Advertisements

Friday, September 4, 2015

Kuiona Stars buku 7, Magufuli aitakia heri.


Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe.


Wakati kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe, ameomba Watanzania waruhusiwe kuingia bure uwanjani kuishangilia Taifa Stars dhidi ya Nigeria kesho, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limetangaza viingilio vikubwa kwa ajili ya mechi hiyo ya kuwania kufuzu fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2017.

Wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho kuhusu uchaguzi mkuu mwaka huu zilizofanyika Mbagala jijini Dar es Salaam Jumapili, Zitto alishauri TFF iruhusu mashabiki waingie bure kwenye Uwanja wa Taifa kuipa sapoti nzito timu ya nyumbani.

Hata hivyo, katika mkutano na waandishi wa habari kwenye ofisi za TFF jijini Dar es Salaam jana, Baraka Kizuguto, ofisa habari na mawasiliano wa shirikisho hilo, atangaza kiingilio cha chini ya Sh. 7,000 huku akimjibu kwa kifupi Zitto kwa kusema: "Tusichanganye siasa na michezo."

Kizuguto alisema maandalizi ya mechi hiyo ya Kundi G yamekamilika huku akieleza kuwa kiingilio cha juu (VIP A) Sh 40,000, VIP B Sh 30,000, VIP C Sh15,000, Rangi ya Machungwa Sh 10,000 wakati viti vya rangi ya Bluu na Kijani Sh 7,000.


Alisema tiketi za mchezo huo zinatarajiwa kuanza kuuzwa leo saa 4 asubuhi katika vituo 10; Ofisi za TFF, Buguruni, Mbagala, Ubungo, Makumbusho, Uwanja wa Taifa, Mwenge, Kivukoni, Posta (Luther House) na Kariakoo (Msimbazi).

Alisema mechi hiyo itakayoanza saa 10:30 jioni kwa saa za Afrika Mashariki, itachezeshwa na waamuzi kutoka Rwanda ambao wanatarajiwa kuwasili jijini jana jioni.

Marefa hao ni Louis Hakizimana (kati), Honore Simba (msaidizi), Jean Bosco Niyitegeka (msaidizi) na Abdoul Karim Twagiramukiza (wa akiba) pamoja na kamisaaa Charles Kasembe kutoka Uganda.

MAGUFULI
Mgombea urais wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), John Pombe Magufuli, ameitakia heri Stars katika mechi yake dhidi ya Nigeria itakayochezwa kesho.

Katika salamu zake rasmi kwa timu hiyo, Magufuli alisema ingawa kila mtu anaamini kuwa mechi hiyo ni ngumu, yeye anaamini kuwa Taifa Stars itawashangaza wengi kutokana na kupata matokeo yasiyotarajiwa.

“Mimi ni mpenzi wa mchezo wa mpira wa miguu na wakati nikicheza mpira nilikuwa napenda kucheza kama golikipa. Nafahamu kuwa wakati wa mechi ngumu, wachezaji hujituma zaidi kuliko mechi ikiwa nyepesi," alisema na kuongeza:

“Mechi dhidi ya Super Eagles (Nigeria) ni miongoni mwa mechi kubwa barani Afrika na duniani pia. Kama Stars itashinda, dunia nzima itajua na kwa sababu hiyo naamini wachezaji watajituma zaidi ili kupata matokeo mazuri. Ndiyo maana nina matumaini na timu yetu.”

Stars inacheza na Nigeria katika pambano linalosubiriwa kwa hamu na washabiki wa soka nchini na Magufuli alisema ama uwanjani au nje ya Uwanja wa Taifa wakati mechi hiyo itakapochezwa, ataifuatilia kwa karibu.
CHANZO: NIPASHE

No comments: