DONALD TRUMP
Na Mwandishi Maalum
Wakati mdahalo wa pili wa wagombea wa chama cha Republican unasubiriwa kwa hamu usiku wa Jumatano tarehe 16 Septemba, ni vyema kuandika machache kuhusu mgombea Donald Trump ambaye anaendelea kuongoza kura za maoni katika kundi kubwa la wagombea wa chama cha Republican kwenye kinyang’anyiro cha kuwania kuingia Ikulu ya Marekani mwishoni mwa mwaka kesho. Katika kuchambua harakati za Bwana Trump za kuusaka uongozi wa juu wa taifa la Marekani pia tumejaribu kuanisha nini ambacho Watanzania wanaweza kujifunza wakati huu ambapo kampeni za kuwania Urais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania zimepamba moto.
Donald Trump na Edward Lowassa
Tungependa kuanza makala hii kwa kuwalinganisha Bwana Donald John Trump na Mheshimiwa Edward Ngoyai Lowassa ambao wote kwa sasa wanawania viti vya Urais wa Marekani na Tanzania. Ni dhahiri kwamba wapo baadhi ya watu ambao wamekuwa wakijiuliza, “Je, Edward Lowassa ndiye Donald Trump wa Tanzania?”
Bwana Trump ni mfanyabiashara na mwanasaisa wa Marekani ambaye ana sifa ya kuwa mmoja wa watu matajiri sana, kama alivyo Mh. Lowassa ambaye pia anasemekana kuwa Mtanzania mwenye utajiri mkubwa. Trump ni mmiliki mkubwa wa ardhi na majengo wakati Mh. Lowasaa anadai kwamba msingi mkubwa wa utajiri wake unatokana na kumiliki ardhi na mifugo mingi huko sehemu za Monduli.
Mara kadhaa Bwana Trump amejaribu kuwania kiti cha urais wa Marekani, kama ilivyo kwa Mh. Lowassa. Wote wamekaririwa wakisema kwamba wanataka kuwania uongozi wa ngazi ya juu katika nchi zao ili kusaidia kuleta neema na maisha bora kwa wanainchi wa nchi zao. Wanadai lengo lao ni kupata fursa ya kutumia vipaji vyao ambavyo vimewapa utajiri ili kuinua hali ya maisha na kutajirisha jamii zao!
Katika kampeni za uchaguzi zinazoendelea nchini Marekani Bwana Trump anawania uteuzi wa chama chenye viti vingi katika bunge la Marekani cha Republican. Lowassa alianza “safari yake ya matumaini” kwa kuwania uteuzi wa chama cha CCM ambacho pia kina viti vingi kwenye bunge la Tanzania. Bahati mbaya alitupwa kapuni kwenye mchujo wa chama hicho huko Dodoma.
Ingawa Bwana Trump anaongoza katika kura za maoni kwenye chama chake cha Republican lakini anaonekana hapendwi sana na viongozi wakuu wa chama chake ambao wanapendelea wagombea wengine. Mh. Lowassa vile vile alianza kuwania uteuzi wa kupeperusha bendera ya CCM ambako mbali na kuungwa mkono na wanachama wengi wa kawaida waliomdhani kwa wingi, lakini alichujwa na viongozi wakuu wa chama hicho ambao inasemekana walikuwa na mapenzi na wagombea wengine.
Awali, Bwana Trump alitishia kujitoa kwenye chama cha Republican na kusimama kama mgombea binafsi endapo atafanyiw amizengwe. Hali hiyo iliwapa kiwewe na wasiwasi viongozi wa chama cha Republican. Hivi karibuni Bwana Trump alitangaza kwamba atamuunga mkono mgombea ambaye atateuliwa na chama cha Republica, huku akisisitiza kuwa bila shaka mgombea huyo atakuwa ni yeye. Katiba ya Tanzania hairuhusu mgombea binafsi wa kiti cha Urais, kwa hiyo baada ya kuenguliwa kutoka kwenye kinyang’anyiro cha kuiwakilisha chama tawala cha CCM kwenye uchaguzi wa Rais, Mh. Lowassa alilazimika kujitoa CCM na kuingia kwenye chama cha upinzani CHADEMA na kupitia huko ameteuliwa kupeperusha bendera ya UKAWA ambao ni muungano wa vyama vine vikuu vya upinzani.
Wote wawili, Bwana Trump na Mh. Lowassa wanaweza kuelezewa kama watu wenye misimamo mikali na maamuzi magumu. Katika safari za kutimiza ndoto zao kibiashara na kisiasa, wamekumbana na misukosuko mingi migumu lakini mara nyingi wameibuka na kusonga mbele. Wote si wanasiasa mahiri au wazungumzaji wazuri sana kwenye majukwaa, lakini wanasifika kwa utendaji, ufuatiliaji na ufanikishaji wa dhamira zao. Wote ni watu wenye roho ngumu na jeuri ya kutokata tamaa kwa urahisi. Na bila shaka wote wawili wanajitambulisha kirahisi kwa muonekano wa nywele zao.
Nafasi ya Donald Trump katika Siasa za Marekani
Baada ya kutoa utangulizi huo, hebu tujaribu kuona kwa undani historia, nafasi na changamoto za Bwana Trump katika siasa za Marekani na nini Watanzania wanaweza kujifunza kutokana na hali hiyo.
Bwana Trump alizaliwa tarehe 14 Juni 1946 akiwa mmoja kati ya watoto watano wa Baba Fred Trump na Mama Mary Anne. Wazazi wote wawili wa Bwana Trump wana asili ya kihamiaji kutoka nje ya Marekani, mama akiwa mzaliwa wa Scotland na upande wa baba wakiwa wahamiaji kutoka Ujerumani.
Kielimu, Bwana Trump ana shahada ya kwanza ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Pennsylavania. Alianza kujiingiza katika mambo ya biashara akiwa na umri mdogo akiongozwa na baba yake mzazi. Baada ya kuhitimu chuo kikuu mwaka 1968, aliingia rasmi kwenye kampuni ya baba yake ya ujenzi, umiliki na uuzaji wa majumba. Donald alipanda haraka haraka na kufikia mwaka 1971, akapewa uongozi wa juu wa kampuni hiyo. Baadaye alipanuwa wigo wa biashara na kujiingiza katika masuala ya utangazji na burudani. Pamoja na misukosuko kadhaa ya kibiashara aliyoipitia, hivi sasa Bwana Trump anakadiriwa kuwa na utajiri wa kiasi cha dola 4.1 bilioni, akipata mshahara wa dola 250 milioni kwa mwaka.
Kisiasa, Donald Trump amewahi kuwa mwanachama wa vyama vya Republican, Reform Party, Democratic na Independent. Ingawa huko nyuma alihama chama cha Republican mara tatu, kwa sasa anawania uteuzi wa chama cha Republican ili aweze kugombea kiti cha Urais wa Marekani.
Ingawa uchaguzi wa Urais wa Marekani utafanyika mwezi Novemba mwakani, tayari kuna zaidi ya wagombea 15 ambao wanawania nafasi ya kupeperusha bendera ya chama cha Repubican kwenye uchaguzi ujao. Kwa hivi sasa kura za maoni miongoni mwa wafuasi wa chama hicho zinamwonesha Bwana Trump akiongoza kundi la wagombea wote kwa alama nyingi. Anafuatiwa kwa karibu na mombea pekee Mmarekani mwenye asili ya Kiafrika, Daktari Bingwa wa mishipa ya fahamu Dr. Ben Carson.
Hata hivyo wachumbuzi wa masuala ya siasa za Marekani wanasema kampeni ya Bwana Trump inatoa changamoto kubwa kwa uongozi wa chama cha Republican ambao unaonekana kutompenda kuwa mgombea wake. Wanamuona Trump kama “mnoko” na “mchafuzi” wa nafasi ya chama hicho kushinda dhidi ya wapinzani wao wa Democtartic. Uongozi wa Republican ungependelea kusimamisha wagombea wengine wasio na utata mkubwa kama Jeb Bush, Marco Rubio, John Kasich au Scott Walker.
Tayari Bwana Trump amezusha mitafaruku mikubwa na misuguano kutokana na matamshi yake hasi dhidi ya wahamiaji wenye asili ya Kihispania (hususani kutoka Mexico) ambao alinukuliwa akiwaita wahalifu, majambazi, wauaji na wabakaji. Pia amekwaruzana na baadhi ya wanasiasa waandamizi wa chama hicho akiwemo Seneta John McCain na Graham Lindsey. Katika mdahalo wa kwanza ukiwapambanisha wagombea kumi kwenye ulingo mmoja, Bwana Trump alisakamwa vikali na wagombea wengine huku akitupiwa maswali magumu na muongozaji wa mdahalo huo, ambayo yasemekana yalilenga kumkata makali. Trump aliweza kujibu mapigo na kumtupia madongo mazito muongozaji wa mdahalo huo Bi. Megyn Kelly wa kituo cha Televisheni cha Fox ambacho kina uhusiano wa karibu na viongozi wakuu wa chama cha Republican. Hivi karibuni pia amekwaruza na mgombea pekee wa kike Carly Fiorina, ambaye aliwahi kuwa mkuu wa kampuni ya kubwa kompyuta ya Hewlett-Packard.
Tatizo kubwa la chama cha Republican ni kwamba ingawa hawampendi Bwana Trump, ni lazima wawe makini jinsi ya kumkabili, kwa vile mpaka sasa anaonyesha kupendwa na wanachama na watu wengi wa kawaida ambao wamechoshwa na uongo wa “wanasiasa wa ndani” wa jiji la Washington. Kwa watu wa kawaida, Trump anaonekana kama mgombea tofauti anayesema kitu kutoka moyoni mwake, ambaye anasema ukweli hata kama unauma. Wanamuona Trump kama mtu ambaye ana pesa zake lakini anataka kusaidia watu wengine kwa dhati na hasukumwi kuwania kiti cha Urais kutokana na “njaa” zake au maslahi binafsi.
Trump amekuwa akitishia kwamba endapo viongozi wa chama cha Republican watamchezea mchezo wa rafu, angeweza kujitoa chama hicho na kusimama kama mgombea binafsi, hatua ambayo itakiweka chama cha Republican kwenye hali mbaya ya ushindani na mahasimu wao wa chama cha Democtratic. Ingawa amelegeza msimam huo hivikaribuni baada ya kuona anaendelea kuongoza, lakini watu wa karibu wanaomfahamu Trump wanasema si ajabu akageuza kibao tena endapo ataona ameonewa au amepigwa “goli la mkono” kwa msemo mpya. Akisimama kama mgombea binafsi, Trump anaweza kuzigawa kura za wafuasi wa Republican na wale wasiokuwa na mapenzi na chama chochote (independents) na hivyo kupelekea wapinzani wao wa chama cha Democratic kupata ushindi kirahisi.
Bila shaka kwa sasa Bwana Trump ameshikilia kura ya turufu na ndiyo maana viongozi waandamizi wa chama chake cha Republican wamekuwa wakimbembeleza na kumsihi asichukuwe uamuzi mgumu wa kutoka chama hicho. Hata baadhi ya wagombea wenzake wamepunguza mashambulizi dhidi yake wakihofia mtafaruku zaidi. Endapo Trump ataendelea kuongoza na hivyo kujihisi anastahili kuteuliwa kuwa mgombea halali wa chama hicho lakini wagombea wengine wakakataa kumuunga mkono, kama ambavyo baadhi ya wagombea wakiongozwa na Gavana wa zamani George Pataki tayari wamejitokeza, hali ya baadaye ya chama hicho inatia mashaka.
Haiyumkiniki wachambuzi wengi wanasema Bwana Trump anayo nafasi ndogo ya kushinda uteuzi wa chama chake cha Republican, achilia mbali uwezo wa kushinda kiti cha Urais katika uchaguzi mkuu mwakani. Hata hivyo wanasema Trump ni mtu ambaye hawezi kubezwa kirahisi. Wakifanya makosa, Bwana Trump anaweza kusababisha chama cha Republican kipoteze nafasi ya kushinda kiti cha wa Urais na hata kuwanyima uongozi wa bunge la Marekani kwa kukosa idadi kubwa ya wabunge kutokana na baadhi ya wapiga kura kuamua kupiga kura za hasira dhidi ya chama hicho na viongozi waalioko madarakani.
Nini Watanzania wanaweza kujifunza
Tumalizie makala hii kwa kuangalia nini wapiga kura wa Tanzania wanaweza kujifunza kutokana na harakati za ugombea wa Bwana Donald Trump wa kiti cha Urais wa Marekani.
Kama tulivyoonyesha mwanzoni mwa makala hii, vipo vielelezo vingi vinavyomfananisha Bwana Donald Trump na Edward Lowassa katika mbio zinazoendelea za kuwania kiti cha Urais nchini Marekani na Tanzania. Baadhi ya mambo ambayo tunaweza kujifunza ni pamoja na haya yafuatayo:
Kwanza, katika medani za siasa, hakuna rafiki au adui wa kudumu. Malengo ya mwanasiasa siku zote ni kupata ushindi katika uongozi na kufikia malengo hayo kunahitaji mbinu na mikakati tofauti. Si vyema kutumia mbinu zile zile au kung’ang’aniza matakwa ya viongozi wachache ambao wakati mwingine yanakinzana na mtizamo au matarajio ya wafuasi au wanainchi wa kawaida walio wengi.
Pili, ingawa mazingira ya hizi nchi mbili ni tofauti, lakini ni vyema chama tawala cha CCM chenye viti vingi bungeni kwa sasa kikawa macho ili kisipoteze uwingi huo kwa kuendeleza kampeni ya kuandama, kumbeza na kujaribu kumchafua Lowassa ambaye alikataliwa CCM na kulazimika kwenda upande wa upinzani ambako amesimamishwa kama mgombea wao. Kura za hasira na huruma kwa wafuasi wa Lowassa na watu wa kawaida tu zinaweza kuwatoa CCM kileleni katika Jumba Kuu huko Dodoma.
Tatu, ipo haja ya kubadili katiba ya nchi ili pamoja na maboresho mengine iweze kuruhusu mgombea binafsi wa kiti cha urais na pia miundo ya serikali za mseto au muungano wa vyama. Endapo kungelikuwa na nafasi hiyo Edward Lowassa huenda asingelazimika kutoka CCM na kujiunga na chama kingine cha upinzani, labda angesimama kama mgombea binafsi, hali ambayo ingeiteteresha CCM kidogo, lakini isingewapa wapinzani matunda yote ya ufuasi wake.
Mwisho, ni muhimu kuendesha siasa za kistaarabu. Hata kama mnatofautiana kimtizamo, Watanzania bado ni watu wa taifa moja. Mpinzani wako kisiasa si adui, leo yuko kule kesho mnaweza kuwa naye huku. Donald Trump amekuwa akifadhili wagombea wa vyama vyote vya Republican, Tea Party na Democratic, hata kama yeye si mgombea au mwanachama wa vyama hivyo kwa wakati huo.
Wanasiasa wa Marekani wanapingana hadharani lakini wanaendelea kuzungumza kirafiki na kibinafsi kwa kuheshimiana. Hata baada ya kushindwa katika sanduku la kura, aliyeshindwa anampigia simu aliyeshinda kumpa pongezi hata kama amemng’oa kwenye kiti alichokuwa amekalia kwa muda mrefu!
Vyombo vya dola vyenye jukumu la kulinda amani na usalama havipashwi kujiingiza katika minyukano ya kisiasa na kamwe havitakiwi kuegemea upande mmoja dhidi ya mwingine. Hiyo ndiyo siri ya ukweli kwamba mara nyingi chaguzi za Marekani zinaendeshwa kwa hali ya utulivu, haki, amani na usalama.
Tujifunze yaliyo mazuri kutoka katika mfumo wa wenzetu (tukiacha yale mabaya) ili na sisi tuweze kusonga mbele na kufanikisha uchaguzi ujao kwa haki, amani na usalama.
Mungu ibariki Tanzania.
8 comments:
Wapiga kura wa watanzania tunaweza kujifunza kutoka kwa mgombea wa uraisi wa republican kutoka marekani ni kwamba bwana Donald Trump ni tajiri wa kupindukia lakini chanzo cha utajiri wake kinajulikana hauna shaka tofauti na bwana lowasa mpaka sasa mali zake ameshindwa kuzielezea kazipata vipi isipokuwa bwana Donald Trump ni mbaguzi anaeamini watu weupe pekee ndio wenye haki ya kubaki hapa marekani wengine wote ikiwezekana waondoke hiyo yakusema kauli yake iliwalenga wahamiaji haramu ni excuse tu kwani alisha mkebehi Raisi Obama kuwa si mmarekani . Hata hao wananchi wanaomuunga mkono ni tabaka la wale watu weupe wenye sera za chuki zidi ya matabaka mengine. Na kauli za kebehi na dharau zidi za wahamiaji wenye asili za mexico pamoja na kumuambiwa Obama kuwa amefoji cheti chake cha kuzaliwa na hakuwa amezaliwa marekani ni miongoni mwa kauli zake zilzo mpandisha chati sana kutoka kwa wafuasi wake. Donald trump alianzia kama mfadhili kwa republican party na mwishoe akaamua kujiingiza katika siasa za ushindani hata hivyo watu wengi hawamchukilii trump serious kutokana na kauli zake za hovyo. Hata chama chake Republican party wanajua anachokifanya trump hivi sasa ni hasara zaidi kwa chama kuliko faida kwani kura za watu weupe pekee haziwezi zikawapeleka ikulu. Sasa sifikirii sisi watanzania tunaweza kujifunza kutoka kwa mtu mbaguzi na anaepita akitukana watu hovyo. Aliwahi kumtukana mtangazaji wa kike aliekuwa anasimamia debate kwa kusema kuwa mwanamama huyo alikuwa kamkamia na wakati akimuuliza maswali ilidhirisha dhahiri yule mama damu zilikuwa zikimvuja sasa maneno gani ya raisi mtarajiwa kwa jamii ?
Trump kumlinganisha na lowasa ni vichekesho vya dunia Trump ni mega billionaire lakini utajiri wake unaeleweka ulipoanzia yaani hauna shaka. Lowasa mpaka sasa kashindwa kuelezea chanzo cha mali zake.
hivi kweli wewe ni mwandishi au unatania, huo mfano wako hauko hata karibu kwa chembe. wewe unasema lowasa ni mfanyabiashara!!! anafanya biashara gani ambayo wanaijua!!!???? acha kupotosha ukweli wa mambo, lowasa hana biashara yoyote halali Tanzania inayojulikana. mali zake amezipata kwa njia ambazo ni za kifisdi, sasa tutajie mali au biashara halali anayofanya na analipa kodi kiasi gani, wewe unafananisha usingizi na kuwa macho, trump sio fisadi wala mwanasiasa, lowasa ni mwanasiasa na fisadi na muongo.
Namsifu muandishi wa article hii hasa kwa kusimamia topic alotaka kuiandika. Staunch critics always huwa wapo na zaidi nadhani ni kwa mara ya kwanza aloandika kaamua kuweka all necessary subtances kunsaidia msomaji kuelewa. Tofauti kubwa nimeiona hapo juu ni kuwa aloandika habari hii yupo huru na hahitaji kuvutia msomaji kwa kuandika heading tofauti na body contents tofauti. It is about time waandishi ea bongo waanze kuandika kitaalamu. Juzi nilisoma heading kuwa Kikwete amemta j a mmiliki wa Richmond, nikaenda kwenye body contents nikakuta ni mashairi tu ya taarabu aloyasema huko kigoma. Waandishi Bongo acheni uvivu, tumieni muda huu kuonyesha umahiri wenu wa kuripoti na kuchambua hoja hasa za wagombea. Asilimia kubwa ni pro CCM hatimae wanadumaa na kusahau majukumu yao ya kuandika.
Wachangiaji wa awali nao ni walewale waloamka kwa kunywa chai ya maji ya bendera ya kijani. Muandishi ameandika na kusema souce ya utajiri wa lowassa na muungwana wa jembe na nyundo anahoji lowassa kapata wapi mali zake!
Ohhh poor Tanzanian. Everyday and everything is about hating propaganda.
When are we going to enjoy free speach and exchange of views and ideas?
Wananiboa wakereketwa.
Rubbish!!! Trump and Lowasa have virtually nothing in common. Lowasa has been in public service all his life, never as a businessman like Trump. No one in public service, anywhere in the world, can possibly become as rich as a businessman without engaging in abuse of office and other corrupt practices.
Lowasa ana utajiro gani wa kutisha. Hamumtizami Mtoto juzi RW1 huonutajiri unavyokuja juu kwa kipindi cha miaka mitano zaidi atakuwa ameshampita hata huyu Lowassa. Na Tanzania wako matajiri wengi na wasio na halali ya utajiri. Kwani Rugemalila aliporuhusu kugawa fedha alizitoa wapi ni tajiri au ni Fisadi mbona hajaulizwa wamekaa kimya. Trump ameridhi utajiri huo na hauna maswali..
Mchangiaji namba moja hapo juu ama hakusoma makala hii kwa kutulia na kuielewa au alichangia kutokana tu na jazba pamoja na mihemko ya kisiasa inayoendelea sasa hivi nchini Bongo. Kuhusu Lowassa kuwa tajiri na chanzo cha utajairi wake, mwandishi alitumia neno zuri la "inasemekana" na wala hakuhalalisha utajiri huo. Baada ya kuondoka Mwalimu Nyerere, viongozi wengi nchini Tanzania ni wafanya biashara, wanayo makampuni ya wazi na mengi ambayo ni bubu, akiwemo Rais Mstaafu Ben Mkapa ambaye alifungua kampuni ya biashara kwa kutumia anuani ya Ikulu na akaendesha biashara akiwa Rais. Pia inaonekena mchangiaji haujui vizuri siasa za Marekani hasa kwa wakati huu ambapo pamoja na kutupiwa madongo mengi (negatives)lakini Bwana Trump bado anaongoza kura za maoni siyo tu miongoni mwa wanachama wa chama cha Republican lakini hata wale wasio wakereketwa wa vyama(independents). Zipo sababu ambazo mwandishi alijaribu kueleza na ndiyo maana akamlinganisha na Edward Lowassa ambaye pamoja na "negatives" nyingi ambazo anasukumiwa lakini bado anaelekea kuwa na mvuto au ufuasi wa watu wengi miongoni mwa wapiga kura wa Tanzania. Watu wanafika mahali wanachoka na wanakuwa tayari kwa mabadiliko! Kitu ambacho mimi nimejifunza kutoka kwenye makala hiyo ni umuhimu wa kufanya siasa na kampeni za kistaarabu bila ya kuchafuana na pia suala la vyombo vya habari kuwa ciritical but balanced na vyombo vya dola kutoegemea upande mmoja. Tukiwa na moyo wa kujifunza kutoka kwa wengine tutafanikisha mambo yetu. La sivyo mambo yatabakia kuwa yale yale ya Kibongo milele na milele!
Siasa gani ya marekani unayoifahamu wewe kuhusu Dornald trump? Unaelewa kwamba bwana Donald Trump na republican wapo kwenye mchakato wa kumtafuta mgombea ndani ya chama chao kwa hivyo takwimu zozote za kura za maoni zinazomuenyesha kuwa Trump yupo juu zinatokana na maoni ya wa republicans hizo habari za kusema sijui independents ni zakwako. Kitu kimoja ningekuomba acha kabisa. Acha kabisa mawazo au fikra za kumfafanisha Donarld Trump na Lowasa kwani ni sawa na mtu aliepata ajali mbaya akawa anaropokwa mambo asiyoyafahamu . Trump halishwi maneno kama lowasa bali anaongea maneno ya trump kila mtu anajua. Hata wewe mwenyewe hapo unajaribu kuzungumza pumba ili kumsaidia lowasa angalau aonekane ni mtu anefaa. kama lowasa angelikuwa mtu msafi basi wewe usingepata taabu na kuhangaika jinsi ya kumsafisha Kama ambavyo unafanya sasa.
Ukweli ni kwamba Wamarekani wamechoka na "status quo" na siasa za ya "business as usual". Ndiyo maana hata Mama Hilary Clinton anapata shida kwenye kampeni yake hivi sasa. Kuna watu wengi wanaotaka mabadiliko ya kiutendaji. Bila shaka hali hiyo ndiyo inajitokeza nchini Tanzania sasa hivi. Watu wanaotumia jina la Nyerere huko Tanzania wanasahahu kwamba he was more genius than them. Hakutaka kuzuia wimbi la mabadiliko ya mfumo wa vyama vingi wakati ule wa miaka ya 80.Bila shaka angekuwapo leo angeangalia upepo unaavyovuma na kusoma alama za nyakati. Kama Watanzania wengi wanataka mfumo wa serikali tatu basi wapeni, kwa nini hilo linazuiwa? Let us not be dogmatic. Tuache tabia ya kung'ang'ania siasa za "business as usual" kwa kutumia visingizio vya kulinda amani na utulivu wa kitaifa. Hakuna amani na utulivu kama watu wana njaa, hawako huru na kama watu wanajiona kwamba hawashiriki kikamilifu katika kufaidika na utajiri au rasilimali za Taifa. Kwa sasa wanasiasa na viongozi wa Tanzania wanapaswa kuembrace the wave of change or the wave will change them and sweep them away!
Post a Comment