Aliyekuwa Mbunge wa Ludewa kwa tiketi ya CCM, Deogratias Filikunjombe, enzi za uhai wake akipanda chopa yake.
Nakupenda Deo
Nimesikitishwa sana na kifo chako. Kweli kifo kipo na kila mmoja wetu atakipitia lakini cha aina hii, cha kijana aliyekuwa akipigania watu wake kiasi hiki? Kinaumiza sana, hata hivyo, hatuna budi zaidi ya kukubali kuwa Deo Filikunjombe, jembe la mkono limeondoka.
Chopa iliyosababsha kifo cha Filikunjombe, Capt. William Silaa na watu wengine wawili.
Nasema kutoka ndani ya moyo wangu, taifa limepoteza mtu muhimu sana, hakusita kupigania alichokiamini bila uoga wala hofu! Wakati mwingine alitofautiana na msimamo wa chama chake kwa maslahi ya Watanzania maskini, kwako ukweli ulikuwa nguzo. Nenda Deo, nenda kapumzike muda si mrefu tutaungana nawe, kila mwanadamu atafariki dunia maana ndivyo ilivyoandikwa.
Lakini cha muhimu ni mtu atakuwa anafanya nini wakati anakufa! Je, atakuwa akiiba au akifanya uzinzi? Deo umekufa ukitumikia watu wako, umekufa kifo chema na Wanaludewa watakuombea. Nenda Deo, pumzika Deo, mema yako yamekutangulia.Hayo ndyo yatakutetea mbele ya Maulana! Mwisho nasema kwa uchungu na ninakuahidi, pale ulipoishia, sisi tutaendelea bila kujali tupata nini mpaka siku moja wananchi wa taifa hili wafaidi mema ya nchi yao.
Nenda Deo, kapumzike kwa amani, umekufa katika mapambano. Natoa pole kwa familia yako, mkeo, watoto, wazazi na wananchi wote wa Jimbo la Ludewa, msiumie sana, Mungu anajua ni kwa nini ameamua jambo hili litokee. Naamini Deo yuko mahali sahihi, kutokana na kile alichokuwa akikifanya wakati anakutwa na mauti, kwetu sisi, kibinadamu ni maumivu lakini kiimani, Deo yuko mahali salama. Nenda kaka Deo. Pumzika kwa amani kaka!
Eric James Shigongo,
Mkurugenzi, Global Publishers Ltd.
Nenda kamanda wangu Deo
No comments:
Post a Comment