kuwepo kwa usalama wa kiuendeshaji, watu na mali.
- Mahitaji ya jumla ya kiuendeshaji
- HITIMISHO
Ili kulinda usalama wa wananchi, wamiliki na marubani wote wanapaswa kuhakikisha wanazingatia Sheria ya Usafiri wa Anga pamoja na Kanuni zake. Rubani anayeendesha chombo ni lazima ahakikishe anatumia weledi wa hali ya juu katika matendo yake.
Mamlaka inawahakikishia wananchi/umma kwa ujumla kwamba haitosita kuchukuwa hatua stahiki kama zilivyoanishwa kisheria na kanuni za usafiri wa anga iwapo mapungufu ya usalama yatajitokeza.
Imetolewa na
Charles M. Chacha
Kaimu MKURUGENZI MKUU
MAMLAKA YA USAFIRI WA ANGA TANZANIA
11 comments:
ni shida mamvi kazi anayo
HUU NI UHUNI WA SERIKALI YA CCM NA HAUKUBALIKI. KWANI ANGA KAZI YAKE NI NINI NA WANAOANGALIA USALAMA WA ANGA SI NDIO NINYI KWANI KAMPENI ZINAFANYIKA ANGANI AU KWENYE VIWANJA MNAVYOZUIA. YAANI MNATAFUTA KILA MBINU ZA KUUA DEMOKRASIA. Mheshimiwa J. KIKWETE unaipeleka nchoi unakotaka na amri hizo zote zinatoka kwako kw ajili ya kupandikiza yule uliyemtaka tume imesema kuwe na kampeni za haki na amani leo inakuwaje vitendo hivi vinaana leo wakati kampeni zimeanza na ni wiki moja tu je kweli kuna amani hapo/ Hebu acheni kukiuka haki za binadamu wengine nao wana haki kufanya hayo mnayofanya. kwani CCM mnataka mtawale hadi mfe wote muishe.???
Napenda nchi ya demokrasia lakini kama nchi yangu imeamua kuwa hivi inabidi niiteme uliwimbo wa taifa sasa hauna maana kama Viwanja haviwezi tumika, mitaani hauwezi tembea na angani tena huwezi ruka demokrasia iko wapi kisa ccm. Tuone kama mtashinda
Watu wengine waaangalie hivo hivo, wanaogopa mabaya yao yatajulikana baada ya October, sasa ndio maaana wanafanya hivo. Alafu wanajifanya wachamungu na wapenda haki . Tuzidi kuomba siku moja nyuso zao zitaonyesha soni.
Sioni tatizo hapa hakuna mtu aliyekatazwa kuruka ni kwamba tuu mamlaka inawakumbusha kufuata sheria hasa kipindi cha uchaguzi maana Helicopter zitakuwa nyingi mambo ya haki za binadamu sijui yanausikaje hapa!!
wewe anonymous wa 5:02pm hata kusoma huwezi!!! hakuna aliyezuiwa, mamlaka ya anga inasema ukitaka kutumia helikopta omba kibali na ndio sharia iliyopo, sasa kipi hapo hamjakielewa acha kutoa mapovu. mnaaanza kutoka jasho, betri ya magufuli imejaa. ya lowasa maji yamekwisha hata haichaji.
ccm wao wameruhusiwa kurusha za kwao bila kibali.
ndio maana mimi sitaki tena KUWA Mtanzania! Hata kama uwezo wa kuwa na uraia wa nchi mbili utakuwepo, KITENDO cha serikali YA CCM kufanya HIVI kimenifanya niseme mimi NA TANZANIA yenye UDIKTETA wa kikwete BASI. SITAKI KUITWA MTANZANIA TENA!
Usalama wa Anga ni moja ya maeneo muhimu katika taifa lolote duniani, ikiwemo Tanzania. Tatizo kubwa ninaloliona ni uvivu mkubwa wa kufikiri miongoni mwa Watanzania wenzangu. Mamlaka husika inatimiza wajibu wake kwa kutoa angalizo na mwongozo wa safari za anga, wasiofikiri vema wanalaumu na kuhusisha na Siasa. Ikiruka helikopta bila ya kuongozwa kisha igongane na Ndege ya abiria mtakuwa wa kwanza kulaumu. Acheni ushabiki wa kisiasa katika mambo muhimu kwa Taifa.
Una tatizo la kutofikiri wewe. Usalama wa anga ni muhimu kuliko siasa za kizushi unazoshabikia
Usalama wa Anga ni moja ya maeneo muhimu katika taifa lolote duniani, ikiwemo Tanzania. Tatizo kubwa ninaloliona ni uvivu mkubwa wa kufikiri miongoni mwa Watanzania wenzangu. Mamlaka husika inatimiza wajibu wake kwa kutoa angalizo na mwongozo wa safari za anga, wasiofikiri vema wanalaumu na kuhusisha na Siasa. Ikiruka helikopta bila ya kuongozwa kisha igongane na Ndege ya abiria mtakuwa wa kwanza kulaumu. Acheni ushabiki wa kisiasa katika mambo muhimu kwa Taifa.
Post a Comment