Advertisements

Tuesday, September 1, 2015

MPENZI WAKO AKIKULALAMIKIA UNA WIVU WA KIJINGA KWAKE... UJUE ANAKUSALITI-2

NAAM! Ni Jumanne tena. Naamini wasomaji wangu mnaendelea kuhesabu siku kuifikia Oktoba 25, mwaka huu ambapo itakuwa siku ya kupiga kura kumchagua rais wa awamu ya tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini pia kuna kuwachagua madiwani na wabunge.

Kwa upande wangu nashukuru sana kwamba pamoja na harakati za uchaguzi mkuu, bado napata meseji nyingi sana kutoka kwenu. Hii inaashiria kwamba, mnanisoma vizuri.

Wiki iliyopita mada yangu ilisema; ukiona hana wivu na wewe...hakufuatilii...meseji mpaka uanze wewe...HUYO ANA MALENGO YAKE. Nilichambua vizuri sana na nilipata meseji nyingi za kunipongeza.
Wiki hii nina mada mpya. Inasema; mpenzi wako akikulalamikia una wivu wa kijinga kwake...UJUE ANAKUSALITI!
TWENDE PAMOJA SASA...


Inajulikana kwamba, wivu ni chachandu ya upendo kwa wawili walioamua kuwa pamoja kimapenzi. Hapa sijalishi wanandoa, wachumba wala wapenzi. Nazungumzia kwa ujumla. Zipo semi mbalimbali kwamba, mapenzi pasipo kuwa na wivu hayapo au hayadumu.

Wivu humsaidia mmoja wa wapendanao kujisikia anapendwa, anakubalika, anathaminiwa na anajaliwa. Hapo ndipo mapenzi hunoga na kukuta mtu anajitoa kwa mwenzake.

LAZIMA KUONESHA
Na ili wivu wa upendo ufanye kazi lazima kila upande uoneshe kwa sauti au kwa vitendo. Mwenzako hajakupigia simu wakati si kawaida yake lazima umuulize; mbona leo hujanipigia. Ulikuwa wapi mpaka ukashindwa kunipigia?’
Au si kawaida ya mpenzi wako kutokuwa hewani kwenye simu. Lazima uoneshe unajisikia wivu kwa kumuuliza; ‘ulizima simu ulikuwa wapi? Na kwa nini uzime simu?’

Mfano mwingine unamfahamu mwenzako kipato chake, sasa ghafla unamwona kanunua simu ya bei mbaya, lazima umuulize; ‘umenunua simu hii fedha umepata wapi?’ Mwingine anamfuata mpenzi wake kwake anakuta hayupo. Kwenye simu hapatikani. Mara anatokea lazima uulize; ‘ulikwenda wapi? Kwa nini hukuniambia kwamba utakwenda kwa shangazi? Mimi nitaaminije kwamba ulikwenda huko wakati ulizima simu?’

CHACHANDU YENYEWE

Mambo kama hayo ndiyo hunogesha mahaba kwa wawili wapendanao. Wivu kama huo humfanya mwenza wako kuhisi kweli yupo na mtu anayempenda na pia humfanya yeye kuwa makini na ratiba zake.

LAKINI SI HIVYO TU
Pamoja na hayo niliyoyasema, lakini wivu pia hautakiwi kupita eneo la usalama na amani. Naaminisha kwamba, wengine wakihisi jambo baya kufanywa na wenza wao basi ugomvi mwanzo mwisho, pengine hata kutengana. Hapana! Mimi simaanishi wivu huo.

MSINGI WA MADA YENYEWE
Mada yangu sasa, imeangukia kwa wale ambao huwa wanawalalamikia wenza wao kwamba wana wivu wa kijinga kwao.Naamini si mara moja wala mbili, utamsikia mtu akisema; ‘ah! Yule tuliachana...alikuwa ana wivu wa kijinga sana... yaani mpaka kero...mbaya zaidi mbona mi nilikuwa simwonei wivu?’

TATIZO LA MSINGI LIKO HAPA

Hapa ndipo kwenye kasoro. Kama mwenza wako unamwona ana wivu wa kijinga kwako hapo ndipo pa kupafanyia kazi.Chimbuko la wivu siku zote ni sintofahamu katika uhusiano. Mpenzi wako hawezi kuibua wivu kama kila kitu mbele yake au kwenye akili yake hakina maswali. Wivu huanza na maswali, hufuatiwa na wasiwasi, mwishowe imani hasi.

Kama kweli wewe unajua unazima simu kwa sababu labda una jambo muhimu kwa wakati huo, kwa nini usimjulishe mwenza wako ukijua anaweza kukutafuta?!
Kama kweli hukuwa mahali pasipo na uadilifu, kwa nini umepigiwa simu hupokei kwa muda mrefu. Pengine baada ya kupigiwa zikakatika dakika arobaini na tano hujajibu. Wakati mwenzako anajua kwa kawaida wewe huchezi mbali na simu.

Kama ulikuwa sehemu salama, mwenza wako akikuuliza kwa nini wewe unamwona ana wivu wa kijinga? Kila swali lenye dalili ya wivu kama ni mtu mwadilifu jibu sawasawa na usahihi wako, hakuna sababu ya kumtuhumu mwenzako ana wivu wa kijinga.

Utafiti wangu wa kina umebaini kuwa, katika kila watu kumi wanaodai wenza wao wana wivu wa kijinga, nane ni wasaliti. Madai yao hayo hukinga au ni kwa lengo la kuzuia ugunduzi.

Pengine mtu anaulizwa, ulikuwa wapi? Hana jibu! Kwa nini ulikuwa hupokei simu? Hana jibu! Mbona umechelewa kurudi? Hana jibu! Atajibu nini wakati ukweli anajua alikuwa kwenye mchepuko!!
Tujisahihishe hapa. Kwa wawili wapendanao, kutoka nje ya utaratibu wa siku zote ndiyo chanzo kikuu cha kuibuka kwa wivu na madai kuwa wivu huo ni wa kijinga.

Tukutane wiki ijayo kwa mada nyingine.
GPL

No comments: