ANGALIA LIVE NEWS

Monday, September 14, 2015

Mwanamke wa UAE aishtaki Kenya


Image captionBi Tuweni anasema alipigwa na kutishiwa kubakwa akiwa kizuizini

Mwanamke ambaye ni raia wa Umoja wa Milki za Kiarabu (UAE) ameishtaki serikali ya Kenya, akidai alitekwa nyara na polisi, akapelekwa Somalia na Ethiopia, na kuteswa.

Kamilya Mohammedi Tuweni anasema alitekwa na maafisa wa kikosi maalum cha polisi na kutuhumiwa kuwa ajenti wa al-Qaeda alipokuwa ziarani Kenya mwaka 2007.
Bi Tuweni aliachiliwa huru bila kufunguliwa mashtaka baada ya kuzuiliwa kwa siku 72.

Mkuu wa kitengo cha polisi wa kupambana na ugaidi Kenya amekanusha madai hayo.

Bi Tuweni ameishtaki serikali ya Kenya akitaka alipwe fidia na kuombwa msamaha rasmi kwa dhuluma anazodai alitendewa.

Amekuwa akitoa ushahidi kwa mahakama Nairobi kupitia kiunganishi cha video kutoka London.

Kwa mujibu wa shirika la kutetea haki la Redress lenye makao yake Uingereza, mwanamke huyo alipigwa, kutishiwa kubakwa na alikuwa karibu kuuzwa.

Bi Tuweni, na washirika wake wawili wa kibiashara, walikamatwa wakiwa mi wa Malindi ulioko pwani ya Kenya, karibu na Mombasa.

"Kwa sababu tulionekana kama Waarabu na washirika wangu hawakuweza kuzungumza Kiingereza au Kiswahili lakini Kiarabu pekee, waliamua lazima tuwe magaidi,” Bi Tuweni aliambia BBC mwaka 2007, muda mfupi baada ya kuachiliwa huru.

Wenzake, waliotoka Oman, waliachiliwa huru baada ya kuhojiwa Nairobi lakini yeye anasema alipelewa Somalia na kufungiwa kwenye chumba lililoharibiwa na mizinga.

"Kwa siku 12 tulikaa bila chakula, hata baadhi ya kina mama waliokuwa wajawazito na watoto wachanga waliokuwa nasi.”

Baada ya mapigano kuzidi Mogadishu, anasema alihamishiwa Ethiopia.

Akiwa Addis Ababa, anasema alihojiwa na maajenti wa FBI kabla ya kuachiliwa huru bila kufunguliwa mashtaka yoyote.

No comments: