ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 27, 2015

JWTZ yavamia kijiji kuondoa vizuizi barabarani



Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi.
By Lauden Mwambona na Justa Musa

Mbeya / Tukuyu. Vijana wa Jeshi la Wananchi jana walivamia nyumba za wananchi waliokaribu na barabara kuu ya kutoka Mbeya kwenda Malawi katika wilaya ya Rungwe na kuwataka waamke kuondoa vizuizi vya moto, magogo na mawe vilivyokuwa kwenye barabara hiyo.

Kazi hiyo ilifanywa baada ya vijana wanaodaiwa kuwa wafuasi wa Ukawa kuweka vizuzi vya moto, magogo na mawe kwenye barabara hiyo ikiwa ni ishara ya kupinga matokeo ya uchaguzi katika jimbo la Rungwe.

Wanajeshi walifika Kijiji cha Ndaga saa 4.00 usiku ambako waliyakuta magari yakiwamo mabasi sita yaliyoshindwa kuendelea na safari ya kwenda Tukuyu, Kyela na Malawi baada ya kuwekewa vizuizi.

Vijana wa Jeshi la Wananchi waliamua kutembea kutoka Ndaga hadi Tukuyu wakitoa vizuizi na kuwaamsha wananchi walio karibu na barabara ili washiriki kazi hiyo huku wakitoa kichapo kwa waliokuwa wakichelewa kuamka.

Waliopigwa ni pamoja na wagonjwa na wazee kadhaa wakiwamo wachungaji ambao walikutwa wamelala usiku huyo.

Kiongozi mmoja wa Kijiji cha Katumba ambaye aliomba jina lihifadhiwe alisema hatua ya jeshi ilitokea baada ya vijana wanaodaiwa kutoka Mbozi,Tunduma na Mbeya mjini wakishirikiana na wafuasi wa Ukawa kufanya vurugu tangu saa 10,00 jioni ya juzi baada ya kutangazwa matokeo ya ubunge katika Jimbo la Rungwe.

Naye mkazi wa Kijiji cha Kiwira Tujobe Mwakipu alisema vijana hao walifanya vurugu bila kuzuiwa na wanasiasa waliogombea ubunge.

Alisema vurugu zilianza baada ya kutangazwa matokeo ya Ubunge ambayo yalimpa ushindi mgombea wa CCM, Saul Amon kwa kura 47,862 akimshinda mpinzani wake wa karibu, John Mwambigija aliyepata kura 43,613.

Alisema vurugu zilianzia Tukuyu mjini ambako vijana walikusanyika kudai matokeo na yalipotangazwa hawakuridhika na kuanza kuchoma barabara kuanzia saa 10 ya jioni.

Akizungumzia yaliyowakuta wazee ,John Mwampi wa Kijiji cha Ntokela alisema usiku wa kuamkia jana wananchi wengi walipigwa na wanajeshi waliovamia nyumba zao kuanzia saa 7.00 usiku hadi 12.00 asubuhi walipomaliza kazi ya kuondoa vizuizi kwenye barabara kuu hiyo maeneo ya Ndaga, Ntokela, Kiwira, KK, Mwabegele na Katumba.

Mwampi alisema wanajeshi walifika eneo la KK saa 10.30 na kuwaamsha kwa bakora wananchi wenye nyumba zilizo karibu na barabara huku wakiwataka wakatoe mawe, magogo na moto uliokuwa ukiwaka katikati ya barabara.

Naye Mchungaji Yesaya Kilindu wa kitongoji cha Ntupwa katika Kijiji cha KK wilayani Rungwe alisema wanajeshi waliingia kwenye nyumba yake saa 10.00 usiku na kuanza kuwatandika bakora huku wakiwaamuru wakaondoe mawe na magogo kwenye barabara kuu.

‘’Walituchapa sisi na pia walikwenda nyumba ya Mwalimu chaula ambako waliwapiga na kuiba simu yenye tamani ya Sh200,000’’, alisema na kufafanua kwamba tukio hilo lilikuwa baya.

Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Moses Mashaka alipoulizwa alisema kamati ya usalama ya wilaya ilikuwa ikiendelea kufuatilia nyenendo za vijana na kwamba haikuwa na taarifa za kutoa kwa vyombo vya habari.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa Ahmed Msangi alipoulizwa alisema polisi waliwadhibiti vijana waliofanya vurugu na kuwakamata kadhaa, lakini alisita kuzungumzia zaidi akisema bado wanawasaka wengine.

Mwananchi

2 comments:

Unknown said...

Tunasema vurugu zote zinazotokea sasa ni mazalio ya kauli za viongozi wa chadema na ukawa kuwaaminisha wafuasi wao kuwa hata wakishindwa kihalali watakuwa wameibiwa kura yaani ni ujinga juu ya umbavu kwa washindani wawili mmoja atokezee kuamini ni yeye tu ndie mwenye haki ya kushinda. kwa msingi huo ukawa na chadema wametengeza viungo vya kuliingiza taifa kwenye machafuko. Mbona CCM wanashindwa ubunge tena kwa karibu zaidi kitakwimu na wameyakubali matekeo bila vurugu na hata kuwashangaza wapinzani kwa kuwapigia simu za kuwapongeza kwa ushindi tumeona mgombea wa CCM kule moshi katika uchaguzi ulio kuwa wa ushindani kweli kweli lakini yule Mosha baada ya kushindwa alimpigia simu mpinzani wake na kumpongeza kwa ushindi na kumuomba radhi yaliotokea wakati wa kampeni ingawaje wao chadema ndio waliopaswa kuomba radhi kutokana na vitendo vyao kihuni waliowafanyia CCM. Ukawa wafahamu kuwa siasa si uadui na anaeamini kuwa katika mashindano ni yeye tu mwenye haki ya ushindi ni muhalifu wa fikra na hizo fikra zake wakati wowote zitampelekea kuzitumia kivitendo ili kutenda vitendo viovu. Tunaomba ili kuepusha machafuko yasiyoyalazima viongozi wa ukawa/chadema wawatulize wafuasi wao waachane na vitendo vya uvunjifu wa sheria na amani la sivyo msije kulilaumu jeshi la police na vyombo vya usalama kwamba watu wenu wanaonewa.

Anonymous said...

Sawa msemaji wa CCM. Napenda sana maelezo yako. Je unaweza kutafuta fursa ukatutolea ufafanuzi wa kinacho endelea huko Znz?
Ni siku ya Tatu sasa baada ya uchaguzi na hatujapata jibu lolote. Lakini tumesikia maelezo ya Maalim seif. kuna kigugumizi gani cha kutangaza mshindi Zenji kama si kuandaa mazingira ya kughushi na the kusababisha fujo?
Tusaidie maelezo mkuu.