ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, September 26, 2015

Utafiti wa Tadip wampaisha Lowassa


Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Tanzania Development Initiatives Program (Tadip), iliyofanya utafiti wa “Kuelekea Uchaguzi Mkuu Watanzania wanasemaje” imeonyesha mgombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, anaongoza kwa asilimia 54.4 na mgombea wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk. John Magufuli akifuatia kwa asilimia 40.

Utafiti huo umekuja siku chache tu baada ya awali uliotolewa na Taasisi ya Twaweza kuonyesha Dk. Magufuli anaongoza kwa asilimia 65 na Lowassa akipata asilimia 25.

Katika utafiti uliotolewa juzi na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), ulionyesha Lowassa ana asilimia 76 ya watu wanaomuunga mkono huku
Aidha, utafiti mwingine uliosambazwa kwenye vyombo vya habari juzi ulionyesha Magufuli anaongoza kwa asilimia 62 na Lowassa kwa asilimia 31.


Kwa upande wa wagombea urais wa vyama vingine vya siasa Tadip ilisema mgombea wa ACT-Wazalendo, Anna Mghwira amepata asilimia mbili, akifuatiwa na mgombea wa Chaumma, Hashim Rungwe, alipata asilimia 0.4, huku mgombea wa ADC, Chief Yemba akipata asilimia 0.1 na asilimia tatu ya wananchi walisema hawafahamu wanampa nani kura.

Mkurugenzi wa Tadip, George Shumbusho, akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuhusu utafiti huo, alisema ulifanyika kuanzia Septemba 4 -23, mwaka huu.

“Utafiti huu uliwalenga wananchi moja kwa moja ambao waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa kutumia mfumo wa Biometric Voter Registation (BVR). Ulifanyika kwa wiki tatu za mwezi huu na mikoa tuliyolenga ni ile ambayo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) ilithibitisha kuwa ina idadi kubwa ya watu,” alisema Shumbusho.

Aidha, utafiti huo ambao ulilenga mikoa 12, ulionyesha kuwa, Lowassa anaungwa mkono na wanaume ambao ni asilimia 57 ya waliotoa maoni huku Dk. Magufuli na Anna Mughwira wakiungwa na wanawake kwa asilimia 43 ya waliopiga kura.

Kuhusu idadi ya walioshiriki katika utafiti huo, alisema walitumia njia za madodoso kuwapa wananchi 2,500 ambao kati yao 2,040 ndio waliorudisha madodoso.

“Tulitumia njia ya kuwapa watu wetu madodoso ambayo waliyafikisha kwa wananchi kati ya nyumba 20 walitoa kwa mtu mmoja na walioweza kujibu madodoso ni 2,040. Tulipokea pia ripoti ya mdodoso na mdodoswa,” alisema. Alitaja mikoa waliyojikita katika utafiti huo kuwa ni Dar es Salaam, Mbeya, Mwanza, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Shinyanga, Geita, Dodoma, Morogoro, Kagera na Kigoma.

Alisema katika ya mikoa hiyo mikoa ya Kagera na Kigoma ilishindwa kupata maoni yao kutokana na kuwahi ukomo wa kuwasilisha takwimu hizo kwa wananchi.

Alitaja takwimu za maoni katika kila mkoa ni kuwa, Mkoa wa Dar es Salaam waliohojiwa (386), Mbeya (154), Mwanza (222), Tanga (118), Arusha (182), Kilimanjaro (208), Shinyanga (188)Geita (206), Dodoma (200) na Morogoro (176). Kuhusu walengwa waliokusudiwa katika utafiti huo, asilimia 51 walikuwa na umri kati ya 18 hadi 28, asilimia 30 umri kati ya 29 na 39, asilimia 10 umri kati ya 40 hadi 49, asilimia 7 umri kati ya 60 na kuendelea.
Waliokuwa na elimu ya sekondari ni asilimia 38 na elimu ya shule ya msingi asilimia 37.

MIKOA ANAYONG’ARA LOWASSA
Kwa mujibu utafiti huo Lowassa anakubalika katika mikoa ya Kilimanjaro, Tanga, Arusha na Dar es Salaam huku Dk. Magufuli akiungwa mkono katika mikoa ya Dodoma na Morogoro.
Aidha, makundi ya watu wanaomuunga Lowassa mkono kwa mujibu wa uatafiti huo ni watu walio chini ya umri wa miaka 47 huku Dk. Magufuli akiungwa mkono kati ya umri juu ya miaka 47.

MAGUFULI: Msibabaishwe na tafiti
MGOMBEA urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), John Magufuli, amewataka wananchi kutobabaishwa na matokeo ya tafiti zinazotolewa na kuonyesha atashinda urais kwa asilimia 65 na kuwataka wasubiri Oktoba 25.
Amesema anatarajia wananchi wamchague kwa kishindo ili apate ushindi mnono wa asilimia 95.

Akizungumza katika kijiji cha Nyarugusu jimbo la Busanda mkoani Geita, Dk. Magaufuli alisema kuna watu wanaweza kuwalaghai wananchi wasiende kupiga kura wakidanganya kwamba ameshashinda.

“Msidanganywe kwamba nimeshashinda, Oktoba 25 amkeni mapema mkanipigie kura, akija mtu akiwaambia kwamba msiende kwasababu nimeshashinda huyo muongo,” alisema Dk. Magufuli.

Alisema anataka wapinzani wake wasiambulie hata kura chache kwenye uchaguzi huo ili yeye aibuke na ushindi wa kimbunga.
Dk. Magufuli alisema anatambua kuwapo kwa mafisadi ndani ya CCM na serikalini hivyo akiingia madarakani kazi yake kubwa itakuwa ni kuwaondoa ili kukomesha mianya ya rushwa.

Aidha, alieleza kushangazwa kwake na kiongozi aliyewahi kushika madaraka makubwa serikalini kama Frederick Sumaye aliyehamia upinzani na kuanza kuirushia lawama na kashfa serikali.

Alisema Sumaye amekaa madarakani kwa miaka kumi mfululizo lakini bila haya anainanga serikali kwamba haijafanya lolote wakati yeye ndiye anastahili lawama hizo.

Alisema serikali yake inajua shida za wachimbaji wadogo wa mji wa Nyarugusu Geita na kwamba akiingia madarakani atawajali kwa kuwapa maeneo ya kuchimba dhahabu.

Alisema wakimchagua kuwa rais atahakikisha mji huo unapata huduma ya maji, barabara ya lami na huduma za afya.

Aidha, akiwaomba kura wananchi wa Mbogwe, mkoani Geita, alisema vyama vilivyoungana na kuweka mgombea mmoja wa urais kupitia Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) vilifanya hivyo vikimhofia, baada ya kubaini havitaweza kupambana naye.

Alisema mara baada ya kuteuliwa kugombea kuwania nafasi hiyo, wapinzani walianza kuhaha kuweka mipango ya kupambana naye wakijua kuwa wanapambana na jabali.

“Mbona siku zote hawakuungana hadi waliposikia nimeteuliwa… Waliniogopa sana sasa nawaambia Ukawa wakawie wasiione Ikulu maana Ikulu ni ya Magufuli na CCM yake, Magufuli ndiye mwenye uwezo wa kuwaletea mabadiliko ya kweli na yaliyo bora,” alisema.
Dk. Magufuli alisema hatakuwa na serikali yenye porojo na visingizio vya hapa na pale na kwamba mawaziri watakaoteuliwa kwenye serikali yake wakae mguu sawa.

Aidha, alisema hata ndani ya CCM kuna mafisadi ingawa wengine wameamua kukimbia baada ya kuona ameteuliwa kuwania urais kwa tiketi ya chama hicho.

CHANZO: NIPASHE

No comments: