
Mkuu wa Mkoa wa Morogoro,Dkt.Rajabu Rutengwe akisalimiana na wafanyakazi wa kampuni ya M-POWER mara baada ya kuwasili kwenye ufunguzi wa ofisi wa kampuni hiyo katika kata ya kihonda magorofani mkoani hapa.

Mkuu wa Mkoa wa Morogoro Dkt.Rajabu Rutengwe akikata utepe wa kufungua ofisi ya kampuni ya M-POWER inayohusika na kusambaza umeme wa jua hapa nchini,kulia ni Mkurugenzi wa Usambazaji wa kampuni hiyo Raphael Robert.

Mkurugenzi wa Usambazaji wa kampuni ya M-POWER Tanzania,Raphael Robert akitoa maelezo ya utendaji wa kampuni kwa Mkuu wa mkoa wa Morogoro,Dkt.Rajabu Rutengwe.(Picha zote na Peter Kimath)
Na,Peter Kimath, Morogoro.
MKUU wa mkoa wa Morogoro Dk Rajabu Rutengwe ameitaka kampuni ya M-Power Tanzania inayoshughulika na utoaji wa umeme mbadala kuhakikisha inatoa huduma ya nishati hiyo kwa gharama nafuu kulingana na kipato cha wananchi wanaowahudumia
Dk Rutengwe alisema hayo mjini Morogoro wakati akizungumza na wananchi wa kata za Kihonda na Kihonda Magorofani walionufaika na umeme mbadala unaotumia nishati ya jua kutoka kwa kampuni ya M-Power Tanzania.
Alisema kutokana na upana wa mahitaji ya wananchi hususani walioko vijijini ni vyema kampuni hiyo ikafanya gharama zake kuwa nafuu ili kuwafanya wananchi kumudu kununua na kuachana na ununuzi wa mafuta ya taa na mishumaa ambyo imekuwa ikisababisha hasara ikiwamo ya kuungua kwa nyumba.
Alisema ni azma ya serikali kushirikiana na wadau wa maendeleo kama ilivyo kwa M-Power Tanzania katika kuwaondoa wananchi na na wimbi la utegemezi wa nishati ya umeme moja,na kwamba ni vyema kampuni hiyo ikatoa huduma hata kwa taasisi za serikali kama Zahanati na vituo vya afya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa usambazaji wa M-Power kwa nchi ya Tanzania na Rwanda,Raphael Robert alisema kampuni yao inatarajia kutoa huduma za bure kwa taasisi za serikali kama Vituo vya Afya,Zahanati pamoja na vituo vya Polisi ili kuweza kutoa huduma kwa wananchi wake nyakati zote.
Robert alisema tangu kuanzishwa kwa kampuni hiyo mwaka 2013 wameweza kufika katika mikoa 13 na kwamba mpaka kufikia 2017 watakuwa wamefikia kutoa huduma kwa mikoa yote ya Tanzania.
Nae Meneja wa Operesheni wa M-Power mkoa wa Morogoro Emmanuel Ngandu alisema kabla ya kutoa huduma kwa jamii huwa wanafanya utafiti kujua idadi gani ya watu wanahitaji huduma hiyo katika eneo husika na hutoa huduma kulingana na uwezo wa mteja kwani huduma yao ipo katika viwango tofuati.
No comments:
Post a Comment