ANGALIA LIVE NEWS

Saturday, September 19, 2015

SERIKALI YA MAREKANI YAZUIA TANZANIA MSAADA WA TRILIONI MOJA

Vitendo vya rushwa vimeendelea kuligharimu taifa baada ya Shirika la Changamoto za Milenia (MCC) kuzuia misaada yake kwa Tanzania yenye thamani ya dola za Marekani milioni 472.8 (Sh. trilioni 1.006).

Taarifa iliyotolewa jana na MCC ilieleza kuwa mkutano wa robo ya mwaka wa Bodi ya Wakurugenzi wa Shirika hilo linalomilikiwa na serikali ya Marekani kwa ajili ya kutoa misaada kwa nchi zinazoendelea ulijadili pendekezo la mkataba mpya na serikali ya Tanzania wenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 472.8 na kuamua kuwa fedha hizo zitolewe baada ya Tanzania kutimiza kigezo cha kuzuia rushwa. Ilielezwa kuwa msaada huo ni maalum kwa ajili ya kuimarisha sekta ya umeme nchini, lengo likiwa ni kuwawezesha Watanzania wengi zaidi kupata nishati hiyo kwa uhakika na kwa bei nafuu.

Kadhalika, ilieliezwa kuwa msaada huo ungehusisha pia uimarishaji wa taasisi zinazohusika na usambazaji wa umeme na usimamizi wake, kusaidia utekelezaji wa mipango ya mageuzi katika sekta ya nishati na kuchochea uwekezaji wa sekta binafsi.

Hata hivyo, taarifa hiyo inaeleza kuwa baada ya mkutano huo uliofanyika juzi (Septemba 17), Bodi ya Wakurugenzi wa MCC ilitoa taarifa rasmi ya kuipongeza Serikali ya Tanzania kwa kufanya mageuzi muhimu kama sehemu ya maandalizi ya utekelezaji wenye ufanisi wa mkataba, lakini haitapewa msaada huo hadi itakapofaulu kigezo cha kiashiria cha kuzuia rushwa (Control of Corruption indicator).

“Pamoja na kutambua mageuzi hayo, Bodi iliendelea kuelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya rushwa nchini Tanzania na kukubaliana kwamba ni lazima kwanza Tanzania ifaulu kufikia kigezo cha udhibiti wa Rushwa (Control of Corruption indicator) katika tathmini ya mwaka 2016 ya jinsi nchi husika zinavyokidhi vigezo vya kusaidiwa na MCC,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, taarifa hiyo ilimkariri Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Mark Childress, akisema kuwa wanafurahishwa na jitihada za serikali ya Tanzania kuinua ufanisi katika sekta ya nishati lakini bado kuna kazi ya kufanywa kwani tatizo la rushwa linaendelea kuathiri karibu kila nyanja.“Tunafurahishwa na jitihada za Tanzania katika miezi kadhaa iliyopita za kufanya mageuzi ya kimuundo na kitaasisi ili kuinua ufanisi, tija na uwazi katika sekta ya nishati.

Hata hivyo, kama ambavyo Bodi ya MCC imebainisha, pamoja na jitihada kadhaa zilizochukuliwa kukabiliana na rushwa, bado tatizo hili limeendelea kuwa kubwa likiathiri nyanja zote za maendeleo na ufanisi katika utendaji wa serikali.”

Taarifa inaeleza kuwa kwa kawaida, shughuli za MCC hufanyika katika msingi wa kuamini kuwa msaada unaotolewa unaleta ufanisi na matokeo makubwa zaidi ikiwa unaimarisha pia utawala bora, uhuru wa kiuchumi na uwekezaji katika watu kwa nia ya kukuza uchumi na kuondoa umasikini.

Kashfa ya Escrow
Katika taarifa yake, Bodi ya MCC haikutaja tukio lolote la rushwa linalowapa hofu katika kutekeleza mktaba huo mpya wa dola milioni 472.8. Hata hivyo, miongoni mwa matukio makubwa yaliyotikisa nchi hivi karibuni ni sakata la fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow, ambalo lilisababisha baadhi ya mawaziri kujiuzulu na vigogo kadhaa kufikishwa mahakamani na wengine kupelekwa mbele ya Baraza la Maadili ya Viongozi wa Umma.

Mpaka sasa mhusika mkuu katika kashfa hiyo Harbinder Singh Sethi bado hajakamatwa na kufunguliwa mashtaka na vyombo husika kama ilivyoagizwa na Bunge mwishoni mwa mwaka jana.

Aidha baadhi ya vigogo toka CCM walihusika katika kashfa hii wamepitishwa na chama hicho mapema Julai kugombea nafasi kadhaa za uongozi ikiwamo ubunge, licha ya baadhi yao kulazimishwa kujiuzulu nyadhifa zao mapema mwaka huu.
CHANZO: NIPASHE

4 comments:

Anonymous said...

Suala la rushwa sawa lakini cha ajabu kipi kitu chenyewe kimeshasemwa ni msaada kweli hapo kuna ishu? Msaada mtu anahiyari yake akusaidie au la. Vile vile misaada ni silaha kubwa kwa nchi za magharibi kulidumaza bara la afrika na kuhakikisha haliwezi kujitegemea bali liwategemee wao kwani misaada mingi inayotolewa na nchi hizi hailengi sehemu za maendeleo ya nch na wananchi wake hasa na siku zote riba zake huishia kuwa kubwa kuliko misaada yenyewe na kwa kweli nchi yenye kujitambua haiwezi kujiendesha kwa mutegemea misaada hasa kutoka nchi kama marekani utanynyasika tu. Kuhusu tuhuma za rushwa na ufisadi na watuhumiwa kupitishwa kugombea nafasi za juu za nchi kwa kweli naona baada ya kuenda mbele na kuutokomeza ufisadi tuna rudi nyumba na kuukumbatia ufisadi hasa baada ya vyama vya upizani chini ya mwamvuli wa ukawa kumsinamisha miongoni mwa wa watuhumiwa waliosababisha ubadhirifu wa mabilioni ya pesa ya kutisha kuwahi kutokea katika historia ya Tanzania na la kushangaza zaidi hao hao upinzani kipindi cha nyuma kidogo tu ndio waliokuwa wakiwatahadharisha watanzania kwamba ikiwa CCM watajitoa fahamu na kumpitusha ngugu Lowasa kama mgombea wao wa uraisi basi wamkatae na waikatae CCM na waidhibu katika uchaguzi mkuu kwa kutoichagua na hawakuishia hapo tu bali chadema waliwaahidi watanzania kwamba ikiwa CCM watamsimamisha Lowasa kuwa mgombea wake wa uraisi wao wanazunguka nchi zima kupinga kitendo hicho kwani ni aibu mtu kama Lowasa aliepaswa kuwa ndani ya mikono ya sheria kuona kuwa anazawadiwa nafasi ya juu uongozi iliotkuka ya nchi yetu walisema wao watakuwa tayari kufa nae kuhakikisha hawi raisi wa nchi hii sasa leo hizo kauli kali za upizani zidi ya lowasa na ufisadi zimeishia wapi? Badala yake wanazunguka nchi zima kujaribu kumsafisha huo ni utapeli wa hali ya juu wa kisiasa kwa watanzania kuwahi kufanyika nchini.

Anonymous said...

Anonymous 11:43 Nini tofauti ya msaada na mkopo? baada kupongeza juhudi za kukomesha rushwa na ufujaji wa fedha na mali ya asili unaofanywa na baba zako (CCM) unaleta ubabaishaji na Sera zilezile mlizozoea za wizi lol

Anonymous said...

kutia ulimi puanu sio pahali pake, ulimi pahali pake ni mdomoni,ikizungumziwa ESCROW ina wahusika ambao wanjulikana kwa majina, na leo ndio ambao chama chao kimewasimamisha kugombea ubunge, hao ndio wanozungumziwa, usipotesha chama tawala huko ndiko kinakotupeleka, wameshindwa kutuletea maendeleo na hata misaada wana wanaifanya isitishwe. pia jaribu kujua tofauti ya msaada ya mkopo, amerika kuna shule za bure, kavute ujinga usiwafanye watanzania wajinga

Unknown said...

Nyinyi waswahili mkikopeshana mnaita mkopo wala hamtiliani riba katika makoposheni yenu. Kwa wazunngu kukukopesha maanake anakusaidia wewe kwa akili zako za madafu kuna mtu atakaekupa pesa bure bila ya yeye kunufaika na chochote ? Labda hizo ni akili za watu wanaojiita watu wa mabadiliko kwamba Lowasa akiwa raisi atakuwa akiwagaia mahela bure bila kufanya kazi upambavu wa kufikiri huo. Mimi binafsi licha ya umaskini wangu sitegemei mtu aje mtu kunipa msaada bure bure tu bila yeye kutagemea something in return huku ulaya hakuna kitu kama hicho . Mtu si ndugu yako au jamaa yako pengine hata si rafiki yako halafu unategemea aje akusaidie tena bure ? Haiwezekani na kama tunamawazo kama hayo si shangai waafrika tuanabakia watu wa kuomba tu na tutaendelea kuwa hivyo mpaka tubadilike.