ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 11, 2015

Prof. Lipumba Amechoshwa na Ukawa au Chama Chake Cha CUF?

lipumba 3
Prof. Ibrahim Haruna Lipumba

NASHANGAA, kwa nini msomi kama Prof. Ibrahim Haruna Lipumba anatafuta uongo kuuficha utashi wake ambao kimsingi ndiyo uliomfanya awe mwanamageuzi na kukubali kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (Cuf)?

Usomi siyo kuwa na vyeti ni uwezo au maarifa ya kukabiliana na changamoto za maisha. Nilitaraji kumuona Prof. Lipumba akifikia tafsiri hii baada ya kubaini kuwa Umoja wa Katiba ya Mwananchi (Ukawa) alimokitumbukiza chama chake lilikuwa ni kosa lililohitaji maarifa kulitatua.

“Nimeamua kujiondoa kwenye nafasi ya uenyekiti kwa sababu wenzangu wameniona kuwa ni kikwazo…Watu walioipinga katiba tuliyoipendekeza ndiyo tunaowapa nafasi ya kuongoza umoja wetu.”

Haya ni maneno ya Prof. Lipumba aliyoyatoa wakati akijiuzulu wadhifa wake wa uenyekiti wa Cuf, maneno ambayo sikuyapangilia ipasavyo kwa sababu nilichotaka kukiweka ni sura tu ya namna alivyoachia ngazi.

Wakati akitangaza uamuzi huo sikuwepo kwenye mkutano wake, nadhani hakuniita makusudi kwa sababu ananifahamu kuwa mimi ni mbishi, sipendi kudanganywa, pengine ningemuuliza maswali magumu ya kumchefua:

“Unajiondoa Ukawa au Cuf? Wewe siyo mwenyekiti wa Ukawa ni wa Cuf! Kwa nini usikitoe chama chako kwenye umoja huo haramu badala yake umejitoa wewe kana kwamba waliokupa kura ya uwenyekiti ni hao Ukawa unaowakimbia?

“Huoni Prof. Lipumba kufanya hivi kunakuondolea heshima mbele ya watu waliokuamini na kukupenda kwa miaka zaidi ya 20 katika harakati zako? Unawezaje kuhama nyumba kwa kufukuzwa na mpangaji mwenzako huku ukiwaacha wanao kwenye huzuni kubwa?”

Haya ndiyo maswali ambayo ningemuuliza mfululizo Prof. Lipumba kwa sababu katika akili yangu sijaona mantiki ya yeye kuachia cheo cha uenyekiti wa Cuf kwa sababu eti ameonekana kikwazo cha Ukawa; kwani Ukawa ni Cuf na Cuf ni Ukawa?

Akili ya kawaida lazima ilete majibu ya mshangao vinginevyo mwenyekiti huyo afanye masahihisho ya kauli yake kwa kusema kuwa waliomuona kikwazo siyo Ukawa bali ni viongozi wenzake ndani ya chama chake, hapo atakuwa na sababu ya kuachia ngazi ya uenyekiti wa Cuf.

Ikiwa hivi ninavyosahihisha kauli ndivyo ilivyo kwamba, Prof hakukubaliana na utaratibu wa chama chake kujiunga Ukawa na viongozi wenzake wa chama wakaona ‘anawazingua’ kwa nini asiseme wazi kuwa ameamua kuachia ngazi baada ya kupingana na viongozi wenzake?

Kulikuwa na ubaya gani kuwaita waandishi wa habari na kutamka hadharani kwamba, katibu mkuu wake, Maalim Seif Sharrif Hamad, amempuuza na kwamba yeye hakuwa tayari kufanyiwa hivyo kwa masilahi ya chama chake? Hapo angeieleza jamii jinsi alivyojitahidi kutatua tatizo hilo, alivyowashirikisha wananchama waliomchagua na namna ilivyoshindikana kiasi cha kufikia kuachia ngazi, hapo angeeleweka na kila mtu!

Lakini kutoa hoja dhaifu kwamba hicho ndicho kikwazo cha nafasi yake nyeti ndani ya chama, hawezi kukwepa tuhuma kwamba amenunuliwa na chama tawala kwa lengo la kuhujumu Ukawa.

Hawezi kukwepa kejeli kwamba maisha ya upinzani kayazoea na kwamba amekuwa hapendi kukiona chama chake kikiwa na nguvu ya kushika dola.

Prof. Lipumba hatakaa ajisafishe na mtazamo kuwa siasa za kashkashi ndani ya upinzani zilikuwa zimemlevya na kwamba alikuwa anasubiri kusukumwa kidogo aanguke, puuu!

Nasikitika Prof. Lipumba amehama nyumba kwa kufukuzwa na mpangaji mwenzake, ameamua kuwaacha wanachama waliopigana kwa kumwaga damu katika changuzi mbalimbali na wengine ni vilema mpaka sasa kwa sababu yake!

Ikiwa ni hivi, siasa na wanasiasa siyo watu wa kuwaamini hata kidogo. Nachochea tu!

GPL

3 comments:

Anonymous said...

Mdau, muwaache Prof. Lipumba na Dr. Slaa wapumzike kwa Amani. Nyie mliohongwa mabilioni na Lowasa endeleeni na safari yenu isiyo na matumaini! Hamtaweza kuinunua dola, hata kama Lowasa atauza ng'ombe wote kula umasaini.

Anonymous said...

Hii si safari tena ya matumaini ni safari ya uhakika.mtataga mwaka huu.lowassa ndo habari ya mujini umeona yale mafuriko yakuchukua formu tu.

na mkiiba kura mtakiona cha mtema kuni.mafuriko hayazuiliki.

professor mzima anadanganywa na wasio soma;washereheshaji what a shame na asepe tu.

wanyamwezi,wa muha na wahaya si watu wakuaminika.ni snitches sana.makabila haya lazima watakusaliti tu wanatabia hizo;na ni wafitinishaji/wana majungu sana

becareful with them

Anonymous said...

Acha ushabiki wa kitoto anony. #2. Ukileta ukabila basi Ukawa hamtachukua dola kwani ni Wachaga, wamasai, na wale wafaa njaa wanaopenda kuishi katika jiji la Dar ndo tegemeo la Ukawa/Chadema. Nakuhakikishia mdau kuwa mikoani kote ni CCM, kwani wananchi/wakulima wameshamjua kiongozi wenu ni FISADI aliyekimbia toka CCM. Muwe pole, mnadhani atawaokoa, wapi! Huyo akianguka Oktoba anakwenda Umasaini kuchunga ng'ombe wake 8,000. Na nyie mashabiki mtafanya nini? Kuwalilia Dr.Slaa na Prof. Lipumba warudi nyumbani tena?