ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 22, 2015

NGO YA TANZANIA YASHINDA TUZO YA UMOJA WA MATAIFA

Bi. Helen Clark, Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa ( UNDP) akiwatangaza washindi wa Tuzo ya Ikweta ambayo hutolewa na Umoja Mataifa kwa NGO ambazo zinajihusisha na utunzaji wa mazingira, ulinzi na uhifadhi wa misitu, matumizi bora na endelevu ya ardhi na mali asili na kupiga vita umaskini. Tuzo ya mwaka huu wa 2015 ambayo ni dola za kimarekani 10, 000 kwa kila mshindi inakwenda kwa NGO 21 ambapo NGO ya Tanzania ijulikanayo kama Mtandao wa Jamii wa Usimamizi wa Misitu Tanzania ( MJUMITA) ni kati ya NGO sita kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara zilizoshinda Tuzo hiyo. wengine katika picha ni Bi. Christiana Figueres ( UNFCCC) Mcheza senema maarufu na mwanaharakati wa Mazingira Bw. Alec Baldwin na Mkewe Bi. Hilaria Thomas na Bw. Hans Brattsker ambaye ni Mshauri wa UNDP kuhusu wazawa. 

Na Mwandishi Maalum,   New York
Mtandao wa Kijamii wa Usimamizi wa  Misitu Tanzania ( MJUMITA) ni kati ya  Asasi   21 ambazo jana ( jumatatu) zimetangawa kuwa washindi wa Tuzo ya Ikweta (Equator Prize )  kwa mwaka 2015
Tuzo hiyo ya Ikwete hutolewa na  Mfuko wa  Maendeleo  wa Umoja wa Mataifa ( UNDP) kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wanaofadhili tuzo hiyo. Kila   NGO iliyoshinda  Tuzo hiyo inanyakua kitita cha dola 10,000 za Kimarekani.
Ushindi wa MJUMITA pamoja na  NGO nyingine  20 ulitangazwa na   Mkuu wa  UNDP Bi. Helen Clark  katika mkutano wake  na wawakilishi wa   Muungano wa  Waandishi wa Habari wa Umoja wa  Mataifa

Wawakilishi wa  NGO hizo   21 watapokea  Tuzo zao mwezi  Desemba wakati wa Mkutano wa Kimataifa utakaojadili mabadiliko ya Tabia nchi ( COP21) utakofanyika Paris, Ufaransa.
MJUMITA  ni mtandano   wenye wanachama katika  vijiji 450 vilivyopo katika Wilaya 23 za Tanzania na  hujishughulisha na  utunzaji wa misitu, kuwasaidia wanavijiji kupata hati za kimila za kumiliki ardhi, kutatua migogoro inayohusisha masuala ya  ardhi na   kubuni miradi ya matumizi sahihi ya ardhi  pamoja na raslimali za misitu.
Zaidi  ya watu 500,000 wamenufaika na huduma zinazotolewa na  MJUMITA
Akizungumza wakati wa kuwatangaza washindi hao Bi Helen Clark, aliyefuatana na  Bi. Christiana Figueres anayeshughulika masuala ya  mabadiliko ya  tabia nchi na Bw. Alec Baldwin ambaye  ni mcheza  sinema maarufu na mwanaharakati wa mazingira.
Amesema kuwa NGO hizo ambazo zinajihusisha Zaidi na utunzaji wa mazingira, kupambana na  umaskini , utunzaji wa ardhi na  matumizi endelevu  ya ardhi  na misitu wamedhihirisha kwamba    wanalo jambo la kuifundisha Jumuiya ya Kimataifa.
Akaongeza kwamba Zaidi ya  washiriki 100 waliingia katika shindano hilo lakini  21 ndio walioibuka kidedea, huku akisisitiza  kila NGO  ilizoibuka mshindi ina hadhithi ya aina yake   yenye funzo   Jumuiya ya Kimataifa
Akasema  kupitia kazi  nzuri zinazofanywa na asasi za kijamii pasipo kutumia gharama kubwa au teknolojia za  hali ya juu  imedhihirika kwamba kuna   juhudi  ambazo  zinatoa matokeo na watu wengi hasa maskini wanasaidia na hali yao ya maisha inaboreka na  maliasili ikiwamo misitu na ardhi.
Akasisitiza kwamba,  juhudi za  kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ni juhudi mtambuka  zinazopwashwa kumshirikisha na kumjumuisha kila mutual kuanzia mtu wa kawaida ambaye haswa ndiye muathirika mkuu.
Bi. Helen Clark anaongeza kuwa Tuzo hiyo inatolewa katika kipindi ambacho  Viongozi Wakuu wa Nchi na Serikali wanakusanyika  Jijini New York  kwa mkutano wao  maalum wa kupitisha Ajenda 17   za Maendeleo  Endelevu, ambapo    ajenda  namba 13 inazungumzia kwa kina mabadiliko ya tabia nchi wakati ajenda  namba   15  inazungumzia  uhifadhi wa  viumbe anuwai, Misitu na  kukabiliana na  jangwa
Akasema  Mkutano huu wa kupitisha ajenda za maendeleo endelevu zinazochukua nafasi ya malengo ya maendeleo ya millennia yanayomaliza muda wake mwaka huu, unatangulia mkutano mwingine muhimu na unaosubiliwa kwa shauku kubwa ,  mkutano wa Mbadiliko ya Tabia nchi ( COP21)
MJUMITA ni kati ya  NGO Sita kutoka Afrika  Kusini mwa Jangwa la Sahara, zilizojinyakulia tuzo hiyo. NGO nyingine  zilizoshinda Tuzo   Nane  zinatoka   Asia na  Pacific na   NGO nyingine Nane ni  kutoka   Latin Amerika na Visiwa vya Karibbean.   


No comments: