ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, September 10, 2015

WASOMI WANAHARAKATI WAMSHUKIA GWAJIMA

Dar es Salaam. Baada ya Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima kuibua mambo mazito ya aliyekuwa Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa juzi, wanaharakati na wasomi wametoa maoni yao na kueleza kusikitishwa na hatua za kiongozi huyo wa dini kutoa siri za waumini wake.

Wanaharakati hao pia wameiomba Serikali ipige marufuku viongozi wa dini kujihusisha na siasa.

Juzi, Gwajima alizungumza na wanahabari Dar es Salaam, alisema Dk Slaa amestaafu siasa kwa sababu ya shinikizo la mkewe, Josephine Mushumbusi.

Kiongozi huyo machachari wa dini katika mazungumzo yake na waandishi wa habari, alipinga kauli iliyotolewa na Dk Slaa, kwamba amejiuzulu siasa kwa sababu chama chake kimekiuka makubaliano kwa kumkaribisha Edward Lowassa.

Kadhalika, Gwajima alikwenda mbali na kudai Mushumbusi alimfukuza na kumrushia Dk Slaa nguo zake, akimtaka ajiuzulu Chadema hali iliyosababisha katibu mkuu huyo wa zamani kulala ndani ya gari.

Gwajima aliyasema hayo wakati Dk Slaa na familia yake wakiwa safarini kuelekea Marekani kwa mapumziko, huku akisema kurejea kwake kutategemea mazingira ya wakati husika. Dk Slaa aliaga kupitia Televisheni ya Azam katika mahojiano maalumu.

Wasomi na wanaharakati

Aliyekuwa Mkuu wa Chuo Kikuu Huria (OUT), Profesa Tolly Mbwete aliwataka Gwajima na Dk Slaa kuachana na masuala ya kupambana kwenye majukwaa, badala yake aliwataka waongelee masuala ya maendeleo.

“Hao wazee waachane na hayo mambo, ni mfano mbaya kwa vijana. Waongee masuala ya kimaendeleo, wanatutia aibu sisi wazee wenzao,” alisema.

Mkazi wa Magumuchila, Masasi mkoani Mtwara, Julius Mazinde alisema vita hiyo ya maneno kati ya watu wawili ambao ni viongozi wa kiroho, inatia shaka na inatishia amani ya nchi.

“Unajua Gwajima ana wafuasi na Dk Slaa ana wafuasi wengi, haya malumbano yao yakizidi, wanaweza kufika pabaya ikaleta machafuko, lakini sisi tunaombea hilo lisitokee,” alisema.

Mazinde alimsihi Gwajima kukaa kimya iwapo Dk Slaa atajibu lolote, pia, alimuomba Dk Slaa asijibu chochote ili kuepusha kuchochea malumbano zaidi.

Serikal ipige marufuku

Kuhusu viongozi wa dini kutoa siri za waumini wao, kwa mfano Gwajima alipotamka kuwa Mushumbusi ana mapepo, Mkufunzi wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM), Dk Eliamani Sedoyeka aliishauri Serikali kupiga marufuku viongozi wa dini kujiingiza katika siasa.

Alisema imekuwa bahati mbaya kuwa viongozi wetu wanachanganya siasa na dini, hali ambayo aliitaja kuwa ni kufilisika.

“Kikubwa mimi sioni kama kutaja zile siri za Dk Slaa kuna mashiko, kwanza Serikali haiamini kuhusu mapepo, haina dini,” alisema.

Alizungumzia pia malumbano ya Dk Slaa na Chadema na kusema hatua zinazofikiwa na baadhi ya viongozi hao, zinawakatisha tamaa wananchi na kuleta taswira mbaya kwa wapiga kura wao.

Alimtaka Askofu Gwajima afute usemi wake kuhusu Dk Slaa na kumsihi Dk Slaa ajisafishe kuhusu tuhuma zake kwa maaskofu.

Akizungumzia hilo, Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo Bisimba alisema kutokana na nafasi ya Gwajima nchini, yaani uaskofu, hakutakiwa kutoa siri za Dk Slaa, bali alitakiwa kujikita kujibu hoja za kuitwa mshenga, kujibu kama amehongwa au hakuhongwa na kujibu tuhuma za maaskofu.

“Kimaadili si vizuri kutoa siri hizo, angeweza kujibu bila kutaja mambo mengine kama masuala ya mapepo, kutokana na nafasi yake si vizuri alivyofanya”alisema.

Alisema kuwa Gwajima alikwenda kinyume na maadili ya kazi yake ya utumishi wa Mungu kwani si jambo jema kueleza siri za muumini kuwa anamapepo.

Maswali kwa Gwajima

1. Kwa nini walinzi wa Gwajima wanamlinda Dk Slaa? Je, Gwajima ana kampuni ya ulinzi.

2. Gwajima anamiliki silaha ngapi? Ni silaha za aina gani? Na kwa nini amiliki silaha nyingi?

3. Kwa nini anatoa siri za waumini wake kuwa wana mapepo?

4. Kwa nini alikuwa anarekodi kila kitu alichozungumza na Mushumbusi na Dk Slaa?

5. Je, kuna utata wa tarehe ya ujumbe mfupi uliyotumwa na Dk Slaa kwa Gwajima na tarehe ya Lowassa kuondoka CCM.

6. Kwa nini ana ulinzi mkubwa unaotia shaka?

MWANANCHI

7 comments:

Anonymous said...

SLAA PIA NI MTUMISHI WA MUNGU, MBONA ALIONGEA MENGI SANA AMBAYO HAYASTAILI KWAKE KM MTUMISHI,

Anonymous said...

aliyeaza haonekani mbaya, mbaya anaonekana anayemaliza mmmm kwahili siwaungi mkono kabisa, aliyataka mwenyewe slaa wacha yamkute

Anonymous said...

HAKIKA MTUMISHI ANAHITAJI KUMJUA MUNGU ZAIDI NA KUMTUMIKIA YEYE KAMA KWELI ALIPATA WITO WA KUMTUMIKA BWANA,KWA MAANA MTUMISHI WA MUNGU HUENDI KWA JINSI YA MWILI ILA HUONOZWA KWA ROHO WA BWANA!HUENENDI KWA KUJISIFU MBELE YA WATU BALI MATENDO YAKO MAZURI MBELE ZA MUNGU!UNASHUHUDIA UKWELI KWA MUNGU SI KWA MWANADAMU MAANA NI YEYE AKUJUAE KULIKO MWANADAMU!INATUPASA KUKOMAA KIROHO KWA KUIGA MITUME ILIYOTANGULIA,WALIVUMILA,WALITESWA,WAZUSHIWA LAKINI WALIONGOZWA NA ROHO WA MUNGU KWANI HAWAKUJIBU WALA KURUDISHA KISASI!WALIZIDISHA UPENDO NA WALA HAWAKULINDWA NA JEHI,WALIMTEGEMEA MUNGU!MTUMISHI WETU HUYU AJITATHIMINI MWENYEWE KAMA JE AMPIGIE MAGOTI MUNGU WAKE KWA KUSHUHUDIA OWONGO,TETESI,MAJUNGU AMA LAH!PUNGUZA MAADUI,ONGEZA MARAFIKI

Anonymous said...

Kaka uko sahihi!mambo ya kuwatangaza waumini wake kuwa wanamapepo wengine waliokwenda pake si watangazwa pia?kakosea!kama mwrnzake anaonekana kamkosea angeomba mungu amsaidie!yeye mwenyewe alimrudhia maneno makali mtumishi wa mungu awaki na hadi leo anajesi ya kujibu mwenzie mbona alisema nimemsamehe?nadhani ni mwanasiasa sio mtumishi hivyo anpe kaisali yaliyo ya kaisali

Anonymous said...

NI KWELI,AAMUE MOJA ASITUCHANGANYE HAPA NA SIASA-DINI.KWANZA NI MCHUNGAJI ANAMWAMINI MUNGU SILAHA ZA NINI?ANAJILINDA KIMWILI AMA KIROHO!ALIWAHI KUMKASHIFU MTUMISHI WA BWANA HAPO AWALI HAKUMJIBU CHOCHOTE ZAIDI YA KUSEMA AMEMSAMEHE NI KWAVILE ANAMAFUNDISHO YA MUNGU NA KAKOMAA KIROHO!GWAJIMA ANADILIKI KUULIZA ETI NANI MJANJA KATI YAKE NA DR SLAA!!!JAMANI,KUNA UJANJA UJANJA KATIKA UTUMISHI?

Anonymous said...

Mwaga yote askofu
Wewe mtu wa mungu wala si wa CCM Wala Ukawa
Unasema kweli
Mungu akulinde

Anonymous said...

gwajima si askofu ni msanii