Advertisements

Monday, September 14, 2015

KIFO CHA MTOI NINI KILITOKEA

Aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga, Mohamed Mtoi.

Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, pamoja na makada wengine wa chama hicho, wanatarajiwa kuhudhuria mazishi ya aliyekuwa mgombea ubunge wa Jimbo la Lushoto mkoani Tanga, Mohamed Mtoi (39), aliyefariki dunia juzi usiku kwa ajali ya gari.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene, mazishi hayo yanatarajiwa kufanyika leo saa 7:00 mchana katika kijiji cha Mkuzi Kwekingo wilayani Lushoto.

Alisema ajali hiyo ilitokea juzi usiku wakati marehemu akiwa kwenye gari lake akitokea kwenye kampeni akirudi nyumbani kwake.

UTATA WAGUBIKA
Makene alisema Mtoi ambaye pia alikuwa Mkuu wa kanda mbalimbali za Chadema nchini, alifariki dunia wakati akipata matibabu hospitalini baada ya ajali kutokea.

“Mara baada ya ajali kutokea, hakuwa na majeraha yoyote bali alionekana mwenye mawenge na alifariki dunia muda mfupi baada ya kufikishwa hospitali,” alisema.

“Bahati mbaya alipata ajali akiwa kwenye gari yeye na dereva aliyetoka naye huku makao makuu yetu Dar es Salaam na dereva aliyekuwa anamuendesha wakati wa ajali ambaye hata hivyo, hatumfahamu kwani alikuwa akifahamiana na marehemu pekee,” alisema Makene.

Alisema kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa dereva ambaye alikuwa naye, baada ya ajali hiyo kutokea, kijana ambaye alikuwa akiendesha gari hilo hakuonekana.

“Ametueleza kuwa mpaka ajali inatokea mtu huyo ndiye alikuwa anaendesha gari hilo, lakini baada ya ajali kutokea hakumuona,” alisema.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tanga, Zuberi Mwombeji, alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kumtaja dereva wa gari hilo kuwa alikuwa ni Miraji Nuru (43).

Kamanda Mwombeji alisema Nuru amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Lushoto akiendelea na matibabu.

Alisema kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi na hivyo dereva gari likamshinda na kutumbukia bondeni.

"Ndani ya gari walikuwapo hao wawili tu ambapo baada ya kutumbukia walikimbizwa katika hospitali ya Wilaya ya Lushoto kwa matibabu na ndipo saa 7:00 usiku Mohamed alipoaga dunia," alisema Kamanda Mwombeji.

Hata hivyo, alisema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kujua chanzo halisi cha ajali hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jimbo la Lushoto kupitia Chadema, Dickson Shekivuli, alisema chama hicho kimepokea msiba huo kwa mshtuko mkubwa hasa kwa kuzingatia kuwa juzi ilikuwa ndiyo uzinduzi wa kwanza wa kampeni za ubunge kupitia Ukawa.

Shekivuli alisema marehemu alifanya mkutano wake wa kampeni kwa mara ya kwanza katika kata ya Mlola tarafa ya Mlola wilayani Lushoto saa 9:00 alasiri mpaka saa 12:00 jioni.

Naye Msemaji wa familia, Salim Shemng'ombe, ambaye ni kaka wa marehemu, alisema taratibu za mazishi zinaendelea ambapo wanatarajia maziko kufanyika leo kijijini kwao Mkuzi.

Kwa mujibu wa Shemng'ombe, marehemu ameacha mke na watoto wawili.

Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Lushoto, Jumanne Shauri, ambaye pia ni Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, alisema tayari wameiandikia Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec ) ili kupata mwongozo kuhusiana na kifo cha mgombea huyo.
CHANZO: NIPASHE

1 comment:

Anonymous said...

Hii ni Tanzia kubwa tunawapa pole wana Lushoto wote na waTanzania wapenda maendeleo. Tatizo kubwa la Tanzania kifo kinatokea na hakina uchunguzi wa kina sana inaharakishwa maziko then uchunguzi ?? Wizara husika zijipange kwa usahihi zaidi ya hapo walipo.