Advertisements

Thursday, September 10, 2015

Maaskofu wapongeza karipio la NEC

SIKU moja baada ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kukemea kitendo kilichofanywa na mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa cha kuomba kura kwa kuwataka waumini wa madhehebu ya Kilutheri, kumchagua yeye kwa kuwa madhehebu hayo hayajawahi kutoa Rais, maaskofu kadhaa nchini wamepongeza karipio hilo.

Aidha, wamewataka viongozi wa dini nchini kutenganisha siasa na udini, lengo likiwa kuendelea kuwafanya Watanzania kuwa wamoja badala ya kuwagawa kwa misingi ya udini au ukabila.

Viongozi hao pia wameeleza kupinga hatua ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, kujihusisha na masuala ya siasa, wakisema inakiuka misingi ya dini huku wakimkana Askofu huyo kuwa msemaji wa Maaskofu.

Viongozi hao walitoa maoni yao jana, walipozungumza na gazeti hili kufuatia uamuzi wa NEC unaotokana na Lowassa kudaiwa amewaomba waumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri (KKKT) mjini Tabora, kumpigia kura kwa madai kuwa ni zamu kwa Walutheri kutoa Rais.

Rais wa Shirika la Kimataifa la Wapo Mission, Askofu Sylvester Gamanywa, aliitaka NEC kuendelea kuwakumbusha wadau juu ya Sheria ya Maadili ya Marais, Wabunge na Madiwani na pia kuhusu Sheria ya Uchaguzi, kwa kile alichosema uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti na ule uliofanyika miaka 10 au mitano nyuma.

“NEC iendelee kuwakumbusha wagombea na wafuasi wao mara kwa mara umuhimu wa kuzingatia sheria za uchaguzi.

“Ni lazima tukubali kuwa uchaguzi wa mwaka huu ni tofauti na uchaguzi mwingine wowote uliopita, kuna mabadiliko mengi na hata maadili ya sasa si kama yale ya zamani, kwani kumekuwepo na utandawazi na upevukaji mkubwa wa masuala ya kidemokrasia,” alisema Askofu Gamanywa, aliyekataa kuzungumzia suala la Lowassa akisema atatoa tamko baada ya kufanya utafiti wa kina kuhusu kile kilichotokea.

Pamoja na ushauri wa kuitaka NEC kuvikumbusha vyama na wagombea wake juu ya kufuata maadili ya uchaguzi, pia alipinga hatua ya Askofu Gwajima kuwa Msemaji wa Maaskofu, kama alivyodai alipozungumza na vyombo vya habari juzi jijini Dar es Salaam.

Kuhusu Gwajima kudai kuwa atawasemea maaskofu, Askofu Gamanywa alisema si sahihi kwa vile kila taasisi ya dini inaye msemaji wake kwa masuala yake, akitoa mfano wa Baraza la Maaskofu (TEC) kwa masuala yanayolihusu Kanisa Katoliki, Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa Makanisa mengine.

Mwenyekiti wa Mkesha Mkuu wa Kuliombea Taifa (Dua Maalumu), Askofu Godfrey Mallassy akizungumzia suala hilo alisema;” Siwezi sana kuzungumzia masuala ya siasa maana si kazi yangu.

Hata hivyo, Askofu huyo akizungumzia suala hilo alisema; “Mimi kama ninavyofahamika na watu wote kazi yangu ni kuliombea Taifa ili liwe katika amani na utulivu. “Suala la kuzungumzia siasa ni kupingana na kile ninachokifanya. Siwezi kutoa maoni yoyote kuhusu siasa na wanasiasa, bali nitaendelea kuomba amani kwa taifa ili makundi yote wakiwemo wanasiasa waweze kutimiza majukumu yao, wafanyakazi wafanye kazi na mambo kama hayo.”

Pamoja na hilo, Askofu Mallassy aliwaasa waandishi wa habari nchini kuisaidia nchi kwa kuandika mambo yanayochochea umoja na mshikamano wa kitaifa, badala ya kuligawa taifa, jambo alilosema ni la hatari.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Makanisa ya Kipentekoste nchini, Askofu David Batenzi, akizungumzia suala hilo pamoja na kuipongeza NEC, alisema kitendo cha Lowassa kuwaomba Walutheri kumchagua si sahihi, kwa vile kiutaratibu kama taifa, hakuna zamu za dini katika urais.

Askofu huyo ambaye pia alimkana Askofu Gwajima kuwa msemaji wao, alisema si sahihi kwa wanasiasa kutumia makanisa kama majukwaa ya kisiasa akisema kama hilo litaachwa likaendelea kutokea, litaligawa Taifa.

Alisema kwa kawaida makanisa yamekuwa yanatoa huduma za kiroho kwa watu, ambao wana itikadi tofauti za kisiasa na hivyo kuruhusu makanisa hayo kutumika kwa mambo ya kisiasa, kutaingiza nchi katika matatizo makubwa, na aliwataka wanasiasa kuacha kutumia makanisa kwa masuala ya kisiasa.

Askofu wa Kanisa la Kiadventista Wasabato Tanzania ambaye hakupenda jina lake kutajwa gazetini, akidai si msemaji wa Kanisa, alisema msimamo wa kanisa hilo ni kuwepo kwa utenganishi baina ya dini na siasa, na aliipongeza NEC kwa karipio lake.

“Sisi hatuamini katika makanisa kufanya kazi za kidini. Dini zifanye masuala ya kidini, na wanasiasa wafanye masuala ya kisiasa. Ukichanganya haya mambo kuna hatari ya kutokea kwa madhara makubwa sana.”

Kiongozi huyo alisema Kanisa hilo, litaendelea kuwapokea waumini wa vyama vyote vya siasa kwa lengo la kuabudu katika makanisa hayo, lakini kamwe haliwezi kuruhusu makanisa yake kutumiwa kama majukwaa ya kuwajenga au kuwabomoa wanasiasa.

Lowassa anadaiwa kutoa kauli hiyo Septemba 6, mwaka huu, katika Kanisa la KKKT la Tabora, ambapo akihudhuria ibada hiyo alinukuliwa na vyombo mbalimbali vya habari akidai kuwa kwa kuwa tangu nchi ipate Uhuru, hajawahi kutokea Rais kutoka madhehebu ya Kilutheri hivyo mwaka huu ni zamu ya Walutheri.

Hata hivyo, juzi NEC ilitoa tamko na kumuonya Lowassa ikisema kitendo hicho kinawagawa Watanzania na kuwapa mwelekeo wa kuchagua viongozi kwa misingi ya udini na ni ukiukwaji wa Kifungu cha 2.2 (i) cha Maadili ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani 2015, kinachosema; “Vyama vya Siasa au Wagombea hawaruhusiwi kuomba kupigiwa kura kwa misingi ya udini, ukabila, jinsia au rangi.”

Tamko hilo la NEC lilikuja saa chache baada ya CCM nayo kulaani kauli hiyo, inayodaiwa kutolewa Lowassa kanisani, kikitaka tume ya taifa ya uchaguzi kuchukua hatua.

CCM kupitia kwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye aliyezungumza jijini Dar es Salaam juzi, ilisema inalaani matumizi ya lugha zinazoligawa Taifa kwa misingi ya udini, ukanda, ukabila na ubaguzi wa aina yoyote ili kutafuta madaraka.

HABARI LEO

No comments: