ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 10, 2015

Ukawa: Tanganyika yaja.

Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) umeahidi kuwa kama utashinda katika Uchaguzi Mkuu wa mwezi ujao, utarejesha serikali ya Tanganyika.

Kauli hiyo ilitolewa mjini Zanzibar jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya mgombea urais wa Zanzibar kupitia Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Sharif Hamad, katika uwanja wa Demokrasia.

Maalim akihutubia umati wa wananchi katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na mgombea wa Ukawa wa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa, alisema wakishinda wataunda serikali ya muundo wa serikali tatu kama ilivyopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Mstaafu, Joseph Warioba.

Tume hiyo iliyokusanya maoni ya wananchi na kuandaa rasimu ya katiba mpya, pamoja na mambo mengine, ilipendekeza muundo wa serikali tatu yaani ya Tanganyika, Zanzibar na ya Muungano.

Hata hivyo, Bunge Maalum la Katiba (BMK) lililokuwa na wajumbe wengi kutoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) lilitupilia mbali mapendekezo hayo na kupitisha katiba inayopendekezwa inayopendekeza muundo wa sasa wa serikali mbili ya Muungano na Zanzibar uendelee kwa maelezo kuwa ndiyo utakaowezesha Muungano udumu zaidi.

Maalim Seif alisema pamoja na wananchi kutaka Muungano wa serikali tatu kupitia Tume ya Katiba Mpya, lakini CCM) ilisaliti maoni hayo na kutengeneza ya kwao ambayo hayakutokana na maoni ya wananchi.

“Ninasema kwamba mimi na Lowassa tukiingia madarakani, tutawahakikishia Watanzania kwamba ni lazima tutarejesha rasimu ya Warioba, Bunge la Katiba litafanyika chini ya serikali yangu na Lowassa ili turejeshe maoni waliyotoa wananchi kwa kuunda Zanzibar inayojitegemea, Tanganyika inayojitegemea na serikali ya Jamhuri ya Muungano,” alisema.

Kadhalika, Maalim Self, alisema jambo la kwanza atakalolifanya ikiwa atachaguliwa kuiongoza Zanzibar, ni kulinda maslahi ya Wazanzibari.

Alisema akiingia madarani atahakikisha Zanzibar inapata mamlaka kamili na kuwa licha ya kwamba Zanzibar inaongozwa na Serikali ya Umoja wa Kitaifa, lakini cha inaongozwa na maamuzi kutoka CCM.

Pia aliahidi kuwa atalinda misingi ya utawala bora na kwamba hatakubali kuona utu wa Wazanzibari unadhalilishwa.
“Mambo ya watu kuvaa soksi usoni mwisho ni Oktoba, siwezi kukubali kuona utu wa mtu unadhalilishwa, ni lazima nitapigana kukomesha mambo haya,” alisema.

Vilevile, alisema atahakikisha mahakama za Zanzibar zinapewa nguvu ili watu wanaohukumiwa washughulikiwe na mahakama za Zanzibar na si kupelekwa nje ya Zanzibar.

Aliahidi kuwa Masheikh walioshitakiwa kwa ugaidi Tanzania Bara watarudishwa kushtakiwa Zanzibar na kwamba siyo sahihi kuifanya Tanganyika kama Gwantanamo.

Jambo jingine alilosema atalifanya akiingia madarakani ni kujenga uchumi imara na unaokua kwa kasi na kuifanya Zanzibar kama Singapore ya Afrika Mashariki na kwamba hiyo ndiyo ndoto yake.

Kadhalika, alisema atahakikisha anajenga bandari ya kisasa ambayo itakuwa inachukua mizigo mikubwa kutoka nchi mbalimbali zikiwamo Burundi na Rwanda.

Kingine alisema atafungua Uwanja wa Ndege wa Zanzibar ambao ujenzi wake haujakamilika hadi sasa.

Kadhalika, Maalim Seif aliahidi kufungua benki ya uwekezaji ya Wazanzibari ambayo alisema itakuwa inatoa mikopo na mitaji kwa vijana, akina mama, wavuvi, wakulima kwa masharti nafuu kwa lengo la kupunguza tatizo la ajira.

Maalim Seif aliongeza kuwa, ataunda wizara ya kushughulikia mafuta na gesi, pamoja na kuunda sheria na sera za kusimami uchimbaji wa nishati hizo ndani ya siku 100 baada ya kuapishwa.

LOWASSA
Kwa upande wake, Lowassa alilaani kitendo cha mahasimu wao kubandua mabango yao na kuyatupa porini.
Alisema kitendo hicho ni ukiukwaji wa haki za raia, na kuwataka waache mara moja.

Aidha, Lowassa alisema pamoja na kufanyiwa yote hayo, lakini aliwahakikishia Watanzania kuwa hakuna atakayewaibia kura Oktoba 25, mwaka huu kwa kuwa uwezo wa kuzilinda wanao.

Pia aliwataka Watanzania wasidanganyike na kauli zinazotolewa na CCM kwamba wakiwapa kura wapinzani kuongoza serikali kutatokea vurugu.

“Msidanganyike na kauli inayotolewa na CCM kwamba mkiwapa wapinzani kuchukua dola kutatokea vurugu, hakuna kitu kama hicho, wambieni waache umbea,” alisema.

“Ninaomba muwe na msimamo katika kipindi hiki, msidanyike na jambo lolote, mvumilie mpaka mwisho ili mchukue dola,” aliongeza na kuwataka wananchi wamchague Maalim Seif kuwa rais wa Zanzibar.

Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni mgombea mwenza wa Lowasa, Juma Duni Haji; Kaimu Mwenyekiti wa CUF, Twaha Taslima; Katibu Mkuu wa NCCR-Mageuzi, Mosena Nyambabe na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zanzibar, Salum Mwalimu.

HALI ILIVYOKUWA
Mkutano wa uzinduzi wa kampeni hizo ulihudhuriwa na umati wa wanachama na wapenzi wa CUF, viongozi wa Ukawa na wananchi.

Pia ulipabwa kwa rangi nyekundu, bluu na nyeupe za chama hicho, sambamba na burudani mbalimmbali.
Msaanii maarufu wa tarabu asilia, Abdallah Issa, alitumbuiza kwa wimbo maalumu.

Licha ya jua kali lililokuwapo katika viwanja hivyo, wananchi walianza kuwasili tangu majira ya asubuhi.

Imeandikwa na Rahma Sulaiman, Zanzibar; Elizabeth Zaya na Hussein ndubikile, Dar
CHANZO: NIPASHE

2 comments:

Anonymous said...

A whole lot of malarkey and wishful thinking!

Anonymous said...

Tunajua siku zote Maalim amekuwa anataka kuvunja muungano wetu.